salmin-awadh
Marehemu  Mh. Salmin Awadh enzi za uhai wake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amempelekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin, Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni katika Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza hilo.
Mheshimiwa Salmin ambaye alikuwa pia Katibu wa Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi, amefariki dunia ghafla mchana wa leo, Alhamisi, Februari 19, 2015, wakati akihudhuria kikao cha CCM kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Kisiwandui, mjini Zanzibar.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Rais Shein, “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin, Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni katika Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza hilo ambaye nimejulishwa ameanguka ghafla wakati akihudhuria kikao mjini Zanzibar.”
“Nimemjua Mheshimiwa Salmin kwa muda mrefu na hakuna shaka kuwa katika miaka 10 iliyopita tokea mwaka 2005 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia Baraza la Wawakilishi ameliwakilisha vizuri Jimbo lake la Magomeni na watu wake, na ameonyesha uongozi katika Baraza la Wawakilishi na kutoa mchango mkubwa katika Chama chetu cha CCM. Tutaendelea kukosa mchango wake na busara zake za uongozi”, amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki kikubwa. Aidha kupitia kwako, nawatumia salamu za rambirambi wananchi wa Magomeni ambao wamepoteza Mwakilishi wao na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliopoteza mwenzao na kiongozi wao.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kupitia kwako,vile vile, natuma pole nyingi sana kwa familia, ndugu na jamaa wa Mheshimiwa Salmin kwa kuondokewa na mhimili mkuu wa familia na mlezi. Wajulishe niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Napenda pia uwajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke pema roho ya marehemu. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
19 Februari,2015

Mwili wa marehemu Salmin Awadhi ukipakiwa gari tayari kwa taratibu za mazishi hapo kesho, katika makaburi ya makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja,  mwili wa marehemu unategemewa kuagwa kesho saa tano katika ukumbi wa baraza la wawakilishi Chukwani Unguja na kusaliwa katika Masjid Muhammad kwa mchina na kuzikwa Kijiji kwao Makunduchi Unguja  






Mbunge wa Jimbo la Magomeni Hassan Chombo akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kifo chake walionana muda mfupi kabla ya kumkuta mauti, amekuwa na majonzi na kustuka na msiba huo. ni pigo kwake.  wakiwa nyumbani kwa ndugu wa marehemu mpendae kunakofanyika maziko hayo hapo kesho saa saba baada ya sala ya Ijumaa masjid Muhammad kwa mchina na kuzikwa makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.