Writen by
sadataley
8 years ago
-
0
Comments
Wa kwanza kushoto mkuu wa wilaya ya
Bagamoyo, Alhaj Magid Mwanga ,wa pili kushoto mkuu wa mkoa wa Pwani,
mhandisi Evarist Ndikilo na Jack Feng mkurugenzi wa kiwanda, wa tatu
kushoto ni waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji Charles Mwijage na
Ridhiwan Kikwete na Cliford Tandari wakiweka udongo kwenye jiwe la
msingi.(picha zote na Mwamvua Mwinyi)
Ramani ya kiwanda
Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Waziri wa biashara, Viwanda na
Uwekezaji, Charles Mwijage, amezitaka taasisi zinazohusika na uwekezaji
kutokuwa na ukiritimba ili hali kufikia malengo ya serikali ya kukuza
sekta ya viwanda. Aidha ameeleza kwamba, wizara hiyo, imeweka mazingira
mazuri ya uwekezaji ambayo yatawezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na
nje.
Hayo aliyasema huko kitongoji
cha Pingo Chalinze,Bagamoyo,wakati akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda
cha Vigae cha Twyford Ceramics Ltd.
Mwijage alisema, uwekezaji huo unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda .
Alisema kwa kuanzishwa viwanda vingi vya aina hiyo kutasaidia kuongeza pato la nchi na kuzalisha ajira kwa wingi.
“Zipo idara ambazo
zinafanikisha uwekezaji ikiwemo brela, idara ya uhamiaji, kazi, mamlaka
ya mapato TRA, wizara ya ardhi, shirika la viwango TBS, baraza la
Mazingira NEMC ambazo zinapaswa kufanya kazi kwa wepesi ili kufanikisha
uwekezaji,” alisema Mwijage.
Alisema kati ya idara hizo baadhi zimekuwa zikifanya vizuri lakini nyingine zimekuwa zikiwapa usumbufu mkubwa wawekezaji.
“Wizara yangu haina tatizo
lakini kuna baadhi ya idara zimekuwa kero na ukiritimba usio na sababu
.,naomba kama kuna idara zinakuwa kikwazo niambieni ili tuwachukulie
hatua,” alisema Mwijage.
Mwijage alisema nchi
zilizofanikiwa kukuza uchumi wake kupitia viwanda zimeweza kutoa ajira
nyingi kwa vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi.
Mkurugenzi mkuu wa kiwanda
hicho Jack Feng alieleza, kiwanda hicho asilimia 95 ya malighafi itakuwa
inatoka nchini ambapo kigae kinatumia maliahafi zaidi ya 10.
Alisema mara kiwanda hicho
kitakapokamilika agosti mwaka huu kitaweza kupunguza asilimia 30 ya
uagizaji wa vigae toka nje ya nchi.
Feng alisema wanatarajia
kuajiri wafanyakazi 2,000 moja kwa moja na 4,000 kazi za muda na gharama
ya mradi huo ni dola mil. 56 sawa na bil. 120 .
Alisema watauuza hadi nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi .
Nae mkurugenzi mtendaji wa
kituo cha uwekezaji Cliford Tandari alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda
hicho ni wa mfano kwani utavutia makampuni mengi.
Alisema kwasasa kituo hicho
kimeweza kutoa wigo mkubwa katika kuandikisha miradi mbalimbali toka
china na kufikia miradi 667 ambayo itazalisha ajira 83,141 kwa
watanzania ,miradi 452 ni miradi inayohusiana na sekta ya uzalishaji
viwandani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema ,mkoa huo una viwanda 264 huku vikubwa vikiwa ni viwili.
Ndikilo alisema uwekezaji huo ni mkubwa na unatarajia kukuza ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Alisema mkoa wa Pwani bado una
maeneo makubwa ya uwekezaji na tayari kuna eneo lenye ukubwa wa hekari
5,000 linahitaji wawekezaji .
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete aliwapongeza wawekezaji hao kutoka nchi ya China .
Alisema Chalinze imejipanga kuwa sehemu ya uwekezaji ambapo kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto kubwa inayokabiliwa wananchi na wawekezaji ni ukosefu wa maji,.
Alibainisha wamekuwa
wakijitahidi kuikabili lakini bado hawajafanikiwa kuidhibiti aliomba
wawekezaji hao kutoa ajira bila ya kuwabagua wenyeji.
No comments
Post a Comment