Writen by
sadataley
5:02 PM
-
0
Comments
Na Daniel Mjema, MwananchiDodoma. Kauli ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta kwamba fedha ambazo zitakuwa zimeokolewa katika siku 60 za uendeshaji wa Bunge hilo hazitarejeshwa serikalini, bali zitatafutiwa utaratibu wa namna ya kuzitumia, imemgonganisha na katibu wake, Yahya Khamis Hamad ambaye amesema “hilo ni jambo la ajabu”.
Sitta alitoa kauli hiyo juzi usiku wakati akiahirisha Bunge hilo lenye wajumbe 500 baada ya wajumbe 130 wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kulisusia tangu Aprili 16, mwaka huu.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh300,000 kwa siku sawa na Sh150 milioni kwa siku kwa wajumbe wote, huku Serikali ikiwa imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya siku 60 za uendeshaji wa Bunge hilo.
Kauli hiyo ya Sitta kuwa fedha zitakazookolewa zitatafutiwa utaratibu badala ya kurudishwa zilikotoka, iliwafanya wajumbe wa Bunge hilo kulipuka kwa furaha na kugonga meza.
Hata hivyo, katibu wa Bunge, Yahya Khamis Hamad alishangazwa na kauli hiyo ya Sitta akisema: “Mimi hayo niliyasikia lakini kwangu pia ni ya ajabu kwa sababu fedha tulizonazo hazitoshi, sasa hizo za kubaki mimi sijui.”
Katibu huyo alisema kwa sasa, Wizara ya Fedha inawapa kiasi cha fedha kwa kile tu ambacho kinahitajika na yeye anatoa taarifa serikalini kwa kiasi kilichotumika. “Mimi sijui labda yeye anajua sitaki kumsemea,” alisema.
Sitta pia aliwaeleza wajumbe hao kuwa baada ya kukabidhi Katiba inayopendekezwa, wote watakabidhiwa cheti na Rais Jakaya Kikwete.
“Cheti hicho kitakuwa na sahihi ya Rais mwenyewe kwa hiyo tutakaa kidogo kusubirisubiri Katiba iliyokamilika, haiwezi kuwa ya ovyo ovyo tu lazima iwe na viwango vizuri,” alisema Sitta na kuongeza:
“Tutachapisha nakala nyingi kila mmoja aende na waraka huo wa kihistoria nyumbani na itakuwa ni Katiba bora sana hapa Afrika na Kusini mwa Sahara.”
Mwenyekiti huyo aliwapiga vijembe viongozi wa Ukawa na makundi mengine yanayopaza sauti kutaka Bunge hilo lisitishwe ili kuokoa pesa
“Tutamaliza zoezi hilo Oktoba 3, mwaka huu ili tutoke na Katiba inayopendekezwa kinyume na wale wanaopiga kelele ovyo bila kuwa na sayansi kichwani eti unaokoa gharama kwa kusitisha mchakato.
“Mchakato huu ungesitishwa ina maana utawala ujao, rais ajaye ingembidi kuanza upya na Tume na aingie tena kwenye Bunge Maalumu la Katiba,” alisema Sitta.
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Fedha-zamgonganisha-Sitta-na-katibu-wake/-/1597296/2455182/-/aykjwyz/-/index.html
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Fedha-zamgonganisha-Sitta-na-katibu-wake/-/1597296/2455182/-/aykjwyz/-/index.html
No comments
Post a Comment