Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Wednesday, July 26, 2017

Panga vyuo vikuu latoa povu mamia

WAZIRI WA ELIMU, PROF, JOYCE NDALICHAKO.

NI povu! Baadhi ya wamiliki wa vyuo vikuu nchini, wanataaluma, wanafunzi na wazazi wametikiswa na taarifa ya Serikali ya kuzuia kufanyika kwa udahili wa vyuo na baadhi ya kozi za masomo kwa muhula ujao kutokana na kasoro mbalimbali.

Jana, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ilitoa taarifa kwa umma inayoeleza hatua iliyochukua ya kusitisha udahili wa wanafunzi wapya katika vyuo 19 na pia kozi za masomo 75 zilizokuwa zikitolewa kwenye vyuo mbalimbali nchini.

Taarifa hiyo ya TCU, ambayo ilitolewa na Kaimu Katibu Mtendaji wake, Prof. Eleuther Mwageni, ilifichua sababu ya kuchukua uamuzi huo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa sifa katika vyuo husika.

Miongoni mwa vyuo vilivyoguswa kwa namna mbalimbali na uamuzi huo wa TCU ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dodoma (UDOM), KCMC, Tumaini, Ruaha, Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), Kampala kampasi ya Dar es Salaam (KIU) na IMTU.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya wanafunzi ambao kozi wanazosomea zimefutiwa udahili walisema wameshtushwa na hatua hiyo na kuwapa hofu kuwa pengine, hata kama wao hawajaguswa moja kwa moja, hali hiyo inawapa hofu kuwa pengine sifa zao zitakuja kutiliwa shaka.

“Inashtusha kwa sababu kama kozi unayosomea umeambiwa kuwa haina sifa kutolewa na chuo chako, maana yake hata wewe unakuwa hujiamini tena. Unaweza kujawa hofu kuwa hapo baadaye itakuja kauli nyingine inayoweza kufuta sifa hata za kile mnachoendelea kukisomea,” mmoja wa wanafunzi aliiambia Nipashe.

Aidha, baadhi ya walimu wa kozi za masomo yaliyofutwa kwa kukosa sifa kwenye vyuo vyao waliiambia Nipashe kuwa tangazo hilo la TCU limewaathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu wanajua kuwa kwa waliopo, ajira zao zitakuwa shakani.

“Wanafunzi wapya wasipodahiliwa, maana yake chuo kitalazimika kupunguza baadhi ya watumishi wakiwamo wahadhiri wasaidizi na hilo linatishia mno ajira zetu,” alisema mmoja wa wahadhiri wasaidizi, lakini akikataa kuilaumu TCU kwa hatua waliyochukua.

Maoni tofauti kuhusiana na tangazo hilo la TCU yalitolewa pia na baadhi ya wazazi na wamiliki wa vyuo, wengine wakiunga mkono kwa kuwaepushia hasara endapo wangedahili watoto wao katika vyuo au kozi kwenye vyuo visivyo na sifa huku wengine wakilaumu kwa kutaka serikali kuvipa muda wa kutosha vyuo husika ili kushughulikia kasoro zilizoainishwa na hivyo kutoa fursa ya kudahiliwa kwa wanafunzi wapya.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARco), Danford Kitwana, alisema vyuo hivyo vitaathirika kifedha kwa kuwa vilishaweka bajeti na vinajiendesha kwa kutegemea ada za wanafunzi.

Alisema vyuo vidogo vitaathirika zaidi kwakuwa idadi ya wanafunzi itapungua na kushindwa kujiendeshwa kwa programu chache zilizobaki.

“Ilitakiwa kabla wangetangaza ili kila mmoja ajue anawekeza vipi,” alisema.

Alisema baadhi ya vyuo vimeshatumia mamilioni ya fedha kwa kutangaza progarmu hizo kwa lengo la kupata wanafunzi
“Kama TCU wamefanya kwa kuzingatia vigezo halisi, itakuwa sawa.

Lakini kwa TUDARCo kuna malalamiko. Wamesitisha shahada ya uzamili kwa madai kuwa inafundishwa na walimu wa Shahada ya Uzamili wakati ukweli inafundishwa na wakufunzi wenye shahada za Uzamivu wakiwa wa kudumu na wengine wa muda mfupi,” alisema.

Alisema athari nyingine ni kwa wanafunzi ambao watakosa nafasi za masomo na hivyo kusubiri hadi mwakani, na kwamba vilivyopo havitoshelezi kwa kuwa vina idadi maalumu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, alisema kilichofanywa na TCU ni utekelezaji wa sheria ya vyuo vikuu ya mwaka 2005, inayotaka kufanyika uhakiki katika maeneo ya taaluma ili kuhakikisha elimu inatolewa kwa ubora unaotakiwa.

“Sekta ya elimu ya juu imekua sana. Kuna vyuo vingi nchini hivyo uhakiki umefanywa na kuthibitisha kuna vyuo havikidhi haja… ili kuimarisha sekta ya elimu ya juu, kuboresha kiwango cha elimu, ni lazima kuimarisha taasisi ziwe na uwezo wa kuendesha hizo programu,” alisema.

Alisema baadhi ya vyuo vilibainika kuwa na uwezo mdogo wa kutoa elimu katika maeneo mengine hivyo kwa sasa wanaweza kutoa kwa ngazi za chini ambazo hazikuwa na uwekezaji wa kutosha.

Alisema vyuo vingi vilianzishwa lakini baadhi havitoi elimu stahiki, na baadhi vilianzishwa ilhali vikiwa havina mazingira mazuri ya kujifunzia, hawana walimu wenye sifa, hawana maktaba wala vifaa vya maabara.

“Mimi navijua vingi tu. Nimekataa kuwa mtahini wa nje wa hivyo vyuo, kuna programu zimesukwa tu, hazina utaratibu,” alisema na kuongeza:

“Lazima kuwekeza kwenye sekta husika kwakuwa na walimu wenye sifa walioandaliwa vizuri na wenye uwezo wa pekee… wawe na shahada ya uzamili na kama hawapo tunakuwa na mashaka makubwa. Ndiyo maana wasomi wengi wanapuuzwa mtaani.”

‘PANGA’ LA TCU KWA VYUO
Katika taarifa yake jana, TCU ilitangaza kufuta udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vikuu 19 nchini kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kushindwa kutimiza msharti kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu Prof. Mwageni, uhakiki wa vyuo vikuu ulifanyika nchini nzima kati ya Septemba na Oktoba mwaka jana ili kuhakiki ubora wa elimu inayotolewa.

Alisema ripoti ya uhakiki ilionyesha upungufu aktika maeneo kadhaa kwenye baadhi ya vyuo na hivyo kufikia uamuzi wa kusitisha udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2017/18.

Vyuo vilivyofungiwa kufanya udahili kabisa ni Kilimanjaro Christian Medical University College (KCMCo), Eckenforde Tanga, Jomo Kenyatta Arusha, United African, IMTU na Chuo Kikuu cha Bagamoyo.

Vingine ni St. Francis University College of Health and Allied Science, Archibishop James, Archbishop Mihayo, Chuo Kikuu cha Kumbukumbu cha Cardinal Rugambwa, Chuo Kikuu cha Kampala Kituo cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Marian na St. John University of Tanzania Msalato Center, St. John University of Tanzania Kituo cha Marks, St Joseph University College of Engineering and Technology, Teofilo Kisanji Mbeya na Tumaini kituo cha Mbeya.

“Kutokana na mapungufu (upungufu) katika vyuo mbalimbali, imeamriwa kwamba jumla ya programu 75 kutoka vyuo 22 nchini zimesitishwa kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/18,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Uamuzi huu hautawahusu wanafunzi wanaoendelea na masomo katika program na vyuo husika.”

Aidha, vyuo hivyo na progarmu zilizozuiwa kwenye mabano ni Hubert Kairuki Memoria University (shahada za uzamili sita), Chuo Kikuu cha Jordan (progarmu 10 za shahada) na St Joseph University College of Management and Commerce (program mbili) na Chuo Kikuu cha St Johns (mkoja).

Vingine na idadi ya program za shahada zilizozuiwa kwenye mabano ni Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (5), Chuo Kikuu cha Mount Meru kituo cha Mwanza na Arusha (11), Chuo Kikuu cha St. John Tanzania (10) ikiwa ni za shahada ya kwanza na shahada ya uzamili.

Vingine ni Chuo Kikuu cha Mwenge Catholic (moja), Chuo Kikuu cha Ruaha Catholic (saba), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (moja), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (mbili), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji Dar es Salaam (moja), Chuo Kikuu cha Arusha Tawi la Buhare (moja) na Chuo Kikuu cha Iringa (tatu).

Vingine ni Chuo Kikuu cha kumbukumbu ya Abdulrahman Al-Samait (Sumait-mbili), Chuo Kikuu cha Kiislam Morogoro (tano), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM-mbili), Chuo Kikuu cha Dodoma (mbili), na Taasisi ya Ustawi wa Jamii (moja).

Aprili mwaka huu, TCU ilitangaza utaratibu mpya wa udahili wa wanafunzi ambao sasa wataomba moja kwa moja vyuoni na maombi hayo yataanza kupokewa rasmi Julai 22 hadi Agosti 13, mwaka huu. Aidha, masomo yataanza rasmi Oktoba 30 na vyuo vyote vitafunguliwa Novemba 6, mwaka huu.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment