Writen by
sadataley
2:50 PM
-
0
Comments
Mjumbe wa Bunge la Katiba (Chadema) Said Arfi akisaini karatasi ya
mahudhurio bungeni jana, kabla ya kwenda kushiriki mjadala wa kamati
yake . Picha na Emmanuel Herman
Na Neville Meena na Sharon Sauwa, MwananchiDodoma. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
amesema chama chake hakitavumilia vitendo vya usaliti na kwamba
mwanachama yeyote atakayekiuka maagizo ya chama hicho atachukuliwa hatua
kali.
“Katika hili hatutakuwa na mchezo na naomba niweke
wazi kabisa kwamba usaliti hausameheki. Tuna vikao vya chama vinakuja
siku za karibuni mtu yeyote ambaye atabainika kusaliti uamuzi wa chama,
uwe wa Kamati Kuu au mwingine wowote, tutachukua hatua hata kama ni
kumfukuza uanachama,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo alikuwa akizungumzia taarifa za
kuwapo bungeni, Dodoma kwa baadhi ya wanachama wa Chadema, kinyume cha
makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wabunge hao ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu),
John Shibuda (Maswa Mashariki) na Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye
aliwasili jana na kwenda kushiriki kwenye kikao cha kamati namba 10
kilichokuwa kikifanyika Ukumbi wa Internet, Chuo cha St. Gaspar.
Mbowe alisema baada ya viongozi wakuu wa Ukawa
kukubaliana kwamba hawatashiriki katika awamu ya pili ya Bunge Maalumu,
kila chama kiliwaelekeza wabunge wake kuhusu msimamo huo ambao pia
uliridhiwa na vikao vya vyama husika.
“Sisi suala hili limepitishwa na Kamati Kuu ya
Chadema, sasa wewe ni nani kukataa, kupinga au kwenda kinyume cha
matakwa ya Kamati Kuu? Ole wake mtu atakayethubutu kushiriki hivyo vikao
vya Kamati za Bunge,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wakati tunagombea ubunge 2010 hakukuwa na ahadi
kwamba kutakuwa na Bunge la Katiba, hili limetokea tu, sasa kama sisi
kwa masilahi mapana ya umma tunauona mchakato hauko sawa, kwa nini wewe
ulazimishe kushiriki, unakwenda Dodoma kumwakilisha nani?”
Vyama vingine vyenye wabunge ambavyo pia wanachama
wake wamesusia Bunge Maalumu ni NCCR Mageuzi na CUF. Kadhalika
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila ni miongoni mwa
waliosusia vikao hivyo.
Kauli ya Arfi
Akizungumzia uamuzi wa kushiriki Bunge alisema
licha ya kwamba yeye ni mwanachama wa Chadema, ameingia bungeni akiwa
mwakilishi wa wananchi katika kutunga Katiba na kwamba ndani ya Bunge
hakuna vyama, bali wawakilishi wa wananchi.
Alisema anaamini katika muungano wa Serikali tatu
na kwamba kama kuna mgongano uliojitokeza lazima uamuliwe ndani ya
mkutano wa Bunge na kwamba kutoka nje ya Bunge ni dalili ya woga na yeye
siyo mwoga.
“Ndiyo nipo kwenye kikao cha kamati namba 10, hivi
sasa hatujamaliza,” alisema Arfi kupitia ujumbe mfupi wa simu yake ya
mkononi baada ya mwandishi wetu kumuuliza jana.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Mbowe--Usaliti-hauna-msamaha/-/1625946/2412232/-/pxjl83z/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/Katiba/Mbowe--Usaliti-hauna-msamaha/-/1625946/2412232/-/pxjl83z/-/index.html
No comments
Post a Comment