Writen by
sadataley
12:44 PM
-
0
Comments
1.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo akimsikiliza Mkandarasi wa
ujenzi wa mradi wa maji Wilunze Enock Masanja.
1.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo akikagua mradi wa maji
Wilunze wilaya ya Chamwino.
.....................................................................................................................................................
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo amefanya ziara ya kutembelea mradi wa maji katika
kijiji cha Wilunze wilaya ya Chamwino na kutoa mwezi mmoja kwa Mkandarasi wa
ujenzi wa mradi huo kukamilisha kutokana na utekelezaji wake kuwa wa muda
mrefu.
Jafo alitoa agizo hilo jana alipokuwa akikagua mradi huo ambao
ujenzi wake umeanza mwaka 2013.
Akizungumza katika ukaguzi huo, Jafo alisema utekelezaji wake
umesuasua hali inayosababisha wananchi wa eneo hilo waendelee kupata adha ya
maji na kuiagiza Halmashauri ya Chamwino kuzuia fedha ya mkandarasi huyo
zilizosalia kwa kipindi cha miezi mitatu mpaka ubora wa mradi huo
utakapoonekana.
Hata hivyo alisema mkandarasi aitwaye M/S Kijima fedha aliyopewa
hadi sasa haiendani na kazi iliyofanyika huku akitilia mashaka mabomba
yaliyowekwa kwamba yapo chini ya kiwango.
“Mkandarasi umepewa Sh. Milioni 305.7, gharama ya mradi kwa
ujumla ni Sh.Milioni 347.9, umebakisha fedha kidogo ambayo ni Sh.milioni 42.1
tukiangalia kazi iliyofanyika hata haiendani na fedha ulizopewa, unachokifanya
hapa ni kama maigizo huu mradi haujafikia asilimia 90 na haya mabomba
yanaonekana yapo chini ya kiwango maana yameanza kupasuka,”alisema Jafo
Aidha alisema Halmashauri hiyo imekuwa na uzembe katika
usimamizi wa miradi ya maji hali inayosababisha wananchi kukosa huduma ya maji
kwa wakati.
Jafo alimtaka Mkandarasi huyo kukamilisha mradi huo na kwamba
ifikapo Aprili 3, mwaka huu atarudi kukagua na kuiagiza serikali ya wilaya hiyo
kuwakamata watu watakaoharibu miundombinu ya maji.
Hata hivyo alisema katika miradi mingi ya maji aliyotembelea
amekutana na changamoto ya wakandarasi kuweka mabomba ambayo yapo chini ya
kiwango na kusababisha wananchi wanapokabidhiwa mradi kushindwa kuiendesha.
Naye, Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho ambaye pia ni Mwenyekiti
wa kitongoji cha Camp A, Waziri Sengoli, alisema wananchi wa kijiji hicho
wamekuwa wakipata adha ya maji ka takriban miaka saba huku akiwaumbua viongozi
wa Halmashauri hiyo kwamba wamekuwa hawatembelei kukagua mradi huo.
Kwa upande wake, Mkandarasi huyo Enock Masanja, alijitetea kuwa
ameshindwa kukamilisha mradi kwa wakati kutokana na kutopata fedha kwa wakati.
Chanzo: Matukiodaima Blog
No comments
Post a Comment