MKUU WA IDARA YA HABARI NA MAWASILIANO WA KLABU YA SIMBA, HAJI MANARA.
TIMU ya Simba inatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Orlando Pirates itakayopigwa leo kwenye uwanja wa klabu hiyo ulioko jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mechi hiyo ni maalum kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu kwa michezo saba itakayochezwa kwenye viwanja saba tofauti hapa nchini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Haji Manara, alisema maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Omog, anatarajiwa kutumia wachezaji wengi zaidi ili kuwapa mazoezi na kupandisha viwango vyao.
Manara alisema kuwa Omog amefurahishwa na mazoezi yanayoendelea na ujio wa wachezaji waliokuwa kwenye timu ya Taifa (Taifa Stars) umeongeza ushindani katika kikosi hicho cha mabingwa wa Kombe la FA.
"Maandalizi ya mechi ya kesho (leo) yamekamilika na wenyeji wetu wamekubali kutukaribisha kwenye uwanja wao, tumefurahi kupata fursa hii ambayo itawasaidia wachezaji wetu kuimarika kiufundi na kujifunza mbinu kutoka kwa wenzao wanaoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini," alisema Manara.
Wakati huo huo, Manara alisema kuwa kipa mpya wa timu hiyo, Aishi Manula anatarajiwa kutua Afrika Kusini kuanza mazoezi na nyota wenzake tayari kwa msimu mpya.
"Manula anaondoka kesho (leo) kuanza mazoezi na hii ni baada ya kumalizana na klabu yake ya zamani ya Azam FC, tunaamini kambi yetu itazidi kuimarika huko Sauzi," alisema Manara.
Aliongeza kuwa baada ya mechi hiyo, Simba itashuka tena uwanjani keshokutwa kucheza mchezo mwingine dhidi ya Bidvest Wits na kujiandaa kurejea nyumbani Agosti 5, mwaka huu kwa ajili ya kutambulisha nyota wake katika tamasha la Simba Day litakalofanyika Jumanne ijayo.
No comments
Post a Comment