Viongozi watano wa Chadema kati ya saba waliokwenda Kituo Kikuu cha Polisi kuitikia wito wa kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, wameachiwa kwa dhamana.
Walifika kituoni hapo leo Februari 20, 2018 saa 6: 10 mchana na kuachiwa saa 7:45 mchana.
Viongozi walioitwa na Mambosasa ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji, naibu makatibu wakuu John Mnyika (bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Pia wamo, mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee; mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni mweka hazina wa Bawacha.
Waliofika leo kituoni hapo na kuachiwa ni Bulaya, Mdee, Matiko, Heche na Mnyika.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mnyika amesema kupitia wakili wao, Peter Kibatala wamepewa dhamana na kutakiwa kuripoti tena kituoni hapo, Februari 27, 2018.
Amedai kuwa fununu zilizopo ni kwamba wanaweza kufunguliwa shataka la kuandamana bila kuwa na kibali.
"Tumefika hapa lakini hatujahojiwa hivyo tumepewa dhamana na tutaripoti siku ya Jumanne wiki ijayo,” amesema.
Wito wa viongozi hao polisi umekuja siku siku nne tangu kutokea kwa kifo cha Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usfairishaji (NIT).
Akwilina aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 16, 2018 akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.
No comments
Post a Comment