Writen by
sadataley
6:59 PM
-
0
Comments
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ameitaka Serikali kufanya uchunguzi hata kwa kampuni kubwa za uwindaji zenye leseni halali kwani yapo yanayokiuka sheria.
Msigwa pia amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu kuwachukulia hatua za kisheria watendaji wa Kampuni ya
Green Miles Safari Ltd, GMS kwa madai kuwa wamekiuka masharti ya
uwindaji.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mchungaji
Msigwa alisema ana wasiwasi hata kampuni kubwa zenye vibali halali
yanakiuka sheria za uwindaji.
Msigwa ndiye aliyeibua video ya Kampuni ya Uwindaji ya GMS na kulazimisha Waziri Nyalandu kuifutia kibali cha uwindaji,
Alisema haiwezekani kuwa kampuni za uwindaji za
Tanzania au za kutoka nje ziko safi kwa asilimia 100 na haziendi kinyume
cha leseni zao, na baada ya uchunguzi, zitakazobainika zifutiwe leseni
na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
“Mimi niko tayari kusimamia na kuhakikisha
wahusika wanafikishwa mahakamani, hii ni rasilimali ya Watanzania na
tunatoa vibali kwa kazi maalumu,” alisema.
Akizungumza suala la Kampuni ya GMS, Msigwa
alimtaka Waziri Nyalandu kutoishia kutangaza kuwafutia kibali cha
uwindaji kampuni hiyo.
“Ninashangaa hadi leo hawajachukuliwa hatua,
niliorodhesha makosa yao 11, lakini Waziri kaishia kuwafutia leseni,
hiyo haitoshi, lazima wachukuliwe hatua,” alisema Msigwa.
Hata hivyo, uongozi wa GMS, umepinga hatua hiyo ya Nyalandu kuwafutia leseni, hivyo wameahidi kulifikisha suala hilo mahakamani.
Msigwa ambaye ni waziri kivuli wa maliasili na
utalii, alisema GMS hawawezi kukwepa mkono wa sheria kwa kile
walichokifanya na ataendelea kupambana kuhakikisha wanalinda maliasili
za nchi kwa kushirikiana na Mtanzania mwenye uchungu bila kujali itikadi
ya vyama.
Hata hivyo, pamoja na kusisitiza mkono wa sheria
kwa GMS na kutaka kuungwa mkono, Msigwa alionyesha wasiwasi wa kuungwa
mkono katika kampeni yake kwa kusema kuwa ni mtandao mkubwa ambao
hauhofii hata kuondoa roho ya mtu anayewafuatilia.
Msigwa kwa upande mwingine, alikanusha tuhuma
kwamba yeye pamoja na Waziri, Nyalandu na Mwenyekiti wa Kamati ya
Maliasili na Mazingira, James Lembeli wanatumika na wametengeneza ‘utatu
mtakatifu’ kwa maslahi yao binafsi.
“Unajua watu wanasema hivyo, mimi siko kwa ajili ya kumbeba
Nyalandu wala Lembeli na wanalifahamu hilo, mimi naangalia ulinzi wa
maliasili.
“Hata nikipewa safari za nje, si ‘favour’ ni haki
yangu kwa nafasi yangu na nikija bungeni kama wataharibu, nawalipua
...niliwahi kuwalipua viongozi mbalimbali wa juu kwa nyara za maliasili,
sasa nitakuwaje kwenye utatu, wenye utatu wanalipuana?” Alihoji.
Msigwa aliwataka Watanzania kuwa na uchungu na maliasili za taifa kwa maslahi ya taifa badala ya kuachia wachache wakihujumu.
No comments
Post a Comment