Writen by
sadataley
1:40 PM
-
0
Comments
Rais Jakaya Kikwete (katikati) akipita kwenye daraja la waenda kwa miguu la Mabatini, Mwanza jana, baada ya kulizindua, daraja hilo limeghalimu kiasi cha sh8bilioni litasaidia kuondoa tatizo la ajali zilizokuwa zikitokea mara kwa mara eneo hilo. kushoto ni Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli. Picha na Michael Jamson
Na Aidan Mhando, Mwananchi
Mwanza. Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje jana amebadilisha upepo kwenye mkutano wa Rais Jakaya Kikwete, kwa kueleza kuwa miradi yote ya Serikali ni fedha za wananchi.
Wenje alisema hayo alipopewa nafasi ya kuzungumza kwenye viwanja vya Mabatini mkoani hapa, akidai kuwa miradi yote inayotekelezwa na Serikali ni kodi za wananchi wala siyo fedha za CCM.
Wenje alitoa kauli hiyo mbele ya Rais Kikwete baada ya Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli kudai kuwa CCM ndiyo inayotekeleza miradi yote ya maendeleo kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Rais Kikwete alikuwa akizindua daraja ya Mabatini lililojengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh1 bilioni na Kampuni ya Adivance Life.
Kabla hajazungumza Wenje alipopanda jukwaani hapo, mamia ya watu waliohudhuria uzinduzi wa daraja hilo walianza kupiga kelele huku wakishangilia kwa kuonyesha ishara ya vidole viwili juu na kuimba ‘Peoples Power’.
Baada ya mbunge huyo kuanza kuhutubia alisema: “Naomba nimjibu Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli kwamba miradi hii siyo yaCCM, bali ni kodi za Watanzania wakiwamo, wakulima, polisi, wafanyabiashara, hivyo asitambe hapa kuwa hii ni nguvu ya CCM siyo kweli hata kidogo.”
Wenje akihutubia kwa jazba alisema kuwa yeye siyo mtu wa kawaida na hana chembe ya CCM wala wasitegemee kuwa yeye ni muumini wa chama hicho.
Alitoa mfano kuwa yeye siyo kama tikiti maji kwamba nje lina rangi ya kijani, lakini ndani lina rangi nyekundu, na kwamba ataendelea kupiga kelele ili CCM waendelee kufanya mambo ya maendeleo, kwani bila hivyo hawawezi kufanya lolote.
Kabla Wenje hajamaliza kuhutubia mkutano huo aliwataka wananchi hao kukunja ngumi ili waagane kwa salamu yao.
“Mheshimiwa Rais hapa Mwanza tuna salamu zetu naomba niage kwa salamu hiyo, haya ndugu zangu naomba tukunje ngumi, koroga koroga, peoples,” alitamka na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo wakaitikia ‘Power’ huku wakinyoosha vidole viwili juu.
Hali hiyo ilisababisha wafuasi wa CCM kuibuka na kuanza kusema CCM oyee, jambo lililosababisha wafuasi hao kuanza kutupiana maneno na kupiga kelele na kusababisha watu kutosikilizana.
Hatua hiyo ilisababisha askari polisi waliokuwa wamevalia sare kuongezwa kwenye uzinduzi huo ili kuimarisha ulinzi.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Wenje-abadili-upepo-mkutano-wa-JK/-/1597296/2482520/-/v34cuc/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Wenje-abadili-upepo-mkutano-wa-JK/-/1597296/2482520/-/v34cuc/-/index.html
No comments
Post a Comment