Writen by
sadataley
2:56 PM
-
0
Comments
“Alichokizu ngumza Mwigulu ni mtazamo wake binafsi, ndiyo maana katika
mchakato wa kuandika Katiba Mpya ilielezwa wazi kwamba watu wavumiliane
katika utoaji wa maoni na mitazamo yao,” alisema Nape.
Na Fidelis Butahe, MwananchiDar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kimejiweka kando na kauli ya naibu katibu mkuu wake, Mwigulu Nchemba
aliyoitoa kwamba Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima
wa kuendelea kutokana na uwezekano mdogo wa wajumbe wake kufanya uamuzi.
Mbali na hilo, chama hicho kimemtaka mwenyekiti wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe
wake kutogeuza rasimu mradi binafsi.
Juzi, akiwa bungeni Nchemba ambaye ni mbunge wa
Iramba Magharibi na naibu waziri wa fedha, alisema kitendo cha Bunge
hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa
pande zote mbili inayohitajika kupitisha rasimu, hakiwezi kueleweka kwa
Watanzania.
Alisema kwa namna moja, ni vyema kujua idadi
halisi ya wale wanaoshiriki katika awamu ya pili ya Bunge hilo na wale
wasioshiriki, ili kutoa uthibitisho wa kihesabu kwamba uamuzi wa
kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema msimamo wa
chama hicho ni Bunge la Katiba kuendelea kuichambua Rasimu ya Katiba na
si vinginevyo.
“Alichokizungumza Mwigulu ni mtazamo wake binafsi,
ndiyo maana katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya ilielezwa wazi
kwamba watu wavumiliane katika utoaji wa maoni na mitazamo yao,” alisema
Nape.
Nape alisema Mwigulu akiwa ndani ya Bunge hilo
anazungumza akiwa mjumbe wa Bunge la Katiba na si kama kiongozi wa chama
kwa maelezo kuwa Katiba si ya chama cha siasa, bali ya Watanzania wote.
Kuhusu upigaji wa kura kwa ajili ya kufanya
uamuzi, Nape alisema kuwa hata kama wajumbe wa Ukawa watarejea bungeni,
hakuna anayejua kuwa watapiga kura ya aina gani.
“Hata Ukawa wakirejea bungeni huwezi kujua
watapiga kura ya aina gani, inawezekana wakawepo na hiyo theluthi mbili
pia isipatikane.
Kwa idadi ya wajumbe waliofika bungeni hadi sasa akidi si tatizo tena maana hata hao Ukawa baadhi yao wameanza kurejea bungeni.”
Nape alisema Katiba si ya CCM wala Ukawa na kwamba
wapo Watanzania wengi ambao wanakubaliana na uamuzi wa kuendelea kwa
hatua nyingine za kupata Katiba Mpya.
“Katiba ni mali ya Watanzania na waliopo bungeni
ni zaidi ya vyama vya siasa. Kama kundi kubwa limeridhia na jingine
ambalo hata kiganjani halijai limesusa, sisi tutaendelea tu,” alisema.
Amshukia Jaji Warioba
Katika mkutano huo uliokuwa mahsusi kwa ajili ya
kumjibu Jaji Warioba kwa kile alichokizungumza pamoja na wajumbe wa
iliyokuwa Tume yake katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere Jumatatu wiki hii, Nape aliwataka viongozi hao kutogeuza rasimu
kuwa mali yao binafsi.
“Wametumia lugha za kejeli, matusi dhidi ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika mdahalo huo.
Walichozungumza hakivumiliki na tutawajibu wao na wote watakaotoa lugha
kama zao,” alisema Nape.
Alisema Jaji Warioba na wenzake waache kuwalazimisha Watanzania wakubaliane na maelezo yao hata kama yanaipeleka nchi pabaya.
Alisema Rais Kikwete wakati anafungua Bunge la Katiba alitoa maoni kama wananchi wengine na si kiongozi wa kwanza kufanya hivyo:
“CCM kina haki na wajibu kama vyama vingine kutoa maoni, iweje leo kionekane kuwa kinatenda dhambi?”
Alisema kuwa Tume ilikuwa huru wakati wa kukusanya
maoni ya wananchi, sasa inatakiwa kutoingilia mchakato huo kwa sababu
ilishavunjwa.
No comments
Post a Comment