Writen by
sadataley
6:56 PM
-
0
Comments
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana. Picha na Maktaba
Na Neville Meena, Mwananchi
Dodoma. Katika jitihada za kuliepusha Bunge la Katiba kupoteza
mwelekeo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wajumbe wake kuacha
kumjadili mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
waliosusia vikao vya Bunge hilo.
Badala yake, CCM imewaelekeza wajumbe hao kujadili “mambo yanayowahusu wananchi” ambayo yamependekezwa katika Rasimu ya Katiba.
Maelekezo hayo yalitolewa na Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana alipokutana na wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni
wabunge wa Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
pamoja na wale walioteuliwa kuingia katika Bunge hilo kupitia wajumbe wa
kuteuliwa na Rais kupitia kundi la 201.
Kikao hicho ambacho kilifanyika katika Ukumbi wa
Mikutano wa CCM Makao Makuu, pamoja na mambo mengine pia kiligusia
mwenendo wa Bunge la Katiba, huku Kinana akitoa maelezo mafupi
kuwahakikishia msimamo wa chama hicho kwamba kinaunga mkono hatua za
kuendelea kwake katika awamu ya pili.
Maelekezo hayo yamekuja baada ya wajumbe hao
kutumia muda mwingi wa siku ya kwanza ya awamu ya pili ya Bunge la
Katiba, kuwashutumu wajumbe wa Ukawa kwa kususia vikao, wakiwaeleza kuwa
mwafaka unaweza tu kupatikana ndani ya chombo hicho cha kuandika
katiba.
Wajumbe hao walidiriki hata kutafuta mfumo wa kuwazuia wajumbe hao wa Ukawa kuzungumzia Katiba wakiwa nje ya Bunge Maalumu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambazo gazeti
hili lilizipata zinasema wajumbe hao walimwomba Kinana kuwa Ukawa na
Jaji Warioba wazuiwe kujadili Katiba nje ya Bunge.
Kinana, akijibu hoja hiyo katika kikao hicho
kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema
wajumbe hao wa CCM hawapaswi kulumbana na watu walioko nje ya Bunge na
asingependa kusikia wakiwataja Ukawa wala Warioba wakati wakichangia
bungeni.
Kadhalika Kinana alisema chama hicho hakiwezi
kushawishi kuzuiwa kwa mikutano wala mijadala inayoendeshwa nje ya Bunge
Maalumu la Katiba.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa suala hilo la wajumbe
wa Ukawa na Jaji Warioba lilitawala mjadala kwa dakika kadhaa kutokana
na baadhi ya wajumbe kupinga mawazo ya kukaa kimya, lakini Kinana
aliwaambia kwamba kama wanataka kujibizana na Ukawa au watu
wanaozungumza kwenye midahalo, iwe maeneo mengine, akisema Bunge si
mahali pake.
“Alisema kama tunataka kuwajibu Ukawa na wengine,
basi tuandae midahalo au mikutano ya hadhara na kwamba bungeni ni mahali
pa kujadili mambo muhimu tena siyo yanayohusu watawala, bali
yanayowahusu wananchi,” kilisema chanzo chetu kikimkariri Kinana.
Kauli ya Kinana
Kinana akizungumza na gazeti hili juzi usiku, alithibitisha
kuzungumza na wabunge wa CCM lakini hakutaka kuingia kwa undani kuhusu
kile kilichojiri katika mkutano wake.
Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye alikiri kwamba Kinana alitoa maelekezo kuwa Bunge Maalumu
litumike kwa ajili ya mijadala ya mambo ya wananchi na siyo kulumbana na
watu walioko nje ya Bunge hilo.
“Kweli katibu mkuu alikuwa na kikao cha wabunge na
hilo ni moja kati ya mambo mengi ambayo yalizungumzwa,” alisema Nape
lakini alikataa kuingia kwa undani kuhusu suala hilo.
Katika siku ya kwanza ya awamu ya pili ya Mkutano
wa Bunge Maalumu ambao ulitumika kwa ajili ya marekebisho ya Kanuni za
Bunge hilo, baadhi ya wajumbe waliwashambulia Ukawa kwa kutorejea
bungeni tangu waliposusia vikao hivyo Aprili 16, mwaka huu.
Kadhalika wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
akiwamo Jaji Warioba walishambuliwa hasa kutokana na mdahalo
walioufanya Jumatatu wiki hii, walipotoa ufafanuzi wa masuala kadhaa
ambayo yamekuwa kiini cha mgogoro kuhusu Katiba hiyo.
Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe walinukuliwa
wakisema kuwa chanzo cha mijadala isiyo na tija ni wabunge wengi
kutosoma taarifa mbalimbali ambazo zingewawezesha kufanya uchambuzi wa
kina kuhusu Katiba, hivyo wamekuwa wakijenga hoja zao kwenye msingi
dhaifu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Celina Kombani alinukuliwa akionyesha moja ya nyaraka
ambazo zingewasaidia wajumbe hao kujenga hoja zenye mashiko, lakini
akasema hicho hakitokei kwa sababu wajumbe hawana utamaduni wa
kujisomea.
Utoro wa mawaziri
Suala jingine ambalo lilizua mjadala mkubwa ndani
ya kikao hicho ni kuhusu mawaziri kutohudhuria vikao vya kamati, hali
ambayo inasababisha kukosekana kwa akidi ya kutosha kupitisha baadhi ya
ibara muhimu za Rasimu ya Katiba.
“Miongoni mwetu wapo waliokuwa wakali sana
wakisema mawaziri wanapuuza mchakato huo kwani mahudhurio yao
hayaridhishi, maana hata katika Bunge lililopita baadhi ya mambo
yalikwama kwa kukosekana kwa kura mbili au tatu na hapo unakuta mawaziri
ambao ni wajumbe hawapo,” kilifafanua chanzo hicho.
Mwenyekiti wa Kamati namba 11 ya Bunge Maalumu,
Anne Kilango Malecela alinukuliwa akitoa mfano wa kamati yake ambayo ina
wajumbe watano ambao ni mawaziri na kwamba ikitokea wote hawapo kwa
wakati mmoja, wanaweza kukwama kufikia baadhi ya uamuzi.
Mawaziri na manaibu wao katika kamati hiyo ni
Christopher Chiza, Dk Kebwe Steven Kebwe, Mwigulu Nchemba, Godfrey Zambi
na Adam Malima.
Waziri Mkuu Pinda alinukuliwa akisema watajitahidi kupunguza
ruhusa za mawaziri kwenda nje ya Dodoma, lakini akasema suala hilo lina
changamoto kubwa kwani lazima shughuli za Serikali ziendelee, haziwezi
kulala wakati wote wa vikao vya Bunge Maalumu.
Pinda alisema baadhi ya shughuli za Serikali
zilishapangwa tangu mwanzo, hivyo siyo rahisi kuahirishwa wala kufutwa
kwani zinaweza kusababisha athari kubwa. Alitoa mfano wa Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye siyo rahisi
kumnyima ruhusa kutokana na aina ya majukumu aliyonayo.
Kauli yake iliungwa mkono na Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ambaye alinukuliwa akitoa mfano
kwamba yeye na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka watalazimika kwenda Bagamoyo kutatua mgogoro wa ardhi
katika eneo kinakojengwa Chuo Kikuu cha Muhimbili na kwamba wasipofanya
hivyo ujenzi huo utakwama.
Leo wajumbe wa Bunge Maalum wanaendelea kujadili Rasimu ya Katiba ikiwa ni siku ya pili.
No comments
Post a Comment