Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Wednesday, February 22, 2017

Madiwani wawasha moto wataka Simbachawene atoe tamko


BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Meru limemtaka Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, kutoa tamko juu ya kitendo cha mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Christopher Kazeri, kuwafungia nje ya ukumbi wa mikutano.

Licha ya kuwafungia nje ya ukumbi, inadaiwa mkurugenzi huyo aliagiza kuficha majoho yanayotumiwa na madiwani hao wakati wa vikao.

Tukio hilo lilitokea juzi katika kikao cha pili cha baraza hilo baada ya kikao cha kwanza kilichofanyika Ijumaa ya wiki iliyopita kuvunjika kutokana na mkurugenzi huyo kuamuru watumishi wote watoke nje ya kikao.

Wakizungumzia suala hilo, baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo walisema wamesikitishwa na hatua ya mkurugenzi huyo kufunga ukumbi wa mikutano bila kutoa taarifa yoyote, kwani maandalizi yote ya kikao yalikwisha kamilika.

"Tumevunjiwa heshima kubwa tuliyopatiwa na wananchi wa Meru, thamani yetu haipo kuanzia ndani ya halmashauri na nje, sasa tunataka kujua mamlaka aliyo nayo mkurugenzi mpaka kufikia hatua ya kufunga ukumbi wa mikutano ambao umejengwa kwa kodi za wananchi wa Meru," alisema diwani mmoja.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Willy Njau, alisema kwa mujibu wa taratibu za halmashauri, walifika ili kuendelea na baraza lao kama kawaida, lakini walishangaa kuona mkurugenzi akiagiza ukumbi ufungwe na majoho yatolewe bila kupewa taarifa yoyote ya kuvunjwa kwa baraza.

Alidai kwa muda mrefu kuna msuguano mkali kati yao na mkurugenzi huyo kutokana na mapato ya halmashauri hiyo kushuka kwa kiasi kikubwa tangu ahamie hapo.

"Huu ni mpango mkakati unafanywa na mkurugenzi kwa lengo la kuhakikisha madiwani wa Chadema hawafanyi kazi ili kufikia kipindi cha uchaguzi waweze kuenguliwa," alidai Njao.

Alisema wameshaandika barua kwa mamlaka husika ya kumkataa mkurugenzi huyo, lakini sasa miezi mitatu imepita bila kupata mrejesho wowote, hivyo wamejipanga kupeleka malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo pamoja na ofisi ya Tamisemi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa halmshauri hiyo, Nelson Mafie, alisema hatua ya mkurugenzi huyo kuwafungia nje madiwani na kushindwa kufanyika kwa kikao imesababisha hasara kubwa ikiwamo vyakula na vinywaji vilivyokuwa vimeandaliwa kugawanywa kwa watumishi na wananchi waliokusanywa kutoka nje ya halmashauri hiyo ili visimwagwe.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Kazeri alipofuatwa na Nipashe ili kuzungumzia suala hilo, alisema hayupo tayari kuzungumzia na kuwataka waandishi wa habari wamwache na wakaandike wanachoweza.

"Kama ni suala la madiwani wenu sitaki kulizungumza, wafuateni madiwani mkawaulize na kama ni kuandika kaandikeni mnavyojua pelekeni hadi CNN," alisema akiwa ameambatana na katibu tawala wa wilaya hiyo.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment