Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Friday, October 24, 2014

Dakta Robert Ouko: Shujaa vita vya ufisadi aliyeuawa kikatili II

 
 
Dk. Robert Ouko
Nasaha za
 
HATUA ya nchi za Magharibi kusitisha misaada kwa Serikali ya Rais Daniel Arap Moi wa Kenya kwa sababu ya kumwandama Dk. Robert Ouko, kupora demokrasia na kukithiri kwa ufisadi nchini, kuliiweka pabaya Serikali ya Kenya.
Vivyo hivyo, hatua ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Magareth Thatcher, na ya Rais wa Marekani, George Bush, kumwamuru Moi amrejeshee Ouko nafasi yake ya Uwaziri wa Mambo ya Nje na kumteua pia kuwa Makamu wa Rais na kudumisha demokrasia nchini Kenya kabla ya kufikiriwa tena kurejeshewa misaada; ilimfanya Moi amwone Ouko kama mtu hatari, mwenye sapoti ya mataifa makubwa.
Masharti mengine aliyopewa ni pamoja na kuteua Mchumi mahiri kuwa Waziri wa Fedha, badala ya Profesa George Saitoti ambaye, licha ya kutomudu Wizara hiyo, alionekana pia kuwa “mratibu” wa ufisadi nchini kupitia Wizara yake. Aliagizwa pia kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa; na  mwisho, kuzingatia utawala wa Sheria na Haki za Binadamu.
Machoni mwa Moi, kisababishi kikuu cha yote hayo alikuwa Ouko. Kwa hiyo,  akaamua kuondokana na “hatari” mbele yake haraka, kwa kumtendea ambalo halikutarajiwa.
Moi amtelekeza Ouko Washington
Kusifiwa kwa Ouko na vyombo vya habari vya Marekani kwamba alistahili kuwa Rais wa Kenya kuliko Moi, kulimtia kichaa Rais huyo.  Huku akiwa amejawa chuki na hasira ya kimaangamizi, hofu na tishio kwa nafasi yake; siku hiyo aliapa kutopanda ndege moja na Ouko maishani; akamwacha Washington akiwa mpweke, mwenye mawazo mengi na msononeko mkubwa, na asiyejua nini kingemkuta baada ya hapo kuhusu wadhifa na hata maisha yake.
Huku akiwa bado haamini kilichotokea, Ouko alipanda ndege tofauti kurejea Kenya peke yake siku hiyo hiyo aliyoondoka Moi kuelekea Nairobi, Februari 2, 1990; na kuwasili siku mbili baadaye Februari 4, 1990, dakika chache tu baada ya Rais Moi kuwasili uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.
Wakati Moi angali akitumbuizwa kwa ngoma za jadi uwanjani hapo, Ouko aliona vyema aungane na msafara wa Rais wake; lakini alipigwa na butwaa kwa mara nyingine, pale Moi alipomwona na kumng’akia akisema: “Bado unanifuatafuata hata huku; una jambo gani nami wewe msaliti mkubwa?”.
Akiwa angali pale uwanjani, Pasi yake ya kusafiria ilichukuliwa na watu wa “Usalama” kwa madai ya kutaka “kufanyiwa marekebisho madogo”;  Ouko akaona giza mbele.
Siku iliyofuata, Februari 5, 1990; Ouko alikwenda Ikulu ya Nairobi kuonana na Rais kujaribu kumwomba msamaha kwa kosa asilolijua wala kutenda.  Moi, badala ya kumsikiliza,  alimwamuru aende kwao Mkoa wa Nyanza na asionekane Nairobi hadi atakapoitwa na yeye mwenyewe.
Kwa utaratibu wa kawaida, mtumishi wa umma anaposimamishwa kazi au kupewa likizo ya dharura na hata kuachishwa kazi kwa sababu maalum; hujulishwa hatua hiyo na mamlaka husika kwa njia ya barua na kutakiwa kukabidhi ofisi na vitendea kazi ili kutokwamisha mwendelezo wa shughuli za ofisi hiyo.  Lakini haikuwa hivyo kwa Ouko; kauli ya Moi ya mdomo ilitosha, kana kwamba taasisi ya Urais ilikuwa ya Moi na familia yake.
Huku akionekana kuchanganyikiwa dhahiri, Ouko alikwenda ofisini kwake baada ya kushauriana na mawakili wake juu ya yaliyokuwa yakimsibu; akachukua majadala yake ya siri na kuagana na watumishi wa ofisi yake, mmoja mmoja kwa kumshika mkono kwa maneno: “Kwa heri ya kuonana”, kisha akaondoka kwa kuwapungia mkono, lakini mwenye mawazo mengi na huzuni iliyojiandika dhahiri kwenye paji la uso wake.
Alipofika nyumbani, alishangaa kukuta mlinzi wake na dreva aliyepewa na Serikali wameagizwa kuondoka, hawapo. Akajihoji kimoyomoyo juu ya maana na ishara ya yote hayo; lakini akapiga moyo konde.
Kikosi cha mauaji chaundwa
Februari 6, 1990, kikao maalum cha kushughulikia “suala la Ouko” kiliitishwa mjini Kericho kwa amri ya Moi, chini ya Uenyekiti wa Nicholaus Kiprono Biwott na viongozi wengine wa Serikali, akiwamo Profesa George Saitoti, ambapo Noah Too aliteuliwa kuwa Mratibu wa “Mradi” huo wa kumwangamiza Ouko.
Siku mbili baadaye, Februari 8, 1990; Moi alitaarifiwa na kutoa baraka kwa yale yaliyoazimiwa kwenye kikao cha Kericho; yakiwa ni pamoja na kuundwa kwa Operesheni maalum iliyopewa jina “OPERESHENI BIKINI RITHISHA” [Operation BIKINI Succession], na kufuatiwa na kikao kingine cha kuweka mikakati, Februari 11, 1990.  BIKINI ni ufupisho wa muungano wa majina ya “Biwott [BI], Kiprono [KI] na Nicholaus [NI] – BIKINI.
Kwa kuangalia kwa juujuu, “mgongano” kati ya Moi na Ouko ulionekana kama matokeo ya Ouko kushambulia dola, kwa maana ya utawala wa nchi kwa maovu yake ya kijamii tuliyokwishayaona mwanzo, akiwamo Rais mwenyewe.
Lakini neno “Operesheni Rithisha”, na zaidi, neno “Rithisha”,  lilionekana zaidi ya hilo, kwamba Ouko alikuwa kikwazo kikubwa kwa Moi katika kuteua mrithi aliyemtaka. Kwa sababu hii, vita hiyo ilikuwa na ndimi mbili za moto wa damu – “Petals of blood”, kama ambavyo mwana riwaya mahiri wa Kenya, Ngungi wa Thiong’o, angependa kuita.
Kwa kuona mambo yakizidi kumwendea vibaya, Ouko aliamua kumwona hasimu wake, kipenzi na mshirika wa Moi, Hezekiah Oyugi; kumuomba amshauri Moi amsamehe “makosa” yake; lakini Oyugi alimjibu kwa jeuri, akisema: “Kama umegongana na Nyayo [kauli mbiu ya kisiasa ya Moi], shauri yako”.  Ouko akainamisha kichwa kwa huzuni, kisha akaondoka, kimya kimya.
Moyoni, Ouko aliwaza na kujihoji kwa kina:  “Hivi niombe msamaha au kutubu kwa kosa gani?.  Kwa nini nijikabidhi kwa binadamu mwovu kinyume cha dhamiri [conscience] yangu iliyo sahihi?”.
Dhamiri yake ikamsuta na kumtesa kwa sababu hakuwa na cha kutubu.  Akajifananisha na watumwa wa Babylon katika Zaburi, waliolazimishwa kutubu dhambi wasizozijua dhidi ya Mungu katili na la kuogofya, la ugenini. Akajihoji tena akisema: “itamsaidia nini mtu mwadilifu kwa sala ya kinafiki kwa kusema: Dhambi nilizotenda, sizijui; Kosa nililotenda, silijui; Uchafu niliopita, siujui; Nisafishe niwe safi, Mungu, dhambi nisizozijua; hata kama dhambi zangu ni sabini mara saba”.
Akaona upuuzi, akaamua heri kujiweka mikononi mwa Mungu wa kweli, Mungu wa Taifa la Kenya; badala ya kuabudu kwa kuinamia Mungu-mtu, dikteta mmwagaji damu.
Ouko hakuwa mpenzi sana wa kwenda kanisani mara kwa mara; lakini Jumapili ya Februari 11, 1990, tofauti na Jumapili zingine kabla ya hapo; alishangaza familia yake kumwona akihudhuria Misa katika Kanisa lake la “African Inland Church” [AIC], Koru, akasali; kisha akataka aombewe sala maalum aliyochagua, baada ya yeye mwenyewe kusoma na kutafakari somo la siku hiyo altareni.
Wiki hiyo pia alijaribu kuomba msaada wa Mwai Kibaki amwombe Moi atafakari upendo wa Mungu na alegeze moyo wake, lakini bila mafanikio. Moi alikuwa ameamua kutorudi nyuma, pengine kwa hofu ya kugeuka “Jiwe”.
Na katika hali ya kuchanganyikiwa zaidi, Ouko alimwendea tena hasimu wake, Hezekiah Oyugi; safari hii akitaka ampatie gari la serikali ili aweze kutoroka nchini; naye Oyugi akakubali kufanya hivyo, lakini huku akiendelea kufuatilia nyendo za Ouko kwa maelekezo ya “Operesheni BIKINI”.  Februari 12, 1990, simu za nyumbani kwa Ouko zilikatwa ili kumnyima mawasiliano na watu wengine.
Siku ya kiama yawadia
Hatimaye siku ya kiama kwa Ouko iliwadia, wakati huo angali akijipa matumaini ya kukimbilia uhamishoni.
Alfajiri ya Jumanne, Februari 13, 1990, yapata saa tisa au 10 hivi; gari jeupe aina ya Mercedes Benz kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Nyanza, lilijongea taratibu lango kuu nyumbani kwa Ouko huko Koru. Waliokuwemo kwenye gari hilo walijitambulisha kama watu waliotumwa na Rais kumwendea Ouko chini ya “wito maalum”.  Baada ya muda mfupi, wakawasili wengine 15 wakiwa katika gari la Serikali pia; Walinzi binafsi wa Ouko wakafukuzwa na kuonywa wasiongee kitu hapo na kwingineko.
Ouko alielewa hima yaliyomkuta na hatima yake; akawaomba “wageni” [watekaji] wake hao wamruhusu arudi ndani kubadili nguo; nao wakakubali.  Alipoingia ndani, Ouko aliandika kwenye karatasi majina ya baadhi ya waliokwenda kumchukua usiku huo kuwa ni Oyugi, Biwott, Koba, Koskei na Noah Too; kisha akaipachika nyuma ya fremu ya picha yake ukutani na kutoka nje kukutana na wauaji wake.
Ouko aliripotiwa kupatikana ameuawa kwa bastola siku moja baadaye huko Nakuru katika mazingira yaliyoonesha kuteswa kabla ya kuuawa, na mwili wake kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Nakuru, huku sehemu zake za siri zikiwa zimeondolewa.
Siku moja baadaye, pengine baada ya wauaji hao kuhofia kufuatiliwa; walipata wazo la pili la kuuchukua mwili huo kutoka chumba cha kuhifadhia maiti, wakaupulizia dawa kali ya kubabua ngozi ili usitambulike, kabla ya kuupakia kwenye Helikopta ya Jeshi la Polisi na kuutupa eneo karibu na nyumbani kwake.
Kisha, Hezekiah Oyugi na Noah Too waliuchukua mwili huo kutoka mahali ulipotupwa na Helikopta na kuupeleka vichakani; wakawasha moto eneo hilo na kuunguza nyasi kwa matarajio kwamba ungeteketea kwa moto ili kupoteza ushahidi.
Wapelelezi kutoka Scotland
Serikali ya Rais Moi ilijitahidi kuficha ukweli, sababu na mazingira ya kuuawa kwa Ouko; lakini kutokana na shinikizo la wananchi kwa njia ya hoja na maandamano nchi nzima, huku wakiinyoshea kidole Serikali; hatimaye Moi alilazimika kuita wapelelezi kutoka Uingereza, maarufu kama Polisi wa “Scotland Yard” kufanya uchunguzi wa kifo hicho.
Hata hivyo, wachunguzi hao walikatisha zoezi hilo ghafla kwa kuhofia maisha yao, baada ya kukumbana na vitisho vya Serikali dhidi yao, hasa kufuatia taarifa ya awali ya uchunguzi wao, ambayo hata hivyo ilifichwa na Serikali na kubakia kama siri kubwa inayolindwa.
Alipoingia madarakani, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Mwai Kibaki; kwa kuelewa jinsi umma wa Kenya ulivyochoshwa na rushwa, demokrasia duni na ufisadi, aliahidi kuwashughulikia wote waliochafuka kwa maovu hayo, pamoja na kufufua uchunguzi wa kifo cha Ouko ili wote waliohusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Kibaki, kwa kiasi fulani kwa kuanzia, alitekeleza hili la wala rushwa na mafisadi, pale alipowastaafisha majaji kadhaa kuhusiana na kashfa ya wizi wa mabilioni ya fedha, maarufu kama “Kashfa ya Goldenberg” na Moi akihusishwa pia.
Lakini pamoja na hatua pekee hiyo ya kujikosha, Moi hakuguswa kutokana na kinga ya Kikatiba kwa Kiongozi kama yeye kutoshitakiwa hata anapokuwa nje ya Utawala; huku Oyugi, Biwott, Koba, Koskei, Too na Saitoti wakiendelea kuvuta hewa huru ya Kenya, sawa tu na Wakenya wema walioporwa jasho lao na “nyang’au” hao.
Lini, tunauliza; Katiba zetu sisi Waafrika, zitawawajibisha Wakuu wa Nchi kwa maovu wawapo na watokapo madarakani ili wakome kukimbilia Ikulu, wakifikiri kwamba kutawala ni kujifanyia wapendavyo kwa kulindwa na Katiba?.
Tuna kila sababu kuamini maneno ya Shaaban Robert, katika Shairi lake “Kweli itashinda”, kwamba siku hiyo inakuja, anaposema: “Kweli itashinda namna tunavyoishi;/kweli haihofu tisho wala nguvu ya majeshi;/La uongo lina mwisho, Kweli kitu cha aushi;/Kweli itashinda kesho, kama leo haitoshi”.
- See more at: http://www.raiamwema.co.tz/dakta-robert-ouko-shujaa-vita-vya-ufisadi-aliyeuawa-kikatili-ii#sthash.OUXqFiSz.dpuf
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment