Writen by
sadataley
12:11 PM
-
0
Comments
WAKRISTO nchini wametakiwa kutambua kuwa uongozi ni huduma ambayo ni haki ya kila mmoja kupata bila masharti magumu na kupata mahitaji kadiri ya makubaliano ya nafasi za huduma.
Kauli hiyo imezungumzwa leo na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa alipokuwa katika maadhimisho ya Misa Takarifu iliyokuwa kwa ajili ya kufunga Mwaka wa Imani kijimbo iliyofanyika katika viwanja wa Kichangani jimboni Iringa.
Mhashamu askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni askofu wa jimbo la Iringa na Msimamizi wa Kitume katika Jimbo Kuu la Songea amesema baadhi ya wakuu wa mataifa huwatawala kwa nguvu watu wao na kuwakosesha amani na haki huku wengine wakiishi kwa wasiwasi.
“Tunapofunga mwaka wa imani tunapata nafasi ya kutafakari dhana ya utawala na uongozi bora. Wakuu wa mataifa huwatawala kwa nguvu. Wengi wanaotafuta uongozi, huingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta madaraka na wengi wao huiongia kwa kutafuta maslahi binafsi” amesema askofu Ngalalekumtwa.
Amesema binadamu anadaiwa kufanya marekebisho ya maisha kwa kuishi kadiri ya maagizo ya Mungu kwa kuishi kwa amani na upendo kwa kutanguliza haki na kuwajibika ipasavyo kwa wengine.
“Uongozi ni kuwatanguliza wengine katika mawazo na katika utendaji. Uongozi ni utii na utumishi mwema” amesema.
Amesema viongozi wa njanja zote wanapaswa kufanya tathmini ya utawala wao na kufanya marekesho pale walipokosea na kuwakwaza wale waliopa dhamana hiyo.
Amesema kila wakati kutawala kwa mabavu ni kuleta mvutano na kuwavuruga watu duniani na kuwafanya kuishi bila amani kinyume na mpango wa Mungu anayependa watu wote duniani waishi kwa amani, upendo na kuheshimiana.
Adhimisho hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kiserikali na kuhusisha Parokia zote 37 za Jimbo la Iringa.
Habari na picha kwa hisani ya mtandao wa gustav chahe
No comments
Post a Comment