Writen by
sadataley
11:05 AM
-
0
Comments
Na Beatrice Moses na Habibu Uwezo, Mwananchi Dar es Salaam. Jaji mstaafu Mark Bomani amelishauri Bunge Maalumu la Katiba kuweka kando suala la muundo wa serikali kwa kuwa ndiyo chanzo cha mgawanyiko mkubwa baina ya wajumbe.
Pia amewashauri wajumbe wa Bunge hilo wanaounda
kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurejea bungeni ili
mchakato huo uweze kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar
es Salaam, Jaji Bomani alisema suala la muundo wa Serikali licha ya
kusababisha mgawanyiko limesababisha hoja nyingine muhimu kusahaulika.
“Kwa bahati mbaya sana kwa maoni yangu, mjadala wa
mapendekezo hayo umezua malumbano na ubishi mkali, kiasi cha kufanya
baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kujitoa,” alisema Jaji Bomani.
Alisema amewahi kutoa maoni kwamba suala lote la
muungano na idadi ya Serikali linatakiwa lijadiliwe kwanza ama na
Serikali mbili zilizopo, yaani Zanzibar na ya Muungano au Wazanzibari
waulizwe iwapo wanautaka muungano.
“Hata hivyo nina wasiwasi kama mwafaka au
maridhiano yatapatikana mwezi Agosti Bunge Maalumu litakapokutana, kwa
kuwa zimejitokeza tofauti kubwa za kimtazamo au kiitikadi bila kusahau
masilahi binafsi,” alisema Jaji Bomani.
Alisema kwa uzoefu wake katiba nzuri kwa nchi yoyote ni ile ambayo imepatikana kwa wananchi wengi kuikubali na siyo vinginevyo.
“Katiba nzuri ni ya maridhiano. Katiba nzuri
haiwezi kupatikana kwa wingi wa kura au hoja ya nguvu tu bali inatakiwa
iwe inakubalika na walio wengi (consensus),” alisema.
Aliyataja mambo mengine muhimu ambayo yanapaswa
kujadiliwa na wajumbe kuafikiana ni pamoja na suala la uwakilishi sawa
wa jinsia yaani asilimia 50 kwa 50, kwenye ubunge na halmashauri za
wilaya.
“Suala la mawaziri kutokuwa wabunge nalo pia
nafikiri linaweza kujadiliwa na mwafaka ukapatikana, muundo wa tume huru
ya uchaguzi na suala la mgombea binafsi nalo naamini linajadilika
wanaoliogopa hawana msingi wa kufanya hivyo,” alisisitiza Jaji Bomani.
No comments
Post a Comment