Writen by
sadataley
1:22 PM
-
0
Comments
Na Raisa Said, MwananchiTanga. Rais Jakaya Kikwete amezungumzia nia ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba kutaka kuwania urais mwakani, akisema mwanasiasa huyo kijana “anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha”.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kutoa maoni
yake kuhusu wanachama wa CCM wanaotaka kuwania urais, baada ya chama
hicho kuwaonya makada sita kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kutaka
nafasi hiyo kubwa.
Akiwa jijini London, Makamba alitangaza nia yake
ya kuwania urais mwaka 2015, akisema huu ni wakati wa fikra mpya ambazo
zinahitaji vijana na kwamba wazee wakae kando.
Jana, Rais Kikwete, ambaye alikuwa akihutubia
mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Soni Bumbuli mkoani Tanga
anakoendelea na ziara ya siku tano, alimtaka Makamba “asilazimishe” kwa
kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka.
“Nasikia kuwa bwana mdogo January anataka mambo
makubwa. Mie hajaniambia, na mie nasikia. Hata alipogombea ubunge
hakuniambia nilisikia baadaye... asilazimishe, wakati ukifika atapata,
na akikosa asilete nongwa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alitoa mfano wake mwenyewe
aliposhindwa katika uteuzi wa mgombea urais wa CCM mwaka 1995, wakati
akiwa na miaka 45 (miaka minne zaidi ya umri wa Makamba ifikapo 2015),
akisema kuwa hakukata tamaa na aliendelea kusikiliza ushauri wa wazee
hadi alipofanikiwa kukalia nafasi hiyo ya juu mwaka 2005.
Mwenyekiti huyo wa CCM, ambaye pia ushawishi wake
unaweza kuamua mteule wa chama, alimtaka mbunge huyo wa Bumbuli
asikilize ushauri wa wazee.
Pamoja na ushauri huo kwa mwandishi wake wa zamani
wa hotuba, Rais Kikwete alimpongeza kwa kazi nzuri ya ubunge jimboni
humo na akaeleza kuwa anamsaidia katika wizara yake.
Alinukuu maneno ya aliyekuwa katibu mkuu wa Afro
Shiraz na swahiba wake, Thabit Kombo aliyemwambia Kikwete kuwa “wakati
ukifika utapata”, hasa kutokana na kiu yake ya muda mrefu ya kuwatumikia
Watanzania.
“Nilipokosa mwaka 1995 sikukata tamaa, ndipo 2005
nikaingia, na huo ndio ulikuwa wakati wangu wa kushika wadhifa huu.
Wakati ukifika watu watake wasitake utakuwa wewe tu,” alisema Kikwete.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja takriban wiki
moja baada ya Makamba kueleza nia yake ya kuwania urais akisema kwa
asilimia 90 ameshaamua kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Mbunge huyo wa Bumbuli, ambaye ni mtoto wa Katibu
Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba, alitangaza uamuzi huo akiwa
Uingereza alikokuwa akihudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya
kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na baadaye
kufafanua nia hiyo katika mahojiano na gazeti hili.
Rais Kikwete akimshauri asikilize ushauri wa wazee, wakati
akitangaza nia hiyo Makamba alisema: “Ni wakati wa fikra mpya kushika
dola na mimi ninaona kwamba wazee wakae kando. Mfano awamu moja
inapoondoka na wazee walioko katika mfumo wakae kando ili kupisha fikra
mpya kuongoza dola.” alisema Makamba ambaye kwa sasa ana miaka 40.
Makamba ameendelea kusisitiza nia yake hiyo na
kutetea nafasi ya vijana katika nafasi hiyo kwenye ukurasa wake wa
facebook akisema: “Tanzania mpya inahitaji viongozi wapya, mazoea mapya,
fikra mpya na maarifa mapya. Inahitaji kuthubutu mambo makubwa siyo
kulinda uzoefu wa nyuma.”
Makamba ni mmoja wa makada sita wa CCM walioonywa
na chama hicho mapema mwaka huu kwa kutuhumiwa kuanza mapema kampeni za
urais kinyume na utaratibu, lakini chama hicho hakijaona kasoro katika
uamuzi wake wa kutangaza nia.
CCM yambariki
Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kimebariki mbio za Makamba baada ya jana kueleza kuwa hajafanya kosa
lolote kwa kutangaza nia yake.
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema alichofanya Makamba ni tofauti na adhabu ambayo chama hicho
kilimpa yeye na wenzake watano miezi mitano iliyopita.
Nape aliwataka wanaohoji suala hilo kurejea adhabu
iliyotolewa na CCM, Februari 18, mwaka huu kwa makada wake sita baada
ya kukutwa na makosa ya kuanza mapema kampeni za urais mwaka 2015,
akiwamo Makamba.
Wengine waliokutwa na rungu hilo ni mawaziri wakuu
wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Waziri wa Mambo ya Nje,
Bernard Membe na William Ngeleja.
“Hili jambo linakuzwa tu wakati katika barua
tulizowapa tulieleza wazi. Waambie wawaonyeshe barua ambazo chama
kimewapa ili mjue nini ambacho hawatakiwi kukifanya,”alisema Nape.
“Yeye amesema akipewa ridhaa ya kugombea urais,
jambo hili halipo kati ya makosa ambayo yalisababisha yeye na wenzake
kupewa adhabu.”
Februari 18, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM ilitoa
adhabu kwa makada hao baada ya kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta
kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na
uaadili za chama hicho.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip
Mangula aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wana-CCM kutangaza mapema nia
ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema
ni wasaliti wakubwa ndani ya chama.
CCM pia ilitoa mwongozo na kanuni za uchaguzi ambazo Ibara 6 (2)
(1-5) ya Maadili ya Viongozi wa CCM inawazuia wanachama kutoa michango,
misaada, zawadi za aina yoyote, kukusanya michango na kufanya kampeni
bila ya kupata kibali kutoka kamati ya siasa ya halmashauri ya eneo
husika.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kanuni za uongozi na
maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i), ni kinyume kwa
wanachama wake kutafuta kuteuliwa kuwania urais kabla ya wakati.
No comments
Post a Comment