Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Sunday, July 23, 2017

Rais Magufuli: Sitakatishwa tamaa

RAIS John Magufuli ametoa ya moyoni na kusema watu wanaojaribu kumkatisha tamaa katika uongozi wake kamwe hawatafanikiwa, huku akisisitiza kwa kufanya hivyo ni kumwongezea kasi ya kupambana na mafisadi na wala rushwa, akilenga kunufaisha Watanzania kwa ujumla wao.

Aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma katika siku ya pili ya ziara yake mkoani humo. “Na kamwe sitakata tamaa, wale wanaojaribu kunikatisha tamaa ndio wanaongeza tamaa yangu ya kupambana nao na kitaendelea kuwatumbua,” alisisitiza.

Alisema anayafanya hayo ili kuwaletea maendeleo Watanzania, ndiyo maana anahakikisha anafanya kila linalowezekana kuhakikisha anakomesha tabia ya watu waliokuwa wanajinufaisha kwa rasilimali za nchi.

Aidha, kupitia mkutano huo, Rais Magufuli kwa mara ya kwanza alifichua siri ya kuwachagua baadhi ya viongozi kutoka vyama vya upinzani na kusema alifanya hivyo kwa kuwa wana akili na wanaweza kuwaletea tija wananchi.

“Kwanza maendeleo hayana chama na Watanzania tumechelewa mno haya mambo ya vyama yanapoteza muda, tumevikuta vyama ila maendeleo hayaangalii chama na ndio maana niliwateua hao kwa sababu ya akili na sio vyama vyao,” alisema Rais Magufuli.

Wakati akielezea siri hiyo, alimsimamisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo na kumwelezea kuwa ni kiongozi mwenye akili na anafanya kazi kwa weledi huku pia akimsifia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira wa Chama cha ACT-Wazalendo, kuwa pamoja na kuwa mwanachama wa chama kingine, ila anafanya kazi vizuri.

“Wote hao niliwachagua sikuangalia vyama vyao bali niliangalia uwezo wao na akili ya kuwatumikia Watanzania, vyama vyao sina haja navyo kwa kuwa maendeleo hayaangalii vyama,” alisema na kuongeza… “Ndio maana sichagui wapiga kelele kwa sababu hawawezi kuleta tija kwa Watanzania.”

Kabla ya uteuzi huo, Profesa Kitila aliyezaliwa miaka 46 iliyopita huko Iramba, mkoani Singida, alikuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Shule Kuu ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE) wakati Mghwira ambaye pia ni mzaliwa wa Singida, alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo.

Aligombea urais wa Tanzania mwaka 2015 akichuana na wagombea kadhaa, akiwemo Rais Magufuli. Alisema Watanzania wanachotaka ni maendeleo kwanza, na akatumia fursa hiyo kuitaka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha mradi wa maji unaotekelezwa mjini Kigoma uanze kufanya kazi ifikapo Novemba 30 mwaka huu ili wananchi wa mkoa Kigoma wapate maji kuanzia saa 12 asubuhi ya siku hiyo, na kwamba kinyume cha hapo hawataelewana .

“Watu wanataka maendeleo na ili kuondoa kutumia muda mwingi kutafuta maji ni lazima maji hayo yapatikane kwa urahisi na ya kutosha ili waweze kutumia muda mwingi kwenye shughuli za maendeleo badala ya kuhangaikia maji,” alisema na kusisitiza Serikali inataka kuiona Tanzania mpya kutokana na miradi inayotekelezwa ambayo inalenga kuboresha maisha ya Watanzana na kuona maisha ya Watanzania yanasonga mbele.

“Tutatekeleza yale yote ambayo yameahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM na nia kubwa ni kuona Watanzania wanakuwa na maisha bora, tunaomba mtuunge mkono kwa yale yote tunayofanya,” alisema.

Aliongeza kuwa, yapo mambo ambayo yamerudisha nyuma juhudi hizo ikiwemo vitendo vya rushwa na ndiyo maana serikali imetunga sheria ya kupambana na rushwa ili kuondoa kadhia hiyo ambayo ilikuwa kero kubwa kwa watanzania.

Rais Magufuli alisema anataka kuona Watanzania wakiwa salama, wenye kufurahi maisha, kwani mabilioni ya shilingi yalikuwa yakitumika isivyotakiwa na kwamba ameamua fedha hizo sasa zirudi zikatumike kuwasaidia Watanzania.

Alitumia fursa hiyo kuyaonya mashirika yanayohudumia wakimbizi kuacha kuhubiri suala la kuwaleta wakimbizi nchini ili kuwezesha kuomba misaada kutoka nje kwa kigezo cha kuwasaidia wakimbizi hao.

Alisema Burundi kuna amani na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkrunziza amekiri nchi yake ina amani, hivyo shirika litakalobainika kuhubiri kuwataka wakimbizi kuja nchini ili kuishi makambini watashughulikiwa.

Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge alisema utagharimu Sh bilioni 42 zilizotolewa na Jumuiya ya Ulaya (EU) kupitia Benki ya Ujerumani ikiwa ni sehemu ya Sh bilioni 164 zilizotolewa kwenye miradi mitano ya maji nchini.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 42 kwa siku kutoka lita milioni 21 zinazozalishwa sasa, huku lita milioni 15 tu ndizo zinazosambazwa kwa wananchi.

Awali, wakitoa salamu zao wabunge wa Kigoma, wakiongozwa na mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) walimshukuru Rais kwa kuwa mstari wa mbele kwenye masuala ya maendeleo na kusema wanaungana naye.

Jana, wananchi kadhaa uwanjani hapo walijitokeza wakibeba mabango ambayo baada ya kumaliza hotuba yake, Rais alizunguka kusoma mabango hayo na kuagiza mkuu wa mkoa huo pamoja na mkuu wa wilaya ya Kigoma kutenga muda kusikiliza kero za wananchi hao.

Alisema mabango hayo ya kero ni ishara kuwa bado wananchi wanaendelea kupata shida kutokana na utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi, hivyo utumbuaji unapaswa kuendelea.

“Nimeona mabango yote, yanayohusu kero ya ardhi nitamtuma waziri wa ardhi aje na hii imenipa moyo kwamba nipange siku nyingine nije kusikiliza kero na pia inaonesha bado utumbuaji unapaswa kuendelea kwa sababu wapo baadhi ya viongozi hawatimizi wajibu wao,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumzia maendeleo ya Kigoma, alisema yapo mambo muhimu ambayo hayakutekelezwa mkoani humo kwa wakati na kukiri kuwa serikali ilichelewa kuyafanya kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali na kuahidi kuyatekeleza hivi sasa. Imeandikwa na Fadhili Abdallah (Kigoma), Ikunda Erick (Dar).
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment