Writen by
sadataley
6:52 PM
-
0
Comments
Na Joseph Zablon, Mwananchi
Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya
waombolezaji katika mazishi ya msanii wa kuigiza na vichekesho, Saidi
Ngamba ‘Mzee Small’ aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mzee Small kwa zaidi ya miaka miwili alikuwa
akisumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi, alizikwa jana katika makaburi ya
Segerea na mamia ya waombolezaji wengi wao wakiwa wasanii wa fani
tofauti.
Rais Kikwete aliwasili nyumbani kwa marehemu
Tabata Kisiwani kunako saa 8:30 za mchana na kukaa kwa zaidi ya nusu saa
akizungumza na wanafamilia kabla ya kuaga na kuondoka ili kuruhusu
taratibu zingine za mazishi kuendelea.
Wakimuelezea marehemu Mzee Small ambaye ameacha
mke na watoto sita mara baada ya mazishi katika makaburi ya Segerea ,
baadhi ya wasanii walisema kuwa marehemu alikuwa mfano mzuri na dira kwa
walio wengi katika fani hiyo.
“Tutamkumbuka mwa mengi, lakini kubwa ni mapenzi
katika kazi yake, aliipenda sana fani yake na alikuwa tayari wakati
wote” alisema Yusuf Kaimu ‘Pembe’ na kuongeza kuwa alikutana na marehemu
kwa mara ya kwanza katika kikundi cha Sanaa cha Reli kilichokuwa
kinamilikiwa na Shirika la Reli (TRC) miaka ya themanini.
Pembe alisema kuwa marehemu alikuwa mcheshi na
mpenda na mwenye mzaha mwingi, lakini hakuwa na simile pale unapokuwa
unataka kuharibu kazi na daima alikuwa mwongozaji na rafiki wa wengi.
Ulimboka Mwakalasa ‘Senga’ alisema kuwa Mzee Small
alikuwa dira ya fani yake ingawa hakuwahi kufanyakazi nao kwa muda
mrefu, lakini daima alikuwa anamfuata nyuma katika kazi yake.
Mtoto wa Mzee Small, Mahmood Saidi alisema kuwa
baba yake alizidiwa siku ya Jumamosi asubuhi alikuwa akikohoa na
kutapika damu na walimkimbiza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Alisema kuwa Alifanyiwa kipimo cha CT-Scan na kubainika kuwa ana uvimbe kama wa kuvia kwa damu kichwani.
No comments
Post a Comment