Writen by
sadataley
1:30 PM
-
0
Comments
Dar es Salaam. Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), kimezitaka mamlaka zinazohusika kuchukua hatua kali za haraka dhidi ya taasisi na watu waliojihusisha na utupaji wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wito wa MAT umetolewa siku moja baada ya uongozi
wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), kukiri
kuhusika na mabaki hayo ya viungo vya binadamu yaliyotupwa katika
utaratibu usio wa kawaida.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Rais wa chama hicho, Dk Primus Saidia alisema wahusika wote
wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali kwa sababu kitendo hicho kimekiuka
sheria, taratibu, ubinadamu, maadili ya ufundishaji na taaluma ya
udaktari.
“Kama ni taasisi ya utafiti imepoteza sifa ya
kufanya utafiti na kama ni ya mafunzo basi imepoteza sifa ya kutoa
mafunzo ya tiba. Kama ni hospitali itakuwa imepoteza sifa za kutoa tiba
kwa binadamu,” alisema Rais MAT, Dk Saidia.
Dk Saidia alisema ni wazi kwamba kwa kitendo
hicho, watu na taasisi iliyohusika wamepoteza sifa za kufanya utafiti au
kutoa mafunzo kwa kutumia miili au viungo vya binadamu.
Alisema kitendo hicho kimeifedhehesha tasnia nzima
ya tiba kwa kuwa mwenendo mzima wa kutumia viungo hivyo na kuviteketeza
hufanywa kuwa siri na kwa hapa nchini wamekuwa wakitumia viungo hivyo
kwa utaratibu mzuri uliowekwa kisheria tangu mwaka 1963 kilipoanzishwa
Chuo Kikuu cha Muhimbili kikiwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema MAT inatoa wito kwa vyombo husika; Polisi,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Baraza la Madaktari Tanzania, Tume
ya Usimamizi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Taasisi ya Utafiti wa
Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kuchukua hatua stahiki kwa mtu au taasisi
iliyohusika.
Ni utaratibu wa kawaida
Dk Saidia alisema katika tasnia ya tiba ni
utaratibu wa kawaida unaokubalika duniani kote kutumia miili na viungo
halisi vya miili ya binadamu (Cadaver) kufundisha na kufanya tafiti
mbalimbali za kiafya, lakini huwahusu zaidi wanataaluma.
“Miili na viungo hivi hutumika kwa heshima kubwa
kama walimu wa kwanza katika mafunzo na tafiti za tiba ya mwanadamu.
Tafiti na mafunzo haya ndiyo nguzo kuu katika kukuza ufahamu wa mwili wa
binadamu na hivyo kuboresha utoaji wa huduma za afya,” alisema.
Alisema kwa sasa jambo geni linaloweza kuzungumzwa
ni jinsi mabaki ya viungo hivyo yalivyotupwa katika utaratibu unaozua
mjadala.
Mtambo wa kuharibu mabaki
Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel
Aligaesha alisema jana kwamba juhudi za kutengeneza mashine ya
kuteketeza taka ikiwamo miili hiyo (Incinerator) ambayo imeharibika kwa
miezi sita sasa, zinaendelea lakini hajui ni lini itakuwa tayari.
Gazeti dada la Mwananchi, The Citizen, lilieleza jana kwamba kwa miezi sita sasa mashine hiyo haijafanyiwa matengenezo.
Pia Aligaesha alisema hawezi kueleza utaratibu wa
kuchukua au kurejesha mabaki hayo katika hospitali hiyo ambayo ndiyo
yenye dhamana ya kusimamia upatikanaji wake akidai kufanya hivyo
kunaweza kuingilia upelelezi wa polisi
Wizara yaeleza kushtushwa
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeeleza
kushtushwa na tukio la kutupwa kwa viungo hivyo na kusema inafuatilia
kwa karibu upelelezi wa polisi ili kuchukua hatua.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa wizara hiyo,
Nsachris Mwamaja alisema jana kuwa tukio hilo ni kinyume na kanuni na
sheria za kitabibu, kwani hakuna sehemu yoyote inayoruhusu mwili wa
binadamu kutupwa kama ilivyotokea.
“Hatuwezi kulizungumzia sana, tunaweza kuharibu upelelezi, hebu tuache tusubiri polisi watatupa majibu gani.”
No comments
Post a Comment