Latest News

GNM Cargo

GNM Cargo
GNM CARGO & LOGISTICS

menu

Wednesday, August 6, 2014

Bunge Maalumu sasa siku 90

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwaeleza jambo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba katika Viwanja vya Bunge hilo mjini Dodoma jana. 
Na Neville Meena,Mwananchi
Dodoma. Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba watakuwapo mjini Dodoma kwa siku 90 kwa lengo la kukamilisha mjadala na kupitisha Rasimu ya Katiba itakayokwenda kupigiwa kura na wananchi.
Siku hizo ni ongezeko la siku 30 zaidi katika siku 60 ambazo ziliongezwa na Rais Jakaya Kikwete Julai 28, mwaka huu na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 254 ya Agosti 1, mwaka huu.
Kwa kuongeza siku hizo, Bunge Maalumu linaweza kutumia zaidi Sh15.5 bilioni kwa ajili ya kugharimia posho ya kujikimu na ile ya vikao kwa wajumbe wake wote 628 bila kuhusisha gharama nyingine kama za watumishi na huduma mbalimbali.
Katika gazeti hilo, Bunge Maalumu lilipaswa kuanza jana, Agosti 5 na kumalizika Oktoba 4 lakini ratiba ya Bunge hilo iliyotolewa jana inaonyesha kuwa litamalizika Oktoba 31.
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta alisema siku zinazohesabiwa kwa ajili ya kazi za Bunge hilo ni za kazi yaani Jumatatu hadi Ijumaa na kwamba Jumamosi na Jumapili siyo sehemu ya siku 60 zilizoongezwa na Rais.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alisema hakuwa na taarifa iwapo Rais Jakaya Kikwete alikuwa amefanya mazungumzo na uongozi wa Bunge Maalumu kuhusu hoja ya siku za mwishoni mwa wiki na kwamba tarehe ya mwisho anayoifahamu kwa Bunge hilo ni Oktoba 4.
“Kwa kweli sifahamu kuhusu suala hilo, lakini kwa kuwa Rais ndiye mwenye mamlaka kisheria, siwezi kufahamu kama uongozi wa Bunge umewasiliana naye na kama wamefanya hivyo basi GN itabadilishwa ili kukidhi matakwa ya mabadiliko hayo,” alisema.
Akizungumza katika Viwanja vya Bunge jana, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema tayari Rais Kikwete alishatoa ruhusa ya kuzingatiwa kwa siku za mapumziko na zile za mwishoni mwa wiki katika ratiba ya sasa.
“Tulipokuwa tunashauriana kuhusu jambo hili, tulipitiwa hatukuzingatia kwamba GN inaweka ukomo wa tarehe ya Bunge Maalumu, lakini baadaye wakati tunaanza utekelezaji tumelibaini hilo kwa hiyo tukasema litarekebishwa,” alisema Pinda na kuongeza:
“Jambo ambalo tumekubaliana ni kwamba kwa sababu suala la kufanya mabadiliko kwenye GN liko kwenye uwezo wa waziri mwenye dhamana, tutamwambia tu aweze kufanya marekebisho kadri ambavyo uongozi wa Bunge Maalumu ulikubaliana na Mheshimiwa Rais.”
Sheria za kazi
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema taratibu zilikuwa zikiendelea kuwasiliana na watendaji serikalini ili kurasimisha uamuzi huo ambao umezingatia sheria za kazi na ile ya utumishi.
Kifungu cha 23 cha Sheria ya Kazi na Uhusiano Kazini Namba 8 ya 2006 kinaeleza kuwa mfanyakazi anapaswa kuwapo kazini kwa siku tano au saa 45 kwa wiki, sheria ambayo inaongoza utendaji katika sekta ya umma na ile ya binafsi.
“Ni kweli kwamba tunajenga hoja hiyo maana kwa mujibu wa sheria za kazi na zile za utumishi, siku za kazi ni tano na ndiyo maana hata mabadiliko ya kanuni yanayopendekezwa yanalenga kubadili vipengele ambavyo awali vilikuwa vikielekeza Bunge kufanya kazi Jumamosi kwa nusu siku,” alisema Hamad.
Katika azimio lake la Aprili 4, mwaka huu, Bunge Maalumu liliipitisha Jumamosi kuwa moja ya siku zake za kazi kwa kuongeza kipengele cha nne katika Kanuni ya 14.
Sehemu ya kanuni hiyo inasomekea: “Bunge Maalumu kwa siku za Jumamosi litakutana kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana…”.
Hata hivyo, jana Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho aliitaja kanuni hiyo ya 14 (4) kuwa miongoni mwa zilizorekebishwa ili kuiondoa Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi.
Muda zaidi
Habari ambazo gazeti hili imezipata zinasema baada ya Serikali kukubali kuzingatia matakwa ya sheria za kazi katika siku za kuendesha Bunge Maalumu, kumekuwapo na hoja ya kutaka Bunge hilo lifidiwe Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu zilizojitokeza.
Hoja nyingine ni ile inayotaka Bunge hilo lifidiwe siku 21 ambazo zilitumika kwa ajili ya kuandaa kanuni kwa maelezo kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2012 inaelekeza kwamba siku 70 zilikuwa kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Katiba na siyo kufanya kazi nyingine.
Ikiwa Serikali itaridhia hoja hiyo, basi Bunge Maalumu linaweza kuongezewa siku zaidi ya 35 kwa mchanganuo wa siku 21 zilizotumika kutunga kanuni, siku 14 zikiwa siku mbili (Jumamosi na Jumapili) kwa wiki saba na siku za mapumziko zinazotokana na sikukuu za kitaifa.
Hamad alisema kumekuwapo kwa hoja za aina hiyo lakini akasema ni mambo ambayo hajaingizwa katika mfumo rasmi wa kutekelezwa kupitia ofisi yake.
“Kama unavyofahamu wataalamu wetu wa sheria wamekuwa wakitushauri mambo mengi kuhusu suala la muda za uendeshaji wa shughuli za Bunge hili, kwa hiyo hayo uliyoyasema pia ni miongoni mwa hoja zinazozungumzwa lakini bado hatujafika huko,” alisema.


« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment