Writen by
sadataley
6:16 PM
-
0
Comments
Na Majuto Omary, Mwananchi
Dar es Salaam. Uongozi wa klabu ya Yanga umetoa
ruksa kwa klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini kufanya mazungumzo
kama wanataka kumsajili mchezaji wao nyota, Mrisho Ngasa.
Awali klabu hiyo ilishangazwa na hatua ya klabu
hiyo kubwa inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini kumchukua mchezaji wao
kinyemela na kumfanyisha majaribio kinyume na taratibu na kanuni za
mpira wa miguu duniani.
Ngassa alikwenda kufanya majaribio na timu hiyo ya
Afrika Kusini takribani wiki mbili zilizopita, na uongozi wa timu hiyo
ulikuwa tayari kutoa Sh132 milioni ili kumsajili mchezaji huyo.
Hata hivyo, mpango huo uligonga mwamba kutokana na
ukweli kuwa viongozi wa Free State Stars walifanya mpango huo na Ngassa
kinyemela.
Hatua hiyo iliufanya uongozi wa Yanga kulishutumu
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuhusika moja ka moja na mpango
huo kwani haukuridhishwa na jinsi Ngassa alivyoondoka nchini kwenda
Afrika Kusini wakati alikuwa kwenye Kambi ya Taifa Stars.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema kuwa
wametoa fursa kwa uongozi wa timu hiyo ya Afrika Kusini kuja nchini na
kufanya mazungumzo mezani ili kufanikisha suala hilo.
Njovu alisema kuwa Yanga haina haja ya kumzuia Ngassa kwenda kucheza soka lake Afrika Kusini kwani hiyo ndiyo kazi yake.
“Tutakuwa hatufanyi haki kumzuia Ngassa, lakini
cha ajabu ni kwamba mpaka sasa sijamwona Ngassa kuja kuzungumzia suala
hilo, nimemwona kwa mbali sana na wala hakuja kuonana na mimi, pamoja na
hayo yote, sisi tupo tayari kuzungumza na timu hiyo aliyokwenda kufanya
mazoezi,” alisema Njovu.
Alisema kuwa hata fedha ambazo klabu hiyo imeahidi
kuzitoa kwa Yanga, wao wanazisoma kupitia mitandao tu kwani hakuna
mawasiliano yoyote. “Nasisitiza waje kuonana na sisi ili kufanikisha
suala hilo, hatuna kinyongo kuhusiana na mpango wake mpya, wasituogope
kwani klabu yetu ipo eneo la wazi na kila mtu anaijua, ila ‘njia za
panya’ hatutaki katika masuala haya makubwa yanayohusu usajili na ustawi
wa wachezaji wetu,” alisema Njovu.
Ngassa alionyesha kuridhishwa na mwenendo wa suala hilo baada ya hatua hiyo ya uongozi wake.
“Sina la kuongezea, si unajua kuwa soka ni kazi
yangu na masilahi ndiyo kila mtu anataka, Free State Stars wamenikubali
na wapo tayari kutoa fedha kwa Yanga ili wanisajili, kinachotakiwa ni
makubaliano tu kati ya Yanga na Free State Stars, sasa sijui awali
ilishindikana nini,” alisema Ngassa.
No comments
Post a Comment