Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Monday, November 4, 2013

Tusiache siasa ichague mfumo wa elimu

Profesa Sifuni Mchome PICHA|MAKTABA 
Na Mwananchi
Kwa muda mrefu sekta ya elimu nchini imepitia mabadiliko mengi, pia kuzua hoja na maswali mengi yakiwamo ya siasa kuachwa itawale mfumo wa utoaji elimu katika nchi yetu.
Hali kadhalika, sekta hii imekutana na changamoto lukuki, zikiwamo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakieleza kwamba elimu yetu inashuka kwa kiwango cha kutisha.
Hadi sasa zimetolewa sababu nyingi za kuporomoka kwa kiwango hiki cha elimu katika Tanzania katika miaka ya karibuni ambazo zinahusisha pande mbalimbali. Pande hizo ni pamoja na walimu, wanafunzi, wazazi au walezi, mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambayo ni pamoja na madarasa, maabara, vitabu, ukosefu wa motisha hasa kwa walimu, utoro wa wanafunzi, mimba na kadhalika.
Ikumbukwe kuwa katika miaka ya karibuni ukiwamo mwaka jana, tumeshuhudia kushindwa vibaya kwa wanafunzi wetu waliohitimu kidato cha nne.
Matokeo hayo mabaya yaliiduwaza, kuilazimisha Serikali kuyafuta, kutaka usahihishaji, upangaji matokeo ufanyike upya na yote yalifanyika.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Serikali aliunda tume maalumu ili kuchunguza na kubaini kilichotokea.
Miongoni mwa kazi za tume ile zilikuwa ni kuchunguza na kubaini upungufu wote uliotokea na kisha kupendekeza ni hatua gani zinafaa kuchukuliwa.
Hata hivyo, ripoti ya tume hiyo ambayo iliongozwa na Profesa Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haijatolewa hadharani.
Ripoti hiyo imekuwa hata hivyo ikinukuliwa na vyombo vya habari ikionyesha upungufu mwingi katika elimu nchini.
Hali ikiwa bado ni hivyo, wiki hii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza mfumo mpya wa kutoa matokeo ya kidato cha nne na sita ambao utaanzia na wahitimu wa kidato cha nne ambao wanaanza mitihani yao kesho.
Uamuzi huo ambao umetangazwa na Profesa Mchome tayari umezua maswali mengi kutoka kwa wadau wakihoji kama kweli unalenga katika kuinua au kuporomosha zaidi kiwango cha elimu.
Wengine wameukosoa mfumo huo kwamba umefanyika zaidi kisiasa, unalenga katika kuwafurahisha wakubwa, hauna uhalisia na mazingira halisi ya elimu katika nchi yetu.Nasi, kama wadau wa elimu nchini bado tunajiuliza ni wapi tuendako katika mipango yetu ya elimu na endapo mfumo huo utakuwa mwarobaini wa kuondokana na matokeo mabaya katika mitihani kwa vijana wetu, upungufu ambao umekuwa ukiendelea nchini katika miaka ya karibuni.
Tunaamini, mabadiliko haya katika mfumo huo wa mtihani ambayo yanahusisha maendeleo ya mwanafunzi darasani, mtihani wa kidato cha pili, mihula kwa kidato cha tatu na nne, unaweza kuwa mzuri, lakini unahitaji kufanyiwa utafiti zaidi.
Wasiwasi wa wengi likiwamo Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) ni kwamba baadhi ya walimu si makini katika kuandaa na kutuma maendeleo ya kila siku ya wanafunzi wao, kwa hali hiyo huenda tukafaulisha hata wale wasiostahili.
Tunaungana na wadau hao kuamini kuwa Tanzania inajichimbia kaburi katika elimu kwani mbele ya safari itakuwa na wahitimu wengi lakini wasiokuwa na uelewa wa kutosha, wasioweza kushindana na wenzao kutoka nchi jirani za ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Kwa maana hiyo, tunashauri wadau na wizara wakutane, wauangalie kwa umakini mfumo huu mpya ambao ukichukuliwa kama mzaha unaweza kuwa kaburi letu kielimu.
Tunasema kama nchi hatujachelewa, lakini lazima kila mmoja akubali kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha tunakuwa na wahitimu walioandaliwa vizuri na kuiva, walimu wanaofanya kazi kwa moyo, uzalendo wala si kwa kuangalia mitihani, bali mtalaa wa elimu, mafunzo katika nchi yetu.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment