Majadiliano kati ya Kamati Maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli na wawakilishi kutoka kampuni ya madini ya Barrick Gold juu ya biashara ya madini yanayochimbwa na migodi ya kampuni hiyo nchini yalianza jana Jijini Dar es Salaam,-
huku Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi akiahidi kusimamia vizuri maslahi ya nchi.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana ilisema Prof. Kabudi ambaye ndiye kiongozi wa kamati maalumu hiyo kwenye mazungumzo hayo alisema wamejipanga vizuri kujadiliana na Barrick juu ya madai ya Tanzania katika biashara ya madini ya kampuni hiyo hapa nchini na kwamba itahakikisha inasimamia maslahi ya Tanzania ipasavyo.
Kampuni tanzu ya Barick Gold, Acacia ilitoa taarifa mwanzoni mwa wiki iliyopita ikieleza kuwa imepokea kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) hati ya madai ya jumla ya Sh. trilioni 425.
Taarifa hiyo ilisema TRA ilionyesha katika taarifa hiyo kuwa mgodi wa Acacia wa Bulyanhulu unadaiwa kodi ya tangu mwaka 2000 na Pangea unadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.
Taarifa ya TRA kwa Acacia inafuatia ripoti ya tume mbili za Rais Magufuli ambazo Mei na Juni, mwaka huu ziligundua udanganyifu mkubwa katika biashara ya makinikia ya Acacia.
Moja ya ripoti hizo ilionyesha kuwa nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.
Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa sh. trilioni 108 na kamati ya wachumi na wanasheria iliyoongozwa na Prof. Aidan Osoro wa Idara ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Wakati kamati ya Tanzania katika mazungumzo yaliyoanza jana ikiongozwa na Prof. Kabudi, kamati ya Barrick Gold inaongozwa na Afisa Mwendeshaji Mkuu, Richard Williams, taarifa ya Ikulu ilisema na kueleza zaidi:
"Kwaupande wake, Richard Williams ameshukuru kuwepo kwa majadiliano hayo na amesema Kampuni ya Barrick Gold Corporation imeyapokea madai ya Tanzania kwa mtazamo chanya na ipo tayari kujadiliana na kufikia makubaliano yenye maslahi kwa pande zote mbili."
Mazungumzo hayo yanafanyika ikiwa ni mwezi mmoja na nusu tangu Mwenyekiti wa Barrick Gold, Prof. John Thornton kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu na kukubali kulipa fedha ambazo nchi imezipoteza kutokana udanganyifu ambao uligundulika kwenye biashara ya mchanga wa madini.
Uchambuzi uliofanywa na TRA, kwa mujibu wa taarifa ya Acacia, ulionyesha kuwa mgodi wake wa Bulyanhulu unadaiwa na mamlaka Sh. trilioni 344.8 na mgodi wa Pangea Sh. trilioni 76.1.
Hivyo madai hayo ya TRA yalionyesha kuwa Acacia inadaiwa Sh. trilioni 89.5 ikiwa ni malimbikizo ya kodi na Sh. trilioni 335.9 za adhabu na riba.
WAKATI MGUMU
Acacia ilikuwa katika wakati mgumu hata kabla ya ripoti ya Prof Osoro ya Juni 24, baada ya kamati ya kwanza iliyoteuliwa na Rais Magufuli Machi 29, ikiwa na wajumbe nane wenye taaluma za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini, kuchunguza kiwango cha madini kwenye makontena yenye makinikia kuonyesha kuwapo kwa udanganyifu.
Acacia ilikuwa msafirishaji mkuu wa makinikia nchini kabla ya Rais Magufuli kuagiza kusimamishwa Februari, mwaka huu.
Kamati hiyo maalumu ilikuwa chini ya uenyekiti wa Profesa wa masuala ya miamba, Abdulkarim Mruma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Rais Magufuli alizuia makontena 277 ya makinikia ya Acacia yaliyokuwa yanasafirishwa kwenda kuchenjuliwa ughaibuni Machi 23, kisha akaunda kamati hizo mbili kufuatilia kilichokuwamo baada ya kuwapo kwa hisia za udanganyifu wa kiasi halisi cha madini kilichomo kwenye mchanga huo.
Baada ya kamati ya kwanza kumkabidhi ripoti ya uchunguzi Mei 24, Rais Magufuli alichukua uamuzi wa kusitisha upelekaji mchanga nje ya nchi mpaka itakapoelezwa vinginevyo baadaye.
Aidha, Rais Magufuli aliwawajibisha baadhi ya watendaji wa serikali ikiwamo kutengua uteuzi wa Prof. Sospeter Muhongo kama Waziri wa Nishati na Madini.
Aidha, miongoni mwa mapendekezo ya kamati ya Prof Osoro ni kupiga marufuku usafirishaji mchanga nje na kujenga kiwanda cha kuchenjua makanikia hapa nchini, jambo ambalo Barick Gold, sasa, imeahidi kusaidia kufanikisha.
No comments
Post a Comment