Writen by
sadataley
6:24 PM
-
0
Comments
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimpongeza Rais wa Baraza la Maaskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania (TEC) ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Iringa,
Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa Kichangani Manispaa ya Iringa
jana wakati wa jubilei yake ya miaka 25 ya uaskofu. Picha na Hakimu
Mwafongo
Na Ibrahim Yamola, Hakimu Mwafongo, MwananchiDar na Iringa. Baraza la Maaskofu la Kanisa
Katoliki Tanzania (TEC), limewataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), kurudi bungeni bila masharti na kuendelea na mjadala
wa Katiba kwa manufaa ya taifa.
Pia, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of
God (TAG), Jimbo la Mashariki Kaskazini, Geoffrey Massawe amewaomba
wajumbe wa Bunge la Katiba kuungana na kuwa kitu kimoja katika mchakato
wa kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hizo za maaskofu hao zimekuja siku moja
baada ya ile ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kusema kuwa hatima ya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea Ukawa, kurejea katika
Bunge Maalumu kuipitisha Katiba Mpya kwa wakati.
Askofu Massawe alitoa ombi hilo wakati wa ibada
maalumu ya sherehe ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa
kanisa hilo nchini iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kinondoni, Dar es
Salaam.
Akitoa salamu za TEC wakati wa kuadhimisha miaka
25 ya uaskofu ya Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa
Kichangani, Iringa, Makamu Rais wa TEC, Mhashamu Severine Niwemugizi
alisema ni vyema wajumbe hao wakarudi kwenye Bunge hilo linalotarajia
kuanza Agosti 5, mwaka huu.
“Ninatumia neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee
bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au kufanya mizengwe mingine na
kutupatia Katiba isiyotufaa, nitawaomba Watanzania wote tuweke uzalendo
mbele na kuikataa Rasimu ya Katiba itakayoletwa pia tuwanyime uongozi
katika Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.
Alisema wameshuhudia mambo ya aibu katika Bunge la
Katiba kabla ya kupisha Bunge la Bajeti na maoni ya wananchi
yaliyokusanywa kupitia tume halali yakibezwa.
Alisema tume ile iliongozwa na wazee wenye uzoefu
mkubwa waliolitumikia taifa kwa muda mrefu na kutumia fedha nyingi za
walipa kodi lakini yalipuuzwa jambo ambalo siyo sahihi.
“Nchi imepoteza dira, wananchi wako njiapanda
hawajui kama watapata Katiba au la na ubinafsi umechukua nafasi kuliko
uzalendo kwa taifa,” alisema.
Niwemugizi aliwataka Watanzania kujitokeza kwa
wingi katika kuboresha Daftari la Wapigakura na kujitokeza kupiga kura
kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na ule mkuu utakaofanyika
mwakani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu, Pinda
aliwataka viongozi wa dini kuliombea taifa kuwa na amani kutokana na
matukio makubwa ya Uchaguzi Mkuu na Katiba yaliyopo.
Pinda alisema amesikia ujumbe uliotolewa na Askofu
Niwemugizi na kuwa kiongozi makini ni yule anayekubali kukosolewa na
kufanya marekebisho.
No comments
Post a Comment