Writen by
sadataley
1:50 PM
-
0
Comments
Na Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Hatimaye Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwania urais amethibitisha rasmi kuwa atagombea kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Kiongozi huyo aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu
wakati alipokuwa akihojiwa na Radio Deutsche Welle (DW) ya Ujerumani
jana mchana na hivyo kuwa kiongozi wa pili kutangaza nia kupitia vyombo
vya habari vya kimataifa.
Julai 3, mwaka huu, Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, January Makamba alitangaza nia ya kuwania urais baada ya
kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) alipokuwa amekwenda
huko kuhudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano.
Akifafanua kwa nini anataka kuwa rais, January
alisema kuwa huu ni wakati wa fikra mpya kushika dola na kwamba anaamini
muda wa wazee kukaa kando umefika.
Sumaye ambaye aliwahi kugusia suala hilo kwa
kusema kuwa angeweza kugombea kwenye kinyang’anyiro kijacho kama
wananchi wangetaka afanye hivyo sasa ametegua kitendawili kwa kusema
kuwa yuko tayari kuwania nafasi hiyo.
“Maana siyo kila mtu anayejaza kutaka kwenda
kugombea. Ni watu wamemtaka na wapo wengi tu ambao wanajaza kwa sababu
wametaka wenyewe eeh! Kwa hiyo kama watu wakinitaka nitagombea kwa nini
nisigombee, nitagombea na ninafikiria nitagombea,” alisema.
Hata hivyo, alionyesha kutishwa na kiwango cha rushwa katika mchakato wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kusema kuwa:
“Ukweli ni kwamba matumizi ya fedha ndiyo yamekuwa
makubwa sana na kwa kiwango fulani Watanzania wanadhani, siwezi kuwamo.
Watanzania ni wale ambao wana nafasi ya kuchagua na wanadhani kama
hawajapata fedha basi huyo ambaye hajatoa fedha anaonekana kama
hachaguliki.
“Ukweli ni kwamba ni jambo la hatari na lazima
tulipige vita katika nchi yetu. Matumaini yangu ni kwamba viongozi wetu
waliopo watajitahidi kupiga vita,” alisema Sumaye.
Pia kiongozi huyo alikosa baadhi ya watu wanaosema
wakati wa kuwa na rais kijana umefika kwa kusema kuwa umri hauwezi kuwa
kigezo pekee cha kumpata rais.
“Kama kuna kijana hata kama ana miaka 41 ambaye
anadhani anafaa na umma unadhani anafaa si kwa sababu ni kijana hakuna
tatizo, mradi asiwe anakwenda pale kwa kusema mimi ni kijana ninayefaa.
Unaweza kusema kila kijana anafaa kuongoza hii nchi? Haiwezekani”
alihoji.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa Januari 1
mwaka huu alitangaza ‘kiaina’ kuwania nafasi ya urais kwa kusema kwamba
anaanza safari ya matumaini.
Februari mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM iliwapa onyo kali makada
wake sita akiwamo Fredrick Sumaye ikiwatuhumu kupiga kampeni za urais
kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kabla ya muda.
Makada wengine waliopewa adhabu hiyo ni Naibu
Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu),
Stephen Wassira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Pia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula
aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wanaCCM kutangaza mapema nia ya
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema ni
wasaliti.
No comments
Post a Comment