Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, July 18, 2014

Shule 10 bora 2013 zaporomoka


Shule ya Sekondari Kisirimi iliyopo Wilayani Arumeru mkaoni Arusha  
Na Mussa Juma, MwananchiArumeru. Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kisirimi wilayani Arumeru, Arusha, Emmanuel Kisongo amesema kufanya vizuri kwa shule yake ni kuthibitisha shule za kata zinaweza kuwa bora nchini.
Kismiri (pichani) imeshika nafasi ya tatu kati ya shule 10 bora nchini mwaka huu, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwalimu Kisongo alisema mwaka huu wanafunzi wa shule yake wamefanya mtihani wa kidato cha sita kwa mara ya saba na shule imefanikiwa kushika nafasi ya tatu kitaifa kwa mara ya kwanza.
“Nimefurahi tumeingia kwenye shule 10 bora nchini mara tano na safari hii tumeshika nafasi ya tatu. Ni wazi shule za kata zinaweza, tofauti na fikra za wengi kuwa shule zipo chini kielimu,” alisema.
Kisongo alisema mwaka jana walishika nafasi ya tano, kitaifa na mwaka juzi, walishika nafasi ya tatu kama mwaka huu.
“Siri ya mafanikio yetu ni ufundishaji mzuri na ushirikiano mzuri wa walimu, wanafunzi na wazazi kwa lengo kubwa la kuthibitisha kuwa walioanzisha shule ya kata hawakufanya makosa,” alisema.
Alisema shule yake, ambayo ina jumla ya walimu 32 kati yao 12 wanafundisha kidato cha tano na sita, inafuata michepuo ya sayansi na sanaa (art) na mwaka huu wanafunzi 52 walifanya mtihani.
“Tunajivunia mafanikio haya na malengo yetu kuifanya shule hii kuwa bora nchini kwani ipo katika mazingira tulivu na wanafunzi wa dini zote tunawajenga kuwa na hofu ya Mungu,” alisema.
Alisema kwa sasa wanafunzi wa shule hiyo, wanajitambua na wanaheshimu masomo yao. Hawana muda wa migogoro na shule, jambo ambalo linawapa muda mzuri kusoma.
Shule 10 bora 2013 zaporomoka
Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Shule za sekondari zilizokuwa kwenye orodha ya Kumi Bora ya matokeo ya kidato cha sita mwaka jana zimeporomoka, huku shule isiyo maarufu ya Igowole, mkoa wa Iringa ikichomoza kutoka nafasi ya nane hadi ya kwanza mwaka huu.
Mazingira ya Shule ya Sekondari ya Igowole iliyopo Wilaya ya Mufindi ni ya kawaida sana, huku kwa muda mwingi wa msimu wanafunzi wakipigwa na baridi kali katika eneo lilipo shule hiyo iliyozungukwa na miti mikubwa.
Katika matokeo ya kidato cha sita mwaka jana, Necta ilipanga shule 10 bora kulingana na idadi ya watahiniwa juu ya 30 na chini ya 30, lakini mwaka huu imeziweka kundi moja, kwa mujibu wa kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles E. Msonde.
Mwaka jana, kati ya shule 10 zilizokuwa na watahiniwa zaidi ya 30, ni shule nne pekee zimeendelea kuwamo katika kundi la shule 10 bora kitaifa mwaka huu licha ya mabadiliko hayo. Shule hizo ni Marian Girls (Pwani) imekuwa ya sita mwaka huu wakati ilishika nafasi ya kwanza 2013. Shule ya Feza Boys (Dar es Salaam) imeshika nafasi ya pili mwaka huu wakati mwaka jana ilikuwa ya tatu.
Shule ya Sekondari ya Kibaha (Pwani) imeshika nafasi ya tano wakati mwaka jana ilishika nafasi ya tisa. Kisimiri (Arusha) imekuwa ya tatu ilhali mwaka jana ilikuwa ya tano kitaifa.
Shule zilizokuwa 10 bora mwaka jana lakini mwaka huu hazimo katika nafasi hiyo ni; Mzumbe (Morogoro) iliyokuwa ya pili, Ilboru Arusha (4) na Mtakatifu Mary Mazinde Juu ya Tanga (6).
Nyingine ni Tabora Girls (7) na Kifungilo Girls ya Tanga iliyoshika nafasi ya 10.
Katika kinyang’anyiro hicho, shule zilizochukua nafasi ya shule zilizong’olewa katika kumi bora na nyingine kupanda kutoka nafasi moja hadi nyingine ni Igowole (Iringa) iliyoshika nafasi ya kwanza mwaka huu na mwaka jana ilikuwa ya nane. Iwawa (Njombe) imeshika nafasi ya nne. Nyingine ni Nangwa (Manyara) nafasi ya saba, Uwata (Mbeya-8), Kibondo (Kigoma-9) na Kawawa (Iringa) imefunga ukurasa kwa kuwa ya kumi.
Shule zilizokuwa za mwisho mwaka jana katika kundi la wanafunzi chini ya 30 na zaidi ya 30 mwaka huu licha ya mabadiliko hayo ni shule tatu ziliyobaki na nyingine maarufu zikiingia kwa mara ya kwanza.
Baadhi ya shule zilizoshika mkia ni Fidel Castro (Pemba), Tambaza (Dar es Salaam), Muheza (Tanga), Mtwara Technical (Mtwara) na Iyunga Technical ya Mbeya. Al-Falaah Muslim (Unguja) na Osward Mang’ombe (Mara) zikiingia kwa mwaka wa pili mfululizo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment