Writen by
sadataley
2:01 PM
-
0
Comments
Waziri MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali haina kipingamizi na wazo la kuifanya hospitali ya
rufaa ya Haydom kuwa ya kanda kwani hatua hiyo itaupunguzia mzigo
Serikali.
“Serikali hii ni sikivu, na
kuifanya hospitali hii kuwa ya kanda ni kazi ndogo. Kwa hiyo nitamleta
Waziri wa Afya aje awaongoze kusimamia vigezo vya kuifanya hospitali hii
iwe ya kanda,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Jumatatu, Februari 20, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa
kata ya Haydom kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa
kata.
“Serikali haina kipingamizi na
wazo lenu, cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe. Kwa hiyo, nitamleta
Waziri wa Afya awasaidie kuangalia vigezo,” amesisitiza.
“Kama vigezo havipo, tushirikiane
kuvikamilisha kwa sababu uwepo wa hospitali hii kwa hadhi ya kanda
kunaisadia Serikali kutokana na nafasi yake kijiografia,” amesema Waziri
Mkuu
“Nia yetu ni kupunguza gharama kwa
mgonjwa anayelazimika kutoka Simiyu hadi Bugando (Mwanza) au kutoka
Arusha hadi Muhimbili (Dar es Salaam). Hapa ni katikati na nimearifiwa
kuwa wagonjwa kutoka mikoa mitano ya Tabora, Simiyu, Arusha, Singida na
Manyara wanafika hapa kupatiwa matibabu,” amesema.
Amesema Serikali imepokea maombi
kwa ajili ya watumishi wanaotakiwa kwenye hospitali hiyo na kwamba hivi
karibuni itaajiri watumishi kati ya 5,000 hadi 6,000 wa sekta ya afya
peke yake. “Tumekwishaanza kuajiri, tumeanza na sekta ya elimu kwa
kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa fani ya sayansi. Na sekta
inayofuata ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90 wanaohitajika
watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” amesema.
Hospitali hiyo inahudumia wananchi kutoka wilaya nane za Mbulu, Hanang, Babati, Karatu, Mkalama, Iramba, Kondoa na Meatu.
Wakati huohuo, Balozi wa Norway
nchini Tanzania, Bibi Hannamarie Kaarstad ambaye alikuwepo kwenye
mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa na Serikali ya
Tanzania kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa hospitali walioko
Norway.
“Hospitali ya Haydom ni mahali
thabiti ambapo mshikamano baina ya Tanzania na Norway unaweza kuonekana
kwa dhahiri. Nawashukuru watumishi wa hospitali kwa moyo wao wa kujitoa
kuwahudumia wananchi wa wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani,” amesema.
Hospitali hiyo ambayo inaendeshwa
na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa
ufadhili kutoka Serikali za Tanzania na Norway, ilianzishwa mwaka 1955
ikiwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50. Hivi sasa ina uwezo wa kulaza
wagonjwa 420 kwa wakati mmoja.
Pia inatoa huduma za upasuaji,
magonjwa ya macho, tiba ya mifupa na mazoezi ya viungo. Ilipandishwa
hadhi kuwa ya rufaa baada ya mkoa wa Manyara kuanzishwa.
Mapema, akisoma taarifa kwa Waziri
Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Emanuel Q.
Nuwass alisema wameomba kibali cha ajira kwa watumishi 90 kupitia bajeti
ya mwaka 2016/2017.
“Tumeomba pia hospitali ipandishwe
hadhi na kuwa ya rufaa ya kanda (Kaskazini kati au Kanda maalum) ili
iweze kutoa huduma bora kwa mkoa wa Manyara na mikoa jirani kwani
wahisani wa maendeleo wako tayari kuchangia ujenzi wa miundombinu,”
alisema.
Pia aliomba waongezewe ruzuku ya dawa ikilinganishwa na ya sasa hivi ambayo ni asilimia 15 na pia waongezwe malipo ya on call allowance kwa ajili ya madaktari na watumishi wengine wa hospitali hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 20, 2017.
No comments
Post a Comment