Writen by
sadataley
4:53 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametaja majina 11 ya wanachama wa CCM wanaofaa kuwania urais kurithi kiti cha baba yake, Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake mwakani.
Ridhiwani (35), ambaye alishinda kiti cha ubunge
wa Jimbo la Chalinze Aprili mwaka huu, alitaja majina hayo katika
mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dodoma hivi
karibuni.
Miongoni mwa aliowataja kuwa wana sifa ni makada
watano walio chini ya uangalizi wa CCM wa mwaka mmoja baada ya kubainika
kuanza kampeni za urais mapema, mawaziri wawili waliopoteza nyadhifa
zao katika kashfa ya Operesheni Tokomeza, mwanamke mmoja na Rais wa
Zanzibar.
“Kutaja majina tu, naweza kuorodhesha wengi tu.
Naweza kuorodhesha hata watu 500, kwa sababu tunaona wengi sana,”
alisema mtoto huyo wa Rais Kikwete ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa muda
mrefu akitokea umoja wa vijana wa chama hicho, UVCCM. “Kwa mfano, kwa
upande wa Bara tunao Emmanuel Nchimbi, William Ngeleja, January Makamba,
Bernard Membe, Steven Wassira, Edward Lowassa na Asha-Rose Migiro,”
alisema.
Aliongeza: “Hawa ni kwa uchache zaidi… ni baadhi
ya watu ambao wanatajwa kwa upande wa Bara, lakini jambo la msingi ni
nani mwenye sifa za kuwa rais.”
Alisema pamoja na kwamba wanasiasa hao wote wanazo
sifa za kuiwania nafasi hiyo ya juu, vikao vya chama ndivyo vitakuwa na
nafasi ya kuwachuja ili kupata wanaotosha. “Kama wanatosha au la, vikao
vya chama vitakaa kuamua licha ya kuwa hao wote niliowataja, kwa sifa
za kugombea urais wote wanajitosheleza. Wana sifa, wana uwezo wa
kugombea na wana uwezo wa kushinda, hao ni kwa upande wa Bara,” alisema.
Alipoulizwa hali ikoje kwa upande wa Zanzibar,
Ridhiwani alisema, “Sisi chama chetu kina utajiri wa watu kwa upande wa
Zanzibar kuna Shamsi Vuai Nahodha, Hussein Ali Mwinyi, Dk Seif Ally Iddi
(Makamu wa pili wa Rais Zanzibar) na Dk Mohammed Ali Shein, Rais wa
Zanzibar. Hawa ni watu ambao wana uwezo na hata wakipewa jukumu la
kuongoza nchi hii wanaweza. Tunao wengi sana.”
Membe, Wassira, Lowassa, Ngeleja na Makamba
walipewa adhabu na Kamati ya Maadili ya CCM ya kutogombea nafasi yoyote
ndani ya chama wala kufanya kampeni baada ya kudaiwa kukiuka taratibu za
chama hicho, wakati Nchimbi na Nahodha walilazimika kujiuzulu nyadhifa
zao za uwaziri kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza ambayo ililenga
kushughulikia majangili, lakini ikahusishwa na vitendo vya ukiukaji
haki za binadamu.
Ridhiwani hakumtaja Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye ambaye pia anatumikia adhabu hiyo ya Kamati ya Maadili ya CCM.
Baadhi kukwama
Hata hivyo, Ridhiwani alidokeza kuwa wapo baadhi
ya wanasiasa watakaokwama kufikia lengo hilo kutokana na kukabiliwa na
kesi ndani ya chama, ambazo hakuzitaja wala kutaja wahusika.
“Kuna watakaopungua kutokana na kesi
zinazowakabili katika chama ambazo zinawafanya wapungukiwe sifa. Kwa
maana hiyo kuna watu kama wanne hivi (wa Bara) unawatoa na ukiwatoa
unabakiwa na watatu, sasa unaweza kujiuliza hao watakaobaki watatu, je,
wanatosha?”
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/2382900/-/tomvl0z/-/index.html
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/-/1597296/2382900/-/tomvl0z/-/index.html
No comments
Post a Comment