Writen by
sadataley
11:53 AM
-
0
Comments
Na Imani Makongoro, MwananchiDar es Salaam. Muogeleaji wa Tanzania, Ammaar Ghadiyali amefanikiwa kuingia hatua 16 bora ya Michezo ya Jumuiya ya Madola baada ya kuongoza kwenye mbizi za mita 50 hapo jana.
Ghadiyali amekuwa Mtanzania wa kwanza kwenye michezo hiyo kuongoza katika mchujo wa mchezo wa aina ya butterfly akitumia sekunde 28:11 kwenye bwawa la kuogelea la kituo cha Tollcross nchini Scotland na kumaliza katika nafasi ya kwanza.
Meneja wa Tanzania kwenye michezo hiyo, Muharami Mchume aliiambia Mwananchi
jana kwa simu akiwa Glasgow kuwa, matokeo ya waogeleaji hao yameongeza
morali kwa wachezaji wengine na wanaamini kuwa wanaweza kufanya vizuri
na kurejea na medali.
“Wote wanasema wana deni kama Rais Kikwete (Jakaya) alivyowaambia kila mmoja ana ari ya ushindani.
Japo wenzetu wawili wa judo tayari wameondolewa,
hiyo haijawaathiri wengine katika kambi yetu hasa baada ya waogeleaji
kuanza vizuri,” alisema Mchume.
Mbali na Ghadiyali, muogeleaji mwingine wa
Tanzanian, Hila Hemed alishika nafasi nne katika mchujo huo wa kuogelea
kwa mtindo wa butterfly.
Kwa mujibu wa Mchume, Ghadiyali tayari ameingia
hatua ya 16 bora na Mariam alimaliza wa pili akitumia muda wa sekunde
37.11 na sasa anasubiri matokeo ya mchujo ya makundi mengine ili kuweza
kuingia hatua hiyo kwenye staili hiyo.
Tayari wana judo, Abubakari Nzige na Ahmed Magogo wameaga kwenye mashindano hayo.
Nzige alipoteza pambano lake dhidi ya Mohamed
Fakri wa Malaysia kwenye uzani wa kg 66 wakati Magogo akiwa ameshindwa
kucheza pambano lake na kumpa ushindi Daniele Grance wa Afrika Kusini
ambaye atacheza hatua ya 16 bora dhidi ya Mghana, Razak Abugiri.
Mchume alisema bado judo ina nafasi ya kufanya
vizuri kwa wachezaji waliosalia wa Mbaruku Seleiman atakayecheza leo
katika hatua ya 16 bora dhidi ya mshindi Dodge na Leat.
“Mbali na judo na kuogelea, tunaamini wachezaji
wetu wa mpira wa meza na kunyanyua vitu vizito watafanya vizuri kwenye
michezo yao.
“Pia, mabondia, Seleman Kidunda na Emmilian
Patrick watacheza kesho (leo) na hivi sasa (jana mchana) wanashiriki
zoezi la kupima uzito na afya,” alisema Mchume.
Wanariadha Fabiano Joseph na John John Leonard wataanza harakati
za kusaka medali leo katika mbio ndefu, huku Alphonce Simbu, Fabian
Sulle na Wilbaldo Peter watachuana kwenye mita 5,000) kwenye uwanja wa
Hamden Park.
Mara ya mwisho Tanzania kupata medali kwenye
michezo hiyo ilikuwa 2006 nchini Australia ambako ilitwaa medali mbili.
Mwaka 1970 ilitwaa medali ya kwanza kwenye michezo hiyo iliyochukuliwa
na bondia Titus Simba (ambaye sasa ni marehemu).
No comments
Post a Comment