Latest News

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)

UNIVERSITY OF IRINGA (Formerly Tumaini University-Iringa)
CALL FOR MARCH INTAKE APPLICATION 2017/18
NOW OPEN!
DEADLINE 30/03/2018
CALL 0743 802 615, 0677 048 677Read More

menu

Thursday, July 24, 2014

Katiba Mpya sasa yawekwa njiapanda


Spika wa Bunge la Katiba Samwel Sitta 
Na Waandishi Wetu, MwananchiDar es Salaam. Kikao cha mashauriano kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kinatarajiwa kuanza leo lakini wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wamesisitiza kuwa hawatashiriki.
Wakati Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe akitoa msimamo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema haoni dalili za kupatikana Katiba hiyo kutokana na makundi mawili yaliyopo katika Bunge hilo kuendelea kugawanyika kuhusu idadi ya Serikali katika Muungano, jambo ambalo linaweka njiapanda uwezekano wa kupatikana Katiba Mpya.
Akizungumza jana, Mbowe alisema wajumbe wa umoja huo hawatashiriki kikao cha siku mbili kilichoitishwa na Sitta kwa sababu ni sehemu ya Bunge la Katiba ambalo wajumbe wa Ukawa walisusia vikao vyake tangu Aprili 16.
“Hatutahudhuria wala hatutakwenda katika kikao chochote kinachohusiana na Bunge la Katiba, huo ndiyo msimamo wetu,” alisema Mbowe kwa simu akiwa safarini kwenda Arusha.
Alisema Ukawa wapo katika vikao vya mazungumzo vinavyoratibiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ambavyo alisema ndivyo vitawapa mwelekeo kama watarejea katika Bunge la Katiba au la... “Msimamo wetu ni kuwa hatutashiriki katika Bunge la Katiba mpaka hapo utakapopatikana mwafaka.”
Mbowe alisema Ukawa inaamini kuwa kitakachojadiliwa katika kikao hicho cha Sitta hakitakuwa tofauti na kilichojitokeza katika Bunge la Katiba.
Sitta aliitisha kikao hicho cha wajumbe 30 wakiwamo viongozi wa Ukawa, kwa lengo la kutathmini mwenendo wa vikao vya Bunge hilo na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuondokana na mgawanyiko.
Maalim Seif
Akiwa katika ziara ya kutembelea wanachama wa chama hicho ambao ni wagonjwa katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Maalim Seif alimweleza mwandishi wetu kuwa: “Sioni matumaini ya kupatikana kwa Katiba Mpya kwani makundi mawili yaliyomo katika Bunge hilo yanatofautiana sana, jambo linalonipa shaka endapo Katiba Mpya itapatikana,” alisema na kuongeza:
“Kuna kundi lenye wajumbe wengi la CCM linataka serikali mbili na kundi jingine linajiita Ukawa linatetea maoni ya wananchi lakini makundi haya yanatofautiana sana, kila kundi lina misimamo yake lakini kinachotakiwa ni kuheshimiwa kwa maoni ya wananchi.”
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema ili Katiba Mpya ipatikane, lazima maoni yaliyotolewa na wananchi yaheshimiwe na mjadala ujikite katika rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Jaji Warioba.
Kuhusu Ukawa kuhudhuria kikao cha mashauriano, Maalim Seif alisema: “Ninachojua hawatakwenda kwani wakienda ni sawa wamerejea katika Bunge hilo. Walichokipinga ni kutetea uvunjifu wa utaratibu lakini huyo aliyeitisha kamati hiyo ndiye huyohuyo aliyeongoza Bunge, sasa ukihudhuria kamati hiyo inamaanisha kwamba umerejea bungeni.”
Kauli ya Sitta
Akizungumza baada ya misa ya mazishi ya Profesa na mtafiti wa tiba asilia katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya Muhimbili (MUHAS), Zacharia Mbwambo iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara Dar es Salaam juzi, Sitta alisema kikao kinachoanza leo si cha upatanishi kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakikichukulia bali, ni kwa ajili ya kuweka wazi tofauti zilizopo miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo kabla vikao rasmi havijaanza Agosti 5, mwaka huu.
“Watu wametafsiri vibaya, kikao hiki hakitarajii kufanya usuluhishi wowote kwa kuwa hakuna ugomvi, isipokuwa kujadili na kuweka wazi baadhi ya mambo yanayoonekana kuwa yanakanganya miongoni mwa wajumbe 621 wa Bunge hili,” alisema Sitta.
Akizungumzia msimamo wa Ukawa wa kususia vikao, Sitta alisema aliwataka kufikiria vizuri kwa kuwa kuna vipengele ambavyo havina tatizo kwao, hivyo ni vyema wakarudi bungeni na kuvijadili huku wakivipinga vile wanavyoona haviko sawa kwao.
Kuhusu madai ya kubadili rasimu iliyowasilishwa na Jaji Warioba iliyotokana na mapendekezo ya wananchi, Sitta alisema mchakato wa Katiba Mpya unapitia hatua nyingi na kila moja inaangalia namna ya kuboresha hatua iliyotangulia.
“Rasimu ya Warioba si msahafu ambao hauhitaji kubadilishwa. Kuna baadhi ya vipengele vinataka hivyo na ndiyo maana tunaijadili ili kufika kule tutakako. Kama tume peke yake ingekuwa imemaliza kila kitu kusingekuwa na umuhimu wa Bunge hili. Ni vizuri kila mjumbe akatambua hilo. Iwapo kuna tofauti kama wanavyodai Ukawa, sidhani kama kususia vikao ni jambo mwafaka litakalosaidia kuipata Katiba bora,” alifafanua.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Julius Mathias na Ibrahim Yamola.
« PREV
NEXT »

No comments

Post a Comment