Writen by
sadataley
5:36 PM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imesema Daftari la Kudumu la Wapigakura, litafanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kwa upigaji wa kura ya maoni kwa ajili ya kupata Katiba Mpya, ili kuwawezesha vijana waliotimiza umri wa miaka 18, ambao hawakujiandikisha, kupata fursa ya kupigakura.
Imesema ili mtu aweze kupiga kura, lazima awe na kitambulisho cha kupigia kura na si kitambulisho cha utaifa, kauli ambayo inapingana na ile iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwamba vitambulisho vya taifa vitatumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza na viongozi 21 wa vyama vya siasa nchini jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Damian Libuva, alishindwa kutaja tarehe wala mwezi ambao maboresho hayo yatafanyika.
Hata hivyo kauli hiyo imekuja ikiwa imebaki miezi mitano kabla ya kuanza kwa upigaji wa kura ya maoni.
Upigaji wa kura ya maoni utafanyika ndani ya siku 74, ikiwa ni baada ya kumalizika kwa Bunge Maalumu la Katiba ambalo litafanyika kwa siku 90, kuanzia Februari mwaka huu.
Jaji Lubuva alisema Nec itaendesha zoezi hilo kwa kutumia mashine maalumu za kielekroniki na kusisitiza kuwa hawezi kueleza tarehe rasmi kwa kuwa tume bado haijapata fedha kutoka serikalini.
Alisema uboreshaji huo utaanzia ngazi ya vijiji ili kuondoa kero ya watu wanaokosa majina yao katika vituo vya kupigia kura.
“Nec ipo katika mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura kwa kutumia teknolojia ya kisasa, mfumo utakaotumika ni kama ule unaotumiwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)” alisema Jaji Lubuva.
Viongozi hao walipendekeza vitambulisho vya taifa vitumike katika upigaji wa kura, ombi ambalo lilipingwa na Nec kwa maelezo kuwa vitambulisho hivyo haviwezi kuwa mbadala wa vitambulisho vya kupigakura.
Katika maelezo yake, Jaji Lubuva alisema Februari 9 mwaka huu, utafanyika uchaguzi wa udiwani katika Kata 27 Tanzania Bara na kwamba katika uchaguzi huo daftari la wapigakura litakalotumika ni lile lililotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
“Kutokana na hali halisi hatuwezi kufanya mabadiliko katika daftari la wapigakura ili tuwahi tarehe ya uchaguzi wa udiwani katika kata hizi, lakini katika upigaji wa kura ya maoni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, daftari litakuwa limeboreshwa,” alisema.
Hoja ya kutaka kuboreshwa kwa daftari hilo ilitawala katika mkutano huo ambapo Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa, waliowaongoza viongozi wengine kumbana Lubuva, ambaye alikiri wazi kuwa suala hilo limekuwa kikwazo kwa wananchi.
No comments
Post a Comment