Writen by
sadataley
11:02 AM
-
0
Comments
Na Ibrahim Yamola na Elias Msuya, MwananchiDar es Salaam. Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ametangaza nia yake ya kuwania urais akisema huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola, licha ya chama hicho kuzuia kutangaza nia na kupiga kampeni kabla ya muda.
Makamba, mmoja wa makada wa CCM walioonywa na
chama hicho baada ya kutuhumiwa kuanza kampeni mapema, alijipigia debe
kuwa iwapo atapitishwa na chama hicho, ataelekeza nguvu kwenye
vipaumbele vyake vinne ambavyo ni ajira, huduma za jamii, uchumi imara
na utawala bora.
Mbunge huyo wa Bumbuli alisema hayo akiwa
Uingereza anakohudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya
kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza na baadaye kufafanua nia
hiyo katika mahojiano na Mwananchi jana.
“Ni wakati wa fikra mpya kushika dola na mimi
ninaona kwamba wazee wakae kando. Mfano awamu moja inapoondoka na wazee
walioko katika mfumo wakae kando ili kupisha fikra mpya kuongoza dola,”
alisema Makamba ambaye ana umri wa miaka 40.
Mwandishi huyo wa zamani wa hotuba za Rais Jakaya
Kikwete, alisema hadi sasa ameshafanya uamuzi kwa asilimia 90 kujitokeza
kuwania nafasi hiyo ya juu kuliko zote nchini, bado asilimia 10 katika
baadhi ya mambo ambayo anaendelea kuyatafakari, kuzungumza na makundi
mbalimbali ya wazee, viongozi wa dini na viongozi waliopita “ili nipate
ushauri wao kuhusu namna ya kufanya jambo hili”.
Alipoulizwa iwapo ameshawishiwa au kushinikizwa na watu au ni utashi wake binafsi, Makamba alisema kuwa yote ni mchanganyiko.
“Huwezi kuamka nyumbani na kusema unakwenda
kugombea. Kuna msukumo wa wapambe wachache ambao ni lazima ukapime kwa
makini kabla ya kuchukua hatua yeyote,” alisema.
“Nchi nzima unakuta inazungumza uwe rais, lazima
upime na chagizo hizo ni za kweli au zinatoka wapi. Lakini unaposikia
hadi viongozi wa dini, wanafunzi wa vyuo unapokwenda wanakuuliza jambo
hilo hilo, unatakiwa utafakari.”
Aliongeza: “Mfano unakwenda Maswa (Shinyanga),
Liwale (Lindi), Simanjiro (Kilimanjaro), Wete (Pemba) unaambiwa unafaa,
ni muhimu katika hili lakini pia wazee, vijana, viongozi wa dini
wanasema unafaa kuwaunganisha Watanzania wote ni jambo la kulitafakari
na kulichukulia hatua.”
Februari mwaka huu, Kamati Kuu ya CCM iliwapa onyo
kali makada wake sita akiwemo January Makamba ikiwatuhumu kupiga
kampeni za urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao kabla ya muda.
Makada wengine waliopewa adhabu hiyo ni mawaziri
wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowasa, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na mbunge wa Sengerema,
William Ngeleja.
Pia makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula
aliwahi kukemea tabia ya baadhi ya wana-CCM kutangaza mapema nia ya
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi ujao, akisema ni
wasaliti wakubwa ndani ya chama.
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/January--Nagombea-urais-2015-kutekeleza-vipaumbele-vinne/-/1597296/2371534/-/10b8qe9/-/index.html
Kwa habari zaidi ingiahttp://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/January--Nagombea-urais-2015-kutekeleza-vipaumbele-vinne/-/1597296/2371534/-/10b8qe9/-/index.html
No comments
Post a Comment