Writen by
sadataley
12:06 PM
-
0
Comments
Morogoro. Waethiopia 17 wanashikiliwa na Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kuingia nchini kinyume na taratibu, huku wakiwa wametelekezwa katika Pori la Kijiji cha Mangae Kata ya Melela wilayani Mvomero.
Kushikiliwa kwa Waethiopia hao kunatokana na baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Mangae kutoa taarifa baada ya kuwaona wakiwa kundi kubwa, huku wakizungumza lugha wasiyoielewa na kisha kutoa taarifa kwa idara hiyo ya uhamiaji.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za uhamiaji Mkoa wa Morogoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji, Msafiri Shomari alisema Waethiopia hao walikamatwa Novemba 30 mwaka huu asubuhi katika Kijiji cha Mangae Kata ya Melela baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi.
Alisema kuwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa na kufanyika kwa utaratibu wa kurudishwa nchini mwao.
“Elimu ya uhamiaji shirikishi imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa watu wanaoingia kiholela nchini bila utaratibu,”alisema kamishna huyo
Akielezea namna walivyowaona Waethiopia hao katika pori la kijiji hicho, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mlinge Mangae,Kadili Kwizi alisema kuwa alipata taarifa kutoka kwa mwananchi aliyekuwa akichanja kuni kuwa amewaona watu ambao si jamii ya pale na wamekuwa wakiongea lugha isiyoeleweka na kutoa taarifa kituo cha polisi Doma.
Alisema walijaribu kuwakagua watu hao lakini hawakuwa na silaha ya aina yeyote,na baadae waliwapatia chakula baada ya Waethiopia hao kuonyesha ishara ya kusikia njaa.
Mmoja wa Waethiopia hao aliyejitambulisha kwa jina la Ayono Abriham(25) akizungumza kwa taabu lugha ya Kiingereza alisema sababu kubwa inayowafanya kukimbia nchini mwao ni maisha magumu,kutokuwa na chakula,hakuna kazi na hata kupatikana kwa mavazi ni taabu.
Ayono alisema walilipa kiasi cha fedha ya kiethiopia 75,000 na wamekuwa wakiahidiwa kupatiwa kazi Afrika kusini na kwamba maisha ya nchi hiyo ni rahisi.
No comments
Post a Comment