Writen by
sadataley
5:16 PM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati Baraza Kuu la Chadema likimthibitisha kwa mara ya pili, Dk Willibrod Slaa kuwa Katibu Mkuu wake, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amekabidhiwa rasmi mikoba iliyoachwa na Zitto Kabwe katika nafasi ya naibu katibu mkuu wa chama hicho Bara.
Pia, baraza hilo lililoketi juzi usiku, limemthibitisha aliyewahi kuwa mtangazaji wa Channel Ten na sasa ofisa wa Vodacom, Salum Mwalimu, kuwa naibu katibu mkuu Zanzibar, baada ya majina ya vigogo hao kupendekezwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Kabla ya chama hicho kuingia katika uchaguzi mkuu, nafasi ya naibu katibu mkuu Bara ilikuwa wazi baada ya Zitto aliyekuwa anaishikilia kuvuliwa wadhifa huo Novemba mwaka jana kwa madai ya kukiuka kanuni, katiba na taratibu za chama hicho.
Baada ya Mbowe kupendekeza majina hayo, Baraza Kuu liliwathibitisha kwa kura na Dk Slaa alipata 173 kama ilivyokuwa kwa Mnyika na Mwalimu kura 124. Viongozi hao ambao wote wanaingia moja kwa moja Kamati Kuu na sekretarieti ya chama hicho, hakuna aliyepigiwa kura ya hapana.
Awali, Mwalimu alichaguliwa mjumbe wa Kamati Kuu kwa upande wa Zanzibar, nafasi ambayo iliamuliwa iachwe wazi hadi itakapopata mjumbe mwingine.
Wajumbe Kamati Kuu
Wajumbe waliochaguliwa kuingia Kamati Kuu na kura zao kwenye mabano ni Profesa Mwesiga Baregu (127), Dk Yaredi Fubusa (127) na Mabere Marando (164), Catherine Vermand (97), Susan Kiwanga (93), Zainab Musa Bakari (111) na Elly Marco Macha (154).Uchaguzi huo wa wajumbe wanane wa Kamati Kuu kati ya 17 walioomba, umekamilisha safu ya uongozi wa chama hicho (mbali ya wajumbe wasiozidi sita wa kuteuliwa na mwenyekiti), baada ya Mkutano Mkuu kuwachagua Mbowe kuwa mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari makamu mwenyekiti Bara na Said Issa Mohammed kuwa makamu mwenyekiti Zanzibar
No comments
Post a Comment