Writen by
sadataley
3:45 PM
-
0
Comments
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.PHOTO|FILE
Na Mwandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameelezea kushangazwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba kitendo cha Ukawa kususia Bunge la Katiba kinauweka njia panda uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kauli ya Mbowe inatokana na Pinda kusema juzi kuwa
hatma ya uchaguzi huo itategemea uamuzi wa wajumbe wa Ukawa (Umoja wa
Katiba ya Wananchi) kurejea katika Bunge Maalum kuipitisha Katiba Mpya
kwa wakati.
Waziri Pinda alisema hayo wakati akizungumza na
mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji nchini uliofanyika
jijini Tanga, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Serikali za
Mitaa yaliyofanyika kitaifa mjini Tanga.
Akizungumzia kauli hiyo na kituo cha Radio One
jana asubuhi, Mbowe alisema: “Nashindwa kujua Waziri Mkuu akizungumzia
Ukawa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa alikuwa akizungumzia kwa namna
ipi, nashindwa kumwelewa.
“Mabadiliko ya sheria ambayo ni muhimu kufanyia
marekebisho kabla ya uchaguzi, hayafanywi na Bunge la Katiba, yanafanywa
na Bunge la kawaida, kwa sasa hakuna Bunge na Bunge la kawaida
linatarajia kukaa Novemba 4 mwaka huu, kipindi ambacho uchaguzi wa
Serikali za Mitaa utakuwa umeshapita.
“Kwa maana hiyo, kuanzia sasa hadi Novemba, Bunge
halitakutana kama bunge la kawaida, kwa hiyo hakuna fursa ya mabadiliko
ya sheria yoyote ile hadi Novemba, labda kuwe na Bunge la dharura, sasa
Waziri Mkuu anaposema kutorejea kwa wajumbe wa Ukawa katika Bunge la
Katiba kutakwamisha uchaguzi, si kweli.
“Serikali yenyewe imechelewa kuleta muswada wa
marekebisho ya sheria. Imechelewa kurekebisha kanuni na sasa inataka
kuleta kisingizio cha nini kinachelewesha na kuwa wajumbe wa Ukawa ndiyo
wanachelewesha. Lakini hivi (uchaguzi na Ukawa) ni vitu viwili
tofauti,” alisema.
Kurejea bungeni
Akizungumzia mustakabali wa Ukawa kwenye Bunge la
Katiba baada ya kuwepo wito wa watu mbalimbali, wakiwamo za viongozi wa
dini, Mbowe alisema kuwa watu wanatafsiri vibaya kuwa wajumbe wa umoja
huo wanagoma kurejea kwenye Bunge la Katiba, kinachotakiwa ni kuangalia
sababu gani zinawafanya kushikilia msimamo huo.
Alifafanua kuwa wakati wanagomea Bunge la Katiba
walikuwa na sababu za msingi na bado zipo, hazijatatuliwa wala
hazijafanyiwa kazi. Kwa maana hiyo, kwa kuwa hazijafanyiwa kazi na
hazijatatuliwa, wataendelea kubaki nje ya Bunge.
Hata hivyo, Mbowe alisema kuwa msimamo wao kugomea Bunge la Katiba siyo wa kudumu kwani unasababishwa na mazingira.
“Watu wakae chini, watathmini, waangalie matatizo
yako wapi na tutatue matatizo mapema na yakikamilika, watu watarejea
bungeni. Lakini hatuwezi kurudi pale kwenda kutukanana, kunyanyasana na
kuvunjiana heshima. Haileti maana kabisa, kitu ambacho si malengo ya
Bunge la Katiba.
“Msimamo wetu (wa kususia Bunge la Katiba) si wa kudumu,
unasababishwa na mazingira. Watu wakae chini, watatue matatizo na
yakimalizika watu watarejea bungeni...lakini kama hatukutatua, itakuwa
ni kama watoto wadogo wasiofanya tathmini wala kujua athari ya kitu,”
alisema.
Kauli za msajili
Kuhusu nafasi zao kwenye vyama kuwa hawana sifa na
wanabanwa na katiba kama ilivyosema ofisi ya msajili wa vyama vya
siasa, Mbowe aliponda kauli ya hiyo akisema kuwa anaweza kuzungumza
chochote na kwa kuwa msajili si mahakama, anaweza kutoa tafsiri yake kwa
mtazamo wake, lakini uhalisia utaonekana katika vyombo husika.
Akizungumzia kuhusu ukomo wa uongozi na madai
kwamba walibadilisha kinyemela kipengele hicho katika Katiba, Mbowe
alisema si wakati muafaka kujiingiza kwenye malumbano yasiyo na maana.
wa juu pekee kama ilivyoelezwa.
“Hili nalitazama katika sehemu mbili: Kwanza; kama
ukomo ni kwa viongozi wote wa nchi nzima katika nafasi mbalimbali,
mikoa hadi kata, na wapo viongozi wametumikia chama kwa zaidi ya miaka
10 hadi 15 na sheria zinatungwa si kwa ajili ya mwenyekiti na katibu
wake.
“Pili; uamuzi wa ukomo na nani aongoze taasisi kwa
muda gani wanaamua wanataasisi kupitia vikao na kama inasemwa mkutano
mkuu uliridhia vinginevyo, sijui msajili alikuwa na maana gani. Lakini
si wakati mwafaka kujiingiza katika malumbano yasiyokuwa na maana,”
alisema Mbowe.
Kuhusu malalamiko kwa viongozi kutotimiza majukumu
ya chama, alisema viongozi wanaolalamika kutotekelezwa mambo mbalimbali
ni wasaliti kwa kuwa mambo ya chama yanazungumzwa ndani ya vikao
halali.
“Kwa sasa ni wakati wa kwenda kwenye uchaguzi na
mahasimu wanafanya mbinu mbalimbali kukidhoofisha chama na ninataka
kusema kuwa chama kiko imara na hao wanaotaka kuleta chokochoko za
kitoto na mambo ya kijinga, hawatakuwa na nafasi,” alisema Mbowe.
“Tumetoka hatua moja kwenda nyingine. Kwa muda
mrefu, tumekiimarisha chama kwa gharama kubwa na tutakilinda chama kwa
gharama zote. Chama hiki kinaheshimu katiba, kinapigania haki na ustawi
wa Tanzania.
“Hatutatetereka kwa watu wachache wanaotumika kwa
mbinu mbalimbali eti kukipaka matope chama ili chama kiingie kwenye
uchaguzi tukiwa tumejeruhiwa. Hatutaogopa kikundi chochote
kinachoandaliwa kimkakati kuichafua Chadema na tutapambana nacho.”
No comments
Post a Comment