Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) Salum Mayanga, ameeleza kusikitishwa na taarifa zinazosambaa kuwa hajachagua mwenyewe kikosi cha timu hiyo kwaajili ya mechi za kirafiki bali amechaguliwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka Tanzania TFF imeeleza kuwa Mayanga hajafurahishwa na taarifa hizo za uzushi kwani yeye anafanya kazi kwa mujibu wa taratibu za kazi yake hivyo hawezi kuchaguliwa timu.
''Watu waache kupotosha umma, mimi ndio nimechagua kikosi chote kilichosafiri kwenda Algeria na si vinginevyo, kocha Ahmed Morocco nilimwachia jukumu la kutangaza kikosi tu baada ya uteuzi'', amesema Mayanga.
Taarifa hizo zilianza kusambaa usiku wa Machi 22 baada ya Taifa Stars kuchapwa mabao 4-1 na Algeria ugenini, kwenye mchezo wa kirafiki wa kalenda ya FIFA kwa mwezi Machi.
Taifa Stars inatarajia kumaliza mechi zake za kirafiki Jumanne ijayo Machi 27 itakapowakaribisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es salaam. Tayari viingilio vya mchezo huo vimewekwa wazi ambapo kiingilio cha chini ni shilingi 1,000.
No comments
Post a Comment