Writen by
sadataley
1:22 PM
-
0
Comments
Na Habel Chidawali na Sharon Sauwa, Mwananchi
Dodoma. Kwa maneno ya siku hizi ni kwamba Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema ‘amelikoroga na kulinywa mwenyewe’, baada ya jana kutoa kauli ya kuudhi alipomtaka mbunge kutoka Zanzibar akaulize swali lake visiwani humo, iliyosababisha baadhi ya wabunge kususia Bunge na kutoka.
Kauli iliyoonyesha kuwagawa wabunge katika mafungu
mawili; wa bara na Zanzibar, ilimlazimu Jaji Werema baadaye kusimama
bungeni na kuwaangukia akiwaomba radhi waliokerwa na kauli yake na pia
kuliomba radhi Bunge, Spika wake, Anne Makinda na wananchi.
Kuondoka kwa wabunge hao kulitokana na mwongozo wa
Spika ulioombwa na Mbunge wa Ole (CUF), Rajabu Mbarouk Mohamed kutokana
na majibu Jaji Werema kwa mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habibu Mnyaa
aliyekuwa ameomba ufafanuzi wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya
kupitisha vifungu vya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Katiba na Sheria kwa mwaka 2014/15.
Mnyaa alisema Wizara ya Katiba na Sheria ni muhimu
lakini imekuwa ndiyo ya kwanza kuvunja sheria na haki za binadamu na
akataka ufafanuzi.
Hata hivyo, aliposimama kujibu swali hilo, Jaji
Werema alimwambia Mnyaa kuwa mambo mengine akaulize Zanzibar na siyo
katika Bunge la Jamhuri kwa kuwa si kila kitu kitaulizwa ndani ya Bunge
hilo.
“Alichokizungumza Mnyaa ni sahihi lakini hapa si
mahali pake, namshauri kuwa akaulize huko Zanzibar kwenye vikao vyao
hapa sisi hatuna majibu,” alisema Werema.
Mara baada ya Bunge kurejea, Mbarouk aliomba mwongozo wa Spika akitaka ufafanuzi wa kauli hiyo kwamba ilikuwa ya kibaguzi.
“Mheshimiwa Spika, huu ni ubaguzi na haupaswi kufanywa na mtu msomi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alisema Mbarouk.
Alisema ubaguzi huo umewabagua wabunge ambao
wamekula kiapo cha kulitumikia Bunge la Jamhuri ya Muungano na
unaonyesha namna ambavyo Wazanzibari wanabaguliwa.
“Mheshimiwa Spika, yanapofanyika mambo kama hayo
na wewe mwenyewe uko hapa unaona ni sawa na kubariki jambo hilo, huu ni
ubaguzi unaoufanya wewe kwa kuwa lilifanyika ukiona bila hata ya
kukemea,” alisema Mbarouk.
Hata hivyo, Spika alipinga na kusema: “Hakuna
mwongozo wowote kwa kuwa hata wewe umevunja sheria kwani hata
nilipokuambia kaa chini umeendelea kuzungumza, tunaendelea.... Katibu
(akimtaka Katibu wa Bunge kutoa mwelekeo wa shughuli iliyokuwa inafuata
ambayo ilikuwa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Nchi).”
Baada ya kauli ya Spika, wabunge wa Zanzibar
walihamasishana na kuamua kutoka nje kwa wakati mmoja na huku wenzao wa
upinzani wakiendelea kutafakari cha kufanya. Wakati huo, Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alikuwa akisoma hotuba yake.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Werema-alikoroga--alinywa/-/1597296/2316522/-/3swsoz/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Werema-alikoroga--alinywa/-/1597296/2316522/-/3swsoz/-/index.html
No comments
Post a Comment