Writen by 
                            sadataley
1:49 PM
                            - 
                            
0
                            Comments
                          
  
  
            
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela.PICHA|MAKTABA 
            
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela 
amesema siku 60 zilizotengwa kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kabla 
ya kupelekwa kwa wananchi hazitoshi kwa kazi hiyo.
Akizungumza na katika mahojiano maalumu mjini Dodoma hivi karibuni, Malecela alisema: “Watahitaji siku zaidi…
Nadhani kosa moja ambalo tumelifanya ni la kujaribu kuweka muda maalumu wa kupitisha Rasimu ya Katiba.
Hata hivyo, huu muda tuliouweka hatukuuweka 
kutokana na uzoefu wa ama nchi fulani, maana tuangalie nchi zilizoandika
 katiba zao, tuseme nchi fulani walichukua miezi fulani kwa hiyo sisi 
itachukua siku fulani. Hebu angalia, kanuni tu zilichukua siku 40 na 
katika hizi siku 40 walizungumza sura ya pili na sita tu.”
Bunge Maalumu la Katiba litaanza Agosti 5, mwaka 
huu mjini Dodoma kwa siku 60 kukamilisha awamu ya pili ya mchakato huo 
baada ya kumalizika awamu ya kwanza mwanzoni mwa mwaka huu.
Akizungumzia mchakato mzima wa Katiba Mpya 
Malecela alisema: “Bado ninaamini inawezekana tukapata Katiba Mpya kama 
tutakwenda na moyo wa kusema nipe nikupe na haya mambo ya watu kutoka 
kwenye mazungumzo unajua mara nyingine tunaangalia hapa tu.
“Nimekwenda katika sehemu nyingine za dunia. Mfano
 wa Jamhuri ya Ireland na Serikali ya Waingereza ilichukua miaka mingapi
 wakae chini? Iliwachukua miaka mingi lakini walikaa chini wakazungumza 
wakafikia mahali walipo sasa hivi hakuna mgogoro.
“Wewe ulifikiria Marekani katika siku hizi itakuwa
 na ubalozi Iran? Lakini sasa hivi wanafikiria kufungua ubalozi Iran. 
Kwa hiyo mimi nasema tufuate mifano ya nchi nyingine, tusikate tamaa 
haraka.
Kuhusu hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi, 
kususia vikao vya Bunge hilo alisema: “Hawa wametoka naamini bado watu 
wanaweza wakazungumza nao na nyie vyombo vya habari mkawasaidia 
kuwatolea mifano mingi tu duniani na kumekuwa na migogoro mahali 
pengine. “Chukua mfano wa Sudan Kusini miezi miwili, mitatu iliyopita 
siyo walikuwa wakipigana, huyu Rais anasema yule ni mhaini na yule 
akatoa vikwazo, mimi siji lazima hiki na hiki kifanyike lakini sasa hivi
 wako wapi! Si wako wanazungumza na mimi nadhani wanaelekea kuunda 
serikali ya maridhiano.
“Kwa hiyo sikati tamaa, bado nina hakika kwamba 
wenzetu waliotoka bado kuna nafasi ya kuzungumza nao kwa kuwapa maelezo 
na wao watakuwa na fikra zao.”
Alisema kila upande utatoa maoni yake na kufikia mwafaka na kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana.
Kuhusu Tanzania kama inahitaji Katiba Mpya kwa 
sasa, Malecela alisema: “Mimi hapo nadhani nitawakera kidogo kwa sababu 
mawazo yangu yako vingine kabisa.
“Suala la Katiba mimi ambaye nimekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM 
kwa miaka 15 na mara nyingi Katiba zilizokuja ama zimetokana na Tanu au 
na CCM. Sasa Serikali ya CCM ilileta mapendekezo ya kutunga Katiba Mpya.
 Nilionana na Tume na nilikaa nao kwa saa mbili kwa hiyo kama ni mawazo 
yangu niliyatoa huko yote.
“Nafikiri tujaribu kuwa makini. Mradi tumefika 
mahali tumekuwa na Bunge la Katiba sasa sisi sote hasa viongozi 
tuliobaki hebu tuwe kama watu wanaoangalia mpira.  “Unajua mpira unaona 
mchezaji kachoka lakini unasema kimbiakimbia, kumbe mwezako nguvu 
zimemwishia.
“Tukianza kusema maneno hapa katikati, mimi 
nikisema watasema unaona hata Malecela kasema... Tuwaachie wenzetu wa 
Katiba, hawa wajumbe wa Katiba, wakae wazungumze, tutaelewana tu!”
Aliwapongeza wajumbe wa Bunge la Katiba kwa 
kuendesha Bunge bila kanuni lakini baadaye wakasimama na kujitengenezea 
utaratibu wao.
“Mfano mdogo, Yanga na Simba unawafungia katika 
chumba kimoja halafu unawaambia watengeneze sheria za mpira. Watafika 
mahali fulani wakimuona mchezaji wa Yanga mrefu sana, Simba watasema 
kwenye kanuni tuweke wachezaji wasizidi futi fulani. Hata hivyo, 
walifikia mahali fulani wakakubaliana.
Imeandikwa na Frank Sanga, Habel Chidawali na Sharon Sauwa.
 
 
 
 
 
 
 
No comments
Post a Comment