Writen by
sadataley
12:12 PM
-
0
Comments
Na Florence Majani, Mwananchi
Dar es Salaam. Homa ya dengue inaendelea
kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari hadi juzi kutoka Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu 376 wamekwishagundulika
kuugua ugonjwa huo.
Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa wizara
hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema hadi jana watu wawili walikuwa
wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema inaweza kuwa kubwa zaidi endapo
upimaji utafanyika katika kila wilaya. “Pengine idadi inaweza kuwa kubwa
zaidi kwa sababu wengi hawapimwi, Ijumaa (kesho) tutatoa, taarifa
zaidi,” alisema.
Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa wengi
zaidi, ikifuatiwa na Ilala na Temeke. Hata hivyo, alisema huenda wilaya
zenye idadi ndogo ya wagonjwa hazijaweza kupima na kubaini watu wenye
maradhi hayo ikilinganishwa na Kinondoni.
Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif
Rashid alisema hali ni mbaya na wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari
wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtafiti wa malaria, tabia za mbu na mazingira, wa
Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Nicholas Govela alisema tayari
wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa kina kuwajua mbu wanaoeneza
homa ya dengue nchini. “Utafiti huu utasaidia kujua ni mbu kiasi gani
wameathirika na virusi hivyo. Tukifanya hivyo tutajua ukubwa wa tatizo,
tutajua wanapatikana wapi zaidi na virusi vyao vimetokea wapi,” alisema.
Dk Govela alisema ni lazima utafiti huo ufanyike
ili kudhibiti maambukizi zaidi ya homa hiyo akisema zipo sababu kadhaa
zinazohisiwa kusababisha maradhi hayo, ikiwamo ya wahamiaji kuleta
virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kuambukizwa kwa njia ya
kuumwa na mbu.
“Ugonjwa huu umeenea zaidi nchi za Amerika ya
Kusini na Kusini mwa Bara la Asia. Hapa kwetu mbu hawa walikuwapo lakini
ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa kiasi hiki, ndiyo maana sababu
zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji,” alisema.
Alisema maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada
ya mtu mwenye ugonjwa huo kuumwa na mbu hao aina ya Aedes Egyptiae na
mbu hao wakichukua virusi, huvisambaza kwa watu wengine. “Inawezekana
tatizo ni kubwa zaidi ya hivi inavyofikiriwa kwa sababu wanaokuja
hospitali kupimwa na kugundulika ni wachache, wengi wasiofika hawawezi
kujulikana,” alisema.
Makazi duni hatarini zaidi
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue,
Mrisho Rupinda alisema watu wanaoishi katika makazi duni wapo hatarini
kuathiriwa zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa taka nyingi na madimbwi.
Alitoa mfano wa wagonjwa wa kwanza wilayani
Kinondoni, akisema walitokea maeneo ya Kambangwa, Mwananyamala Komakoma
ambako kulikuwa na madimbwi na bwawa la maji.
“Wagonjwa wengi huonekana zaidi kwenye makazi duni
kwa sababu ya mpangilio mbovu na kuzagaa kwa taka. Lakini pia maeneo
mengine ambayo watu huhifadhi maji kwenye matenki au ndoo kwa muda mrefu
bila kuyafunika,” alisema.
No comments
Post a Comment