Writen by
sadataley
12:41 PM
-
0
Comments
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Vigogo sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambao walipewa onyo kali na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi 12 wamezidi kukitesa chama hicho, na katika kuwadhibiti, kimetoa maagizo kwa Kamati ya Usalama na Maadili kufuatilia nyendo zao.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha kawaida
cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, kuwa
kamati hiyo ifanye mapitio ya mwenendo wa utekelezaji wa adhabu kwa
vigogo hao waliotiwa hatiani kwa kufanya kampeni za urais kabla ya
wakati.
Vigogo waliopewa adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na
Madini, William Ngeleja.
Vigogo hao ambao wamekuwa wakitajwa na wakati
mwingine wenyewe kuzungumzia nia ya kushika nafasi hiyo, walipewa onyo
kali ikiwamo kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 tangu Februari
mwaka huu ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokiuka
maadili ya chama hicho.
Vigogo hao walipatikana na makosa ya kuvunja ibara
ya 6 (2) (1-5) ya maadili ya viongozi wa chama hicho inayozuia kutoa
michango, misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya
kampeni bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya
eneo husika.
Jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye alisema mwezi ujao kamati hiyo itafanya mapitio
ya utekelezaji wa adhabu hiyo ili kubaini iwapo wanaitekeleza au la.
“Kama itabainika kuwa hawatekelezi ipasavyo
masharti ya adhabu zao, itapendekezwa kwa Kamati Kuu ili waongezewe
adhabu nyingine kufuatana na taratibu za chama,” alisema Nnauye.
Kwa mujibu wa Nnauye, Kamati Kuu imepokea taarifa
za kuwapo kwa harakati za baadhi ya wanachama walioonyesha nia ya kuomba
ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya kutafakari kwa kina Kamati Kuu
inawakumbusha kuwa ili wanachama hao wasipoteze sifa za kugombea, ni
muhimu wakazingatia katiba, kanuni na taratibu za chama zinazosimamia
masuala hayo,” alisema Nnauye.
Tangu wapewe adhabu hiyo, makada hao wamekuwa
wakijitokeza hadharani kwa nadra, lakini Makamba na Wassira walikaririwa
na vyombo vya habari wakitangaza nia ya kugombea urais.
Hata hivyo, CCM ilisema kuwa Makamba hakukiuka
taratibu kwa kutangaza nia hiyo, ingawa Rais Jakaya Kikwete alisema
mtoto huyo wa katibu mkuu wa zamani wa chama hicho anataka mambo makubwa
na hakumtaarifu nia hiyo.
Yajadili Ukawa
Kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya, Nnauye
alisema Kamati Kuu imefurahishwa na mazungumzo yanayosimamiwa na Msajili
wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kati ya CCM na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujaribu kuwashawishi
wapinzani kurejea bungeni.
“Kamati imepongeza juhudi zinazofanywa na msajili
na kwamba ni imani yake kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda ili wajumbe
waliosusia Bunge Maalumu la Katiba waweze kurejea kuendelea na mijadala
ya mchakato wa Katiba Mpya,” alisema Nnauye.
Wajumbe wa Bunge wanaounda Ukawa walisusia Bunge
Aprili mwaka huu ni kutoka vyama vya upinzani vya Chadema, NCCR-Mageuzi,
CUF na baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 ili kushinikiza kujadiliwa kwa
rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza muundo wa
serikali tatu badala ya ile ya serikali mbili inayodaiwa kupigiwa debe
na CCM.
Wajumbe hao wanasisitiza hawawezi kurudi bungeni
hadi watakapohakikishiwa kwamba kitakachokwenda kujadiliwa bungeni ni
Rasimu ya Katiba na si vinginevyo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Mutungi ameanzisha
mazungumzo na vyama hivyo ili kuwashawishi wajumbe kubadilisha uamuzi
wao na hatimaye kurejea bungeni Agosti 5, mwaka huu.
No comments
Post a Comment