YANGA SC imefanikiwa kwenda Raundi ya Kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya sare ya 1-1 na wenyeji, Saint Louis Suns United jioni ya leo katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Uwanja wa Linite mjini Victoria, Shelisheli.
Mabingwa wa Tanzania wanasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya Februari 10 kushinda 1-0 pia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la kiungo Juma Mahadhi aliyekosekana uwanjani leo kwa sababu ya homa.
Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa Madagascar, Andofetra Avombitana Rakotojaona aliyesaidiwa na Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina na Pierre Jean Eric Andrivoavonjy, hadi maopumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji mjuzi wa kuuchezea mpira, Ibrahim Ajib Migomba dakika ya 45 akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia, Hassan Ramadhan Hamisi ‘Kessy’.
Kabla ya bao hilo, timu hizo zilikuwa zikishambuliana kwa zamu, ingawa hayakuwa mashambulizi ya kusisimua na ilikuwa kazi rahisi kwa safu zote za ulinzi kuokoa.
Katika kipindi hicho, ilishuhudiwa kila timu ikionywa kwa kadi ya njano, Herve Rakotoarison kwa upande wa Saint Louis dakika ya 16 na Nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa upande wa Yanga dakika ya 29.
Kipindi cha pili, Yanga iliendelea kusukuma mashambulizi langoni mwa wenyeji kujaribu kuunenepesha ushindi wao, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi.
Saint Louis wakasawazisha bao hilo dakika ya pili kati ya nne za nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida kupitia kwa Nahodha wake, Betrand Esther aliyefunga kwa kichwa baada ya mabeki wa Yanga kuzembea kuokoa mpira wa juu.
Katika kipindi hicho, refa Andofetra Avombitana Rakotojaona aliwaonyesha kadi za njano Elijah Tamboo wa Saint Louis na Kessy wa Yanga kwa makosa tofauti.
Kwa matokeo hayo, Yanga itakutana na mshindi kati ya El Merreikh ya Sudan na Township Rollers ya Botswana. Township Rollers ilishinda 3-0 nyumbani pia.
Saint Louis; Michael Ramandimius, Jean Paul Algae, Steve Henriette, Damien Maria, Betrand Esther, Travis Laurence, Herve Rakotoarison/Jude Nancy dk58, Tahiry Andriamandimby, Mervin Mathiot/Roddy Melanie dk58, Elijah Tamboo, na Karl Hall.
Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gardiel Michael/Mwinyi Mngwali dk77, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Raphael Daudi dk59, Pato Ngonyani, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin.
No comments
Post a Comment