Writen by
sadataley
11:48 AM
-
0
Comments
Na Fidelis Butahe, MwananchiDar es Salaam. Kikao cha mashauriano kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kimeamua kuwa Bunge hilo liendelee kama kawaida Agosti 5, mwaka huu licha ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao vyake.
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza
kwamba mkutano wa Bunge Maalumu utaendelea kama kawaida kwa kuangalia
akidi na iwapo haitatimia wakati wa upigaji kura, wananchi waelezwe
kwamba Ukawa ndiyo wamekwamisha na hivyo hawana nia na Katiba Mpya.
“Kutokana na hali hiyo tumekubaliana kwamba hiyo
Agosti 5, tutaangalia idadi ya wajumbe watakaoripoti bungeni ili kuona
kama akidi itatimia kisha utatolewa ufafanuzi.”
Taarifa hizo zilieleza kuwa kama akidi haitatimia
moja ya mambo yatakayofanywa ni pamoja na Watanzania kuelezwa jinsi
kususa kwa Ukawa kunavyokwamisha mchakato huo.
Sitta aliitisha kikao hicho cha wajumbe 30
wakiwamo viongozi wa Ukawa jana, akisema kilikuwa na lengo la kutathmini
mwenendo wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba na kuangalia ni jinsi
gani wanaweza kuondokana na mgawanyiko uliopo.
Licha ya mwaliko huo, hakuna mjumbe yeyote wa
Ukawa aliyehudhuria, lakini kwa upande wa vyama vya upinzani wajumbe
waliohudhuria ni Peter Mziray wa APPT-Maendeleo na Mbunge wa Wawi (CUF),
Hamad Rashid Mohamed ambaye alisimamishwa uanachama wa chama hicho.
“Uamuzi wao (Ukawa) unaweza kukwamisha mambo mengi
ikiwa ni pamoja na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu 2015.
Ila kifupi vikao vitaendelea na lolote linaweza kutokea. Uamuzi
utategemea na akidi itakayokuwapo,” kilisema chanzo chetu ndani ya
mkutano huo.
Hata hivyo, mjumbe mwingine wa kikao hicho cha
jana alisema: “Unajua katika kikao imeonekana wazi kuwa akidi itatimia
kwa kuwa theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar itatimia tu.”
Habari kutoka katika kikao hicho cha siku mbili
kilichoanza jana saa nne asubuhi na kumalizika saa 8:14 mchana,
zilieleza kuwa mvutano mkali uliibuka kuhusu akidi ya wajumbe kwa ajili
ya kupitisha uamuzi katika Bunge hilo.
Kifungu cha 26 (2) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kinaeleza: “Ili Katiba inayopendekezwa iweze kupitishwa katika
Bunge Maalumu, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya
idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi
mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania
Zanzibar.”
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili Julai 8,
mwaka huu, Sitta alisema iwapo Ukawa watarudi bungeni lakini wakasusa
tena kadri mjadala utakavyoendelea, Bunge litaangalia upya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ambayo inataka theluthi mbili kufanya uamuzi.
Hata hivyo, wazo hilo tayari limepingwa na
wanasheria mbalimbali wakisema suala hilo haliwezekani kwa kuwa Bunge la
Muungano lenye dhamana ya kutunga sheria halitakuwa na kikao hadi
Novemba na kwamba hitaji la mambo ya Muungano kuamuliwa kwa theluthi
mbili ya wajumbe kutoka kila upande si tu la kisheria, bali pia ni la
kikatiba.
Vilevile, mwenyekiti huyo alidokeza kuwa mkutano wa jana
ungekuwa kipimo cha kuwaonyesha Watanzania iwapo Ukawa wako tayari kwa
Katiba Mpya au la.
Taarifa zaidi zilifafanua kuwa hoja ya Ukawa ya
kutaka ijadiliwe Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba nayo iliibuliwa katika kikao hicho jana, lakini ilipingwa kwa
maelezo kuwa Rasimu hiyo inaweza kubadilishwa na si kuboreshwa pekee.
Awali, jana Sitta alisema kuwa atatoa ufafanuzi wa
kilichojadiliwa katika kikao hicho saa 10 jioni, lakini baadaye alituma
ujumbe kwamba atafanya hivyo leo saa tatu asubuhi na baadaye muda huo
ukaongezwa kuwa itakuwa saa tano asubuhi.
Alipoulizwa kama akidi isipotimia nini
kitafanyika, Sitta alisita kujibu swali hilo na kueleza kuwa atakapotoa
ufafanuzi kwa wanahabari atafafanua jambo hilo.
Kwa nyakati tofauti, Rais Jakaya Kikwete na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda wamenukuliwa wakisema kuwa iwapo Katiba Mpya
haitapatikana itaendelea kutumika ya sasa ingawa italazimika kufanyiwa
marekebisho katika maeneo fulani, ambayo hawakuyataja baada ya
maridhiano na pande zote.
No comments
Post a Comment