Writen by
sadataley
7 years ago
-
0
Comments
Waziri Mkuu mteule wa Ethiopia, Abiye Ahmed ataapishwa Jumatatu ijayo. Hayo yameelezwa na Bunge la Ethiopia baada ya muungano wa chama tawala kumchagua kwa ajili ya kuziba nafasi iliyoachwa na Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia aliyejiuzulu.
Muungano wa chama tawala Ethiopian People's Democratic Front Jumanne iliyopita ulimchagua Abiye Ahmed mwenye umri wa miaka 42 kuongoza serikali baada ya kujiuzulu Hailemariam Desalegn. Waziri Mkuu huyo mpya wa Ethiopia ni Luteni Jenerali msaatafu kutoka kabila kubwa nchini Ethiopia la Oromo.
Ethiopia ni nchi ya pili barani Afrika iliyo na idadi kubwa ya watu na ambayo imekuwa na uchumi unaokuwa kwa kasi zaidi barani humo katika muongo mmoja uliopita. Hata hivyo maandamano yaliyoanza nchini humo mwaka 2015 yamekuwa tishio kuu kwa chama tawala tangu kishike hatamu za uongozi mwaka 1991.
Bunge la Ethiopia litakuwa na kikao maalumu Aprili Pili kwa ajili ya
kumuapisha Dakta Abiye Ahmed kuwa Waziri Mkuu mpya wa nchi hiyo. Mtangulizi wake, Hailemariam Desalegn ambaye anatoka kabila dogo la Wollayta alijiuzulu mwezi uliopita baada ya kukabiliwa na mashinikizo na maandamano katika mikoa ya Oromiya na Amhara ambapo wakazi wake wamekuwa wakilalamika kuwa serikali imewaweka kando katika masuala ya kisiasa na kiuchumi.
Parstoday
No comments
Post a Comment