Writen by
sadataley
11:39 AM
-
0
Comments
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2014/15 kutangazwa bungeni mjini Dodoma, baadhi ya wachumi wamesema Watanzania wasitarajie chochote kipya katika bajeti hiyo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti,
baadhi ya wataaamu wa masuala ya uchumi wamesema, fedha nyingi huenda
zitaelekezwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2015, ukarabati wa miundombinu na
kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya.
Waziri wa Fedha, Saada Nkuya Salum kesho saa 10.00
jioni atawasilisha Bajeti Kuu ya Serikali, ikiwa ni ya tisa tangu
kuingia madarakani kwa Rais Jakaya Kikwete, lakini ikiwa ni bajeti yake
ya kwanza akiwa waziri kamili.
Nkuya aliyechukua nafasi ya mtangulizi wake,
marehemu William Mgimwa, amejikuta mwenye changamoto kubwa kutokana na
Serikali kushindwa kupata fedha za kutekeleza makadirio ya matumizi
yaliyoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2013/14, hivyo
kuamsha hasira za wabunge ambao wanataka pengo hilo lifidiwe katika
bajeti itakayotangazwa kesho.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk
Prosper Ngowi alisema bajeti haitakuwa na matumaini kwa sababu fedha
nyingi zitatumika katika ujenzi wa mindombinu iliyoharibiwa na mvua
kubwa zilizonyesha mwaka huu.
Mbali na kugharimia miundombinu, Dk Ngowi alisema
fedha za bajeti, pia zitatakiwa kugharimia mchakato wa Katiba Mpya na
uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Haya ni mambo muhimu ambayo ni lazima yafanyike
katika bajeti ya mwaka huu, barabara zimebomoka hatuwezi kuziacha,
mchakato wa Katiba Mpya lazima uendelee na uchaguzi ufanyike,” alisema
Dk Ngowi.
Alisema bajeti ijayo inatakiwa kufidia fedha za maendeleo ambazo zimepungua katika bajeti inayomalizika June 30, mwaka huu.
Alisema kwa ukusanyaji wa mapato ulivyo na upungufu anaona bajeti hii itakuwa ngumu na isiyo na matumaini kwa Watanzania.
“Mwaka huu tunatakiwa `kukuna vichwa’ kwa sababu
bado tuna deni la bajeti iliyopita ili tuiunganishe na hii ya sasa.
Tunachotakiwa kujiuliza tutapata wapi fedha hizo?” aliuliza.
Naye Mhadhiri wa Shule ya Biashara katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Omar Mbura alisema kutokana na
upungufu wa fedha katika bajeti ya mwaka huu, miradi hiyo inapaswa
kupewa fedha katika bajeti ijayo. Alisema Serikali inapaswa kubadilisha
mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuzishirikisha ngazi za chini za
uongozi kama vile vijiji.
“Serikali itafute vyanzo vya mapato hata kama
itakuwa ni gharama kubwa kufanya hivyo,” alisema na kuongeza kuwa hivi
sasa ni wakati mwafaka wa kufutwa kwa misamaha ya kodi, kwani
inakwamisha maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisema bajeti ya mwaka huu itakuwa ngumu kwa wananchi kwa sababu ya uchaguzi.
Kwa upande wake Profesa Ibrahim Lipumba alisema bajeti ya mwaka huu itakuwa ngumu kwa wananchi kwa sababu ya uchaguzi.
“Wananchi wasitarajie mambo mazuri katika bajeti
hii, kuna uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Septemba mwaka huu
na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2015, fedha zitatoka katika bajeti
hii,” alisema Profesa Lipumba.
Msomi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF,
alisema bila Serikali kuchukua uamuzi mgumu wa kufuta misamaha ya kodi,
kuongeza vyanzo vya mapato na kuziba mianya ya kukwepa kodi, wananchi
wasitarajie mapya.
“Serikali isipofanya hivyo tutaendelea kuwa na
bajeti zisizotekelezeka. Tunatenga bajeti ya fedha tusizokuwa nazo,
matokeo yake miradi ya maendeleo itakuwa inakwama mwaka hadi mwaka,”
alisema.
Alisema misamaha ya kodi na wakwepa kodi ndiyo
wanaoitafuna nchi hii na kwamba hao ndiyo wanaosababisha hata miradi ya
maendeleo ishindwe kutekelezwa.
“Tunahitaji mabadiliko kama tunahitaji katika
masuala ya kodi, inasikitisha tunakuwa na upungufu wa fedha katika
bajeti lakini tunasamehe kodi, hili ni jambo la ajabu,” alisema Lipumba.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa
Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samwel Wangwe alisema serikali ibuni
vyanzo vipya vya mapato kwani utaratibu wake wa kupandisha kodi katika
bidhaa zilezile umepitwa na wakati.
“Kila mwaka katika bajeti bidhaa kama sigara, soda
na bia zimekuwa zikipandishiwa kodi, utaratibu huu ukiendelea watu
watashindwa kumudu bei ya bidhaa hizo,” alisema.
Profesa Wangwe alisema wananchi wakikosa uwezo wa
kununua bidhaa hizo kwa sababu ya bei kubwa Serikali itakosa mapato,
hivyo alipendekeza misamaha ya kodi ifutwe ili kuiongezea Serikali
iongeze uwezo wa kujiendesha badala ya kutegemea wahisani.
“Nashauri bajeti ziwe zinapangwa kulingana na
uwezo wetu wa kifedha, miradi ya maendeleo nayo tuiendeleze kulingana na
uwezo wetu badala ya kuwa na miradi mingi ambayo haimaliziki,” alisema
Wangwe.
No comments
Post a Comment