Writen by
sadataley
6:00 PM
-
0
Comments
Na Lauden Mwambona, MwananchiMbeya. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi amefichua sababu za chama hicho kushikilia msimamo wa muundo wa serikali mbili katika mjadala wa Katiba Mpya, akisema ni “maagizo ya mwenyekiti wa CCM”.
Mjadala wa Katiba Mpya ulikumbwa na mtikisiko
baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kitu alichokiita maoni yake binafsi
wakati akizindua Bunge la Katiba kwa kueleza kuwa angependa muundo wa
Muungano wa serikali mbili tofauti na Rasimu ya Katiba iliyopendekeza
serikali tatu.
Mjadala huo ulivurugika kabisa baada ya kundi la
wajumbe kutoka vyama vya upinzani waliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kususia vikao likidai mjadala umepoteza mwelekeo kwa kuweka
kando maoni ya wananchi ya kutaka muundo wa serikali tatu.
Akifungua mkutano wa Baraza la Utendaji la Umoja
wa Vijana wa CCM wa Mkoa wa Mbeya juzi jioni, Zambi alisema mwenyekiti
wa CCM alishawaambia kwamba msimamo wa chama ni kuhakikisha zinabaki
serikali mbili kwenye Katiba Mpya.
‘’Vijana sasa lazima niwaeleze ukweli kuhusu
muundo wa serikali, ni kwamba piga ua, CCM inataka kuimarisha muundo wa
serikali mbili na hili ni agizo la mwenyekiti wetu Rais Jakaya Kikwete,”
alisema huku akishangiliwa.
Alisema suala la Muungano ni maelewano na kwamba
baadhi ya shughuli muhimu za Zanzibar zimehamishiwa Bara wakati nyingine
za Bara zimehamishiwa Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kero iliyopo kwa sasa kwenye
Muungano huo ni namna ya kugawana mapato makubwa ambayo alisema Serikali
inaendelea kuyafanyia kazi.
“Rais Kikwete katika kutueleza msimamo wa chama,
pia alifafanua vizuri suala la serikali tatu kuongeza gharama za
uendeshaji, jambo ambalo hata mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Jaji Joseph Warioba aliliona, ingawa alifafanua kwamba halina
namna,” alisema.
Zambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, alisema anamshangaa Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe anapotamka kwamba serikali tatu ni lazima.
“Vijana wote na wanaCCM mkoani Mbeya naomba
muelewe kwamba sisi chini ya mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Kikwete,
tumeamua muundo wa serikali mbili tu,” alisema.
Alisisitiza kwamba kama wachache hawataafiki msimamo huo kwa busara, Serikali ya CCM itaendelea na katiba iliyopo.
Akieleza sababu za msimamo wake wa serikali mbili
wakati akizindua Bunge la Katiba, Rais Kikwete alizungumzia gharama za
uendeshaji wa serikali tatu akisema katika muundo wa serikali tatu,
Serikali ya Muungano haitakuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha na kwamba
hilo linaweza kusababisha kushindwa kulipa mishahara kama ya wanajeshi
na hivyo kusababisha chombo hicho cha dola kuchukua serikali.
Awali kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba, kulikuwa na habari
kwamba CCM imesambaza waraka wa kutaka wabunge wake wapigie debe muundo
wa serikali mbili na baadaye Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye alisema chama hicho kina masilahi na muundo huo.
Ukawa imegoma kurudi kwenye Bunge la Katiba ikidai
kuwa itafanya hivyo tu ikiwa kutakuwepo makubaliano ya kuheshimu maoni
ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
siyo kuingiza maoni mapya.
Kauli ya Zambi imekuja wakati mmoja wa wajumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akisema anamshangaa Rais Kikwete kwa
kuiponda rasimu wakati alikuwa anapewa taarifa katika kila hatua
waliyokuwa wakifikia. Hivi karibuni, mmoja wa wajumbe hao, Dk Salim
Ahmed Salim alinukuliwa na gazeti hili akisema kuwa Tume ya Katiba
ilikuwa ikimpatia Rais taarifa za kila hatua zilizokuwa zikifanyika.
Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaa
akihojiwa na gazeti hili mwishoni mwa wiki alisisitiza kwamba mwenye
rungu la kutengua utata wa Katiba Mpya ni Rais Jakaya Kikwete.
Awali, Katika hotuba yake, Zambi pia alizungumzia
hali ya kisiasa mkoani Mbeya akisema CCM imeanza kupata nguvu baada ya
wananchi kuelewa ukweli kwamba maisha bora hayatakuja kwa watu
‘wanaocheza pool, wanaoshinda baa wala wavivu’.
Pia aliwataka vijana mkoani hapa kuacha
kushabikia mabadiliko ya vyama vya siasa akisisitiza kuzichunguza nchi
za Malawi, Zambia na Kenya kujua wananchi wamefaidikaje kimaisha baada
ya kubadilisha vyama vya siasa mara kadhaa.
“Nasisitiza, hakuna Serikali itakayowanunulia nguo
watu wake, itakayowalisha watu wote bure au kuwapatia viatu watu
wasiofanya kazi yoyote. Kazi ya Serikali ni kuboresha huduma za jamii,”
alisema.
Kuhusu hali ya chakula nchini, alisema wakulima
watavuna karibu tani milioni 15 wakati mahitaji ya Watanzania ni tani
milioni 12 za nafaka. Mwaka jana zilivunwa tani 14 milioni.
No comments
Post a Comment