Writen by
sadataley
3:49 PM
-
0
Comments
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin.
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin akiwa amebakiza siku chache kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu, ameanika kiasi cha fedha alizojipatia kipindi cha miaka mitano iliyopita ambacho si kikubwa kama ambavyo ilifikiriwa.
Taarifa iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Shirikisho la Urusi imeeleza kuwa, Rais Putin alijipatia mapato ya Rouble Milioni 38.5 za Urusi sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 1.9 kati ya mwaka 2011 na 2016.
Hiyo maana yake ni kwamba kiongozi huyo wa nchi ya Urusi ana mshahara wa Dola za Kimarekani 143,000 kwa mwaka.
Fedha hizo hazizidi hata theluthi moja ya ule anaopokea Waziri Mkuu wa Australia, Malcom Turnbull ambaye hulipwa Dola za Kimarekani 527,852.
Kwa mujibu wa Gazeti la Washington Post, Rais Putin pia ameorodhesha akaunti 13 za benki mbalimbali ambazo kwa pamoja zina akiba ya Dola za Kimarekani 307,000 sawa na zaidi ya shilingi milioni 650.
Rais Putin pia ameorodhesha kumiliki nyumba zake mjini St Petersburg, hisa katika benki moja pamoja na magari mawili ya kimichezo ya nyakati za uliokuwa Muungano wa Kisovieti wa Urusi (USSR).
Ingawa mshahara wa Rais Putin unaweza kuwa mdogo ikilinganishwa na viongozi wengine duniani, ni mkubwa mno ikilinganishwa na wanaopata raia wa Urusi.
Raia wa Urusi kwa wastani hupata Dola za Kimarekani 8500 kwa mwaka nao hupata watu wachache.
Vyombo vya habari vya Urusi vimeripoti hivi karibuni kuwa Rais Putin alitakiwa kutoa takwimu za kipato chake na mali alizonazo kama sehemu ya mchakato wa usajili kwa wagombea urais kutokana na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Machi 18 mwaka huu.
Taarifa hizo zimekuja huku wakosoaji wake wakidai kwamba Rais Putin ana utajiri wa kupindukia na wakimuweka daraja moja na hata zaidi ya matajiri mabilionea wa dunia.
PUTIN NI NANI?
Rais Putin alizaliwa Oktoba 7, 1952 na ni Mwenyekiti wa Chama cha Kisiasa cha Muungano wa Urusi na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Umoja wa nchi hiyo wa Belarus.
Ratiba ya kila siku ya Vladimir Putin ina mambo mengi zikiwemo saa kadhaa za kuogelea, kuchelewa kulala, kutokunywa pombe kabisa. Unapotaka kumfurahisha Rais wa Urusi, Vladimir Putin, mpatie vitu viwili, mbwa mtukutu kabisa na kifungua kinywa cha mayai ya ndege wa porini aina ya tombo. Jarida la Newsweek la Marekani limeripoti kuwa vitu hivyo vinapatikana kutoka “mashamba ya rafiki yake ambaye ni kiongozi wa dini nchini Urusi anayeitwa Kirill.
Hiyo ni kwa mujibu wa wasifu wa Putin ulioandikwa mwaka 2014 na mwandishi wa jarida la Newsweek, Ben Judah aliyetumia miaka mitatu kumfanyia utafiti Rais huyo wa Urusi kwa ajili ya kitabu chake kinachoitwa, “Fragile Empire: How Russia Fell in and Out of Love with Vladimir Putin.”
Rais huyu wa Urusi hivi karibuni amekuwa akitajwa nchini Marekani kwa mambo mbalimbali ikiwamo kufanya utafiti unaolenga kubaini kampeni za Rais wa Marekani Donald Trump, msimamo wake juu ya mgogoro nchini Syria na alichokiongea kuhusu Marekani kujitoa katika majadiliano ya hali ya hewa nchini Ufaransa.
LAKINI AKIWA NYUMBANI KWAKE MAMBO YAKOJE?
Alikaimu kiti cha urais mnamo Desemba 31, 1999 mara baada ya Rais Boris Yeltsin kujiuzulu ghafla, na kisha Putin akashinda uchaguzi wa rais mwaka 2000. Mwaka 2004, alichaguliwa upya na kushinda, hivyo kuendelea na kipindi chake cha pili hadi Mei 7, 2008 kabla ya kuachia utawala wa nchi kwa Damitry Medvedev aliyeshinda kiti cha urais.
Medvedev kwa kutambua umuhimu wa Putin, mara moja alimteua kuwa Waziri Mkuu katika kile kilichoelezwa kuongoza kwa pamoja bila kinyongo (tandemocracy).
Jina lake lina asili ya watu wa mashariki mwa Urusi likiwa na maana ya mila katika mji wa Leningrad alikozaliwa.
NI LUTENI KANALI
Kwa miaka 16 Putin alikuwa Ofisa Mwandamizi wa Jeshi la Urusi likifahamika kwa kifupi KGB, akipanda cheo hadi kufikia Luteni Kanali kabla ya kujiuzulu na kuingia kwenye siasa akijiunga na chama kilichoanzishwa huko Saint Petersburg, mwaka 1991.
Baada ya kuwa kwenye chama hicho kwa miaka mitano, mwaka 1996 alihamia jijini Moscow kuungana na utawala wa Rais Boris Yeltsin ambako alipaa kwa haraka hadi kuteuliwa kuwa kaimu rais Desemba 31, 1999 baada ya Yeltsin kujiuzulu ghafla.
Septemba 2011, Urusi ilifanya Marekebisho ya Katiba yake katika kipengele cha muda wa rais kukaa madarakani. Marekebisho ya kutoka miaka minne hadi sita na Putin akatangaza kuwania madaraka ya urais kwa mara ya tatu katika uchaguzi uliofanyika Machi 2012.
Nia hiyo ya Putin ilipingwa kwa maandamano katika miji mbalimbali nchini Urusi, lakini alipambana na kushinda. Mipango mingi ya Putin haipiti kwa wepesi kwani huwa inakutana na changamoto au vikwazo vingi kutoka kwa watu wa kawaida hadi hata waangalizi wa kimataifa kuona kuwa demokrasia imekiukwa, lakini mwisho wa siku, anashinda.
Tangu mwaka 2011, Putin amekuwa mbabe akitangaza Urusi yenye mabadiliko ya kweli katika kila sekta badala ya kuwa na serikali isiyo na mamlaka.
Muungwana blog
No comments
Post a Comment