Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, January 10, 2014

Moto wamwakia Profesa Tibaijuka

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.PICHA|MAKTABA 
Na Raymond Kaminyoge na Lauden Mwambona, Mwananchi
Dar es Salaam/Mbeya. Viongozi wa vyama vya siasa na wanaharakati wa masuala ya ardhi, wamesema kuzomewa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ni matokeo ya makosa yanayowafanywa na Serikali kuwapendelea wawekezaji wa nje na kuwapuuza wananchi.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya Profesa Tibaijuka kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo cha kumruhusu mwekezaji kuendelea kumiliki shamba la Kapunga, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya lenye ukubwa wa hekta 7,370.
Wananchi hao walikasirishwa na kitendo cha Profesa Tibaijuka kubadili msimamo wake awali wa kumpokonya ardhi mwekezaji huyo kwani mara ya kwanza alishawaeleza viongozi wa vijiji kuwa serikali itawarudishia eneo lao.
Mwekezaji huyo alitakiwa kumiliki ekari 5,500 lakini serikali ilimmilikisha ekari nyingine 1,870 ambazo ni mashamba ya wanakijiji.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Ardhi, Yefuz Myenzi alisema hayo ni makosa ya serikali kuwapa ardhi wawekezaji wa nje bila kutenga ardhi ya wanavijiji.
“Serikali inabinafsisha hadi vijiji ambako wananchi wangeweza kulima na kuendesha maisha yao, unategemea nini wakimwona kiongozi wa serikali ni lazima watamzomea,” alisema Mnyezi.
Alisema ubinafsishaji wa ardhi unafanywa na ngazi za juu za taifa bila kuushirikisha uongozi wa ngazi za vijiji hali inayosababisha vurugu katika maeneo mengine.
“SiYo katika Shamba la Kapunga tu, kuna maeneo mengi ambako wawekezaji wa kigeni wamepewa ardhi lakini wao wanaikodisha kwa wananchi kitendo ambacho ni kosa,” alisema.
Myenzi alisema katika maeneo yenye matatizo kama hayo, Rais anatakiwa kutumia madaraka yake kwa kubadilisha matumizi ya ardhi ili wananchi waweze kupewa kwa ajili ya kilimo.
Viongozi wengine
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema viongozi wa Serikali wanawapendelea wawekezaji wa nje na kuwapuuza wanavijiji.
“Migogoro hii ya ardhi inavyochukiza watu kama kiongozi utakwenda kusuluhisha na kutoa majibu yasiyowaridhisha wananchi, basi viongozi wataendelea kuzomewa kama Waziri huyo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema wananchi wanakatishwa tamaa na viongozi wa serikali kuwapendelea wawekezaji.
“Ajira pekee inayotegemewa vijijini ni kilimo, serikali inabinafsisha hadi mashamba ya wanavijiji, wamekata tamaa ndiyo maana wanazomea ovyo. Viongozi hawana nia ya dhati kutatua migogoro iliyopo,” alisema.
Akizungumzia suala hilo, Katibu Mkuu wa NCCR -Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema ili kuondokana na migogoro, wawekezaji wanatakiwa kuwa na vibali vya ardhi kutoka katika uongozi wa kijiji.
“Wanakijiji ndiyo wenye ardhi, migogoro ya namna hii isingetokea kama wangeshiriki kutoa vibali kwa wawekezaji,” alisema.
DC amtetea Tibaijuka
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kifu amesema pamoja na kwamba wananchi wa kijiji cha Kapunga wanataka mgogoro huo umalizike haraka, lakini anaamini uamuzi wa Profesa Tibaijuka kufanya mazungumzo na mwekezaji wanayevutana naye utaleta ufumbuzi wa tatizo hilo.
Profesa Tibaijuka alisema majuzi kuwa Kampuni ya Kapunga Rice Project inamiliki kihalali mashamba kwenye eneo hilo na kudai kuwa serikali ndiyo yenye makosa kwenye mgogoro huo.
Mashamba hayo mara ya kwanza yalikuwa yanamilikiwa na Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco) lakini yalibinafsishwa na kuchukulikuwa na mwekezaji huyo.
Kifu alisema pamoja na kwamba wananchi wengine hawakuridhika na uamuzi wa Waziri lakini anaamini kuwa Profesa Tibaijuka ndiyo yuko sahihi kuzungumza na wawekezaji ili waliachie eneo hilo kwani hawana makosa.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment