Writen by
sadataley
1:00 PM
-
0
Comments
Jovina Bujulu – MAELEZO
Mizigo mikubwa waliyonayo
wanawake ni miongoni mwa changamoto za kijamii ambazo zimekuwa kikwazo
kwa wao kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa.
Hayo yamesemwa na Balozi Getrude
Mongella ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Bunge la Afrika alipokuwa
akizungumzia ushiriki wa wanawake katika siasa nchini.
“Changamoto kubwa ni pamoja na
teknolojia duni ambayo inamlazimisha mwanamke kuendelea kulima kwa
kutumia jembe la mkono, kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kutafuta
kuni na suala zima la kulea watoto” alisema Balozi Mongella.
Akizungumzia suala la teknolojia
duni alisema kuwa katika nchi zinazoendelea hilo limeendelea kuwa tatizo
kubwa na kwa kuwa wanawake ndio wazalishaji mali wakubwa, wamejikuta
wanaweka nguvu zao nyingi katika matumizi ya jembe la mkono. Hivyo
ukulima kwa kutumia jembe la mkono haukidhi mahitaji yao ya chakula
katika familia na kujikuta wamebaki kuwa omba omba.
Pamoja na changamoto hizo Balozi
Mongella amesema kuwa ushiriki wa wanawake bado ni mkubwa na ameitaka
jamii kuwawezesha kubeba baadhi ya mizigo kwa mfano kuimarisha huduma za
afya ya jamii.
Balozi Mongella alitoa ushauri
kwa jamii kutokukaa kimya bali kuzungumzia changamoto hizo na utatuzi
wake ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wanaume, kwani wakielimika na
kutumika vizuri baadhi ya changamoto zitaondoka na kasi ya mwanamke
kupiga hatua itakuwa kubwa.
Aidha, alivitaka vyama vya
wanawake kuamka na kuendeleza mapambano ya kumkomboa mwanamke kwani
ajenda ya wanawake ni ya kudumu na haijakamilika hata kidogo.
Zaidi ya hayo, Balozi Mongella
amewataka wanawake kutambua nafasi yao katika kuchangia uchumi wa taifa,
ili wafike mahali waonyeshe mchango wao katika Tanzania ya viwanda
ambayo Watanzania wanaitaka na kuwashauri wanawake waliopata elimu
kusaidia kuwavusha wanawake wengine.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha
ACT-Wazalendo ambaye alikuwa Mgombea Urais pekee mwanamke katika
uchaguzi uliopita wa 2015, Mama Anna Mgwira alisema wanawake wakipewa
nafasi wanajitoa kwa ukamilifu hivyo aliwataka wasimamie nafasi zao huku
wakifanya kazi kwa weledi, uaminifu, wajiheshimu na wawajibike ili
kuondokana na dhana ya kwamba hawawezi kazi bila kusimamiwa na
kusaidiwa.
No comments
Post a Comment