Writen by
sadataley
3:27 PM
-
0
Comments
Polisi wakijitahidi kudhibiti umati wa watu waliofika kushuhudia eneo
lililotokea mlipuko wa Guruneti nje kidogo ya jiji la Nairobi nchini
Kenya jana.Takribani watu 10 wanahofiwa kufariki na 70 kujeruhiwa.Picha
na Tony Karumba
Na Na Mwandishi Wetu
Nairobi. Watu 10 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 70
kujeruhiwa baada milipuko miwili kutokea karibu na soko kubwa la nguo la
Gikomba mjini Nairobi.
Kuna uwezekano idadi hiyo ya watu waliofariki dunia ikaongezeka kutokana na hali ya baadhi ya majeruhi kuwa mbaya.
Milipuko hiyo imetokea siku moja baada ya nchi za
magharibi ikiwamo Uingereza kuwataka raia wake wanaoishi nchini humo
kurejea nyumbani kwa hofu ya usalama.
Jeshi la polisi limesema kuwa linamshikilia mtu
mmoja kwa madai ya kuhusika kwenye tukio hilo na hakuna taarifa zaidi
zilizotolewa.
Msemaji wa Hospitali ya Kenyatta aliliambia
Shirika la Habari la AFP kuwa baadhi ya majeruhi waliopelekwa
hospitalini hapo hali zao ni mbaya.
Mfanyabiashara mmoja aliyekuwepo kwenye eneo la
tukio alisema kuwa alisikia mlio mkubwa uliofuatiwa na moshi uliotanda
eneo lote la soko na kwamba baada ya tukio hilo watu wengi walikimbia
ovyo kuokoa maisha yao.
“Watu wengi wamejeruhiwa. Sijui idadi ya watu
waliopoteza maisha, lakini kusema kweli mlipuko huu ni mkubwa na utakuwa
umeleta madhara makubwa,” alisema Mwangi Maina.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na tukio
hilo, lakini wachunguzi wa mambo wanalitaja Kundi la Al-Shabaab kuwa
huenda likawa nyuma ya matukio hayo.
Kenya imekuwa ikiandamwa na matukio ya kigaidi
tangu ilipopeleka askari wake nchini Somalia kukabiliana na kundi lenye
msimamo mkali wa Kiislamu, Al-Shabaab.
Taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya nchi
za magharibi zinasema kuwa zaidi ya watu 100 wamepoteza maisha katika
kipindi cha miezi 18 iliyopita tangu Kenya ianze kuandamwa na
mashambulizi ya kigaidi.
Milipuko hiyo imekuja huku raia wengi wa kigeni
waliokuwa nchini Kenya kwa shughuli za utalii wakiwa wanarejea nyumbani
kuitika wito uliotolewa na serikali zao.
Tahadhari hiyo kutoka kwa Serikali ya Uingereza
ilieleza kuwa askari wa Al-Shabaab, huenda wakafanya mashambulizi nchini
Kenya katika muda wowote kuanzia sasa.
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Watu-10-wafa-katika-mlipuko-wa-bomu/-/1597296/2318040/-/1s09ntz/-/index.html
Kwa habari zaidi ingia http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Watu-10-wafa-katika-mlipuko-wa-bomu/-/1597296/2318040/-/1s09ntz/-/index.html
No comments
Post a Comment